Jumapili, 25 Disemba, 2016
Leo ni Jumapili tarehe 25 Rabiul Awwal inayosadifiana na Tarehe 25 Disemba 2016.
Siku kama ya leo miaka 2017 iliyopita, Nabii Issa Masih (AS) alizaliwa katika mji wa Bait Laham (Bethlehem) huko Palestina. Nabii Issa Masih alipewa uwezo na Mwenyezi Mungu wa kufanya miujiza mingi. Issa Masih AS alianza kuzungumza akiwa mdogo na kujibashiria unabii. Mwenyezi Mungu anaashiria tukio la kuzaliwa kwa Nabii Issa katika Qur'ani Tukufu katika Suratu Aal Imran aya ya 45 kwa kusema: Kumbukeni waliposema Malaika: "Ewe Mariam! Mwenyezi Mungu anakubashiria mwana kwa neno litokalo kwake; jina lake ni Masih, Issa mwana wa Maryam, mwenye hishima katika dunia na Akhera na miongoni mwa waliokurubishwa." Inafaa kuashiria hapa kwamba, tarehe 25 Disemba kila mwaka inajulikana kote duniani hasa kwa Wakristo kuwa ni Sikukuu ya Krismasi. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa wafuasi wa kweli wa Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu.
Miaka 373 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 25 Disemba 1643 alizaliwa Isaac Newton, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika na alitambuliwa kama mwanasayansi mkubwa aliyepata umashuhuri. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy. Ugunduzi wa Isaac Newton ulikuwa msingi mkuu wa ugunduzi wa wasomi wengine kuhusu kanuni kuu za hisabati na uhandisi.
Tarehe 25 Disemba 1665, Ufaransa ilianzisha French East India Company katika kipindi cha utawala wa Mfalme Louis II ili kushindana kisiasa, kiuchumi na kikoloni na serikali ya Uingereza huko India. Uingereza ilikuwa imeasisi British East India Company miaka 66 kabla ya hapo. Vilitokea vita kadhaa baina ya tawala hizo mbili za kikoloni kwa shabaha ya kuikoloni ardhi ya India.
Miaka 140 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alizaliwa Muhammad Ali Janah, mpigania uhuru mashuhuri wa Bara Hundi na mwasisi wa Pakistan. Janah alizaliwa mwaka 1876 katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistan. Muhammad Ali Janah alikuwa miongoni mwa shakhsiya wakuu walioasisi chama cha Muslim League mnamo mwaka 1906. Chama cha Muslim League awali kilikuwa kikijishughulisha na masuala ya kitamaduni na kidini, lakini baadaye kikaingia katika uwanja wa siasa na kutaka kuundwa nchi huru kwa ajili ya Waislamu.
Tarehe 25 Disemba miaka 39 iliyopita alifariki dunia msanii mashuhuri na mcheza filamu za kuchekesha Charlie Chaplin. Sir Charles Chaplin anatambuliwa kuwa mtayarishaji, mchezaji na mtengeneza filamu mkubwa wa Holywood na mshindi wa tuzo ya Oscar. Filamu nyingi za msanii huyo ni za vichekesho na za kimyakimya zisizo na sauti. Alifanya kazi katika tasnia ya filamu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 65 na alianza kazi hiyo katika ukumbi wa Victoria nchini Uingereza akiwa mtoto hadi alipokamilisha umri wa miaka 88. Mwaka 1919 Charles Chaplin na wenzake kadhaa walianzisha Jumuiya ya Filamu. Msanii huyo mashuhuri alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 88 kutokana na maradhi ya kisukari.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita inayosadifiana na tarehe 25 Disemba 1979, viongozi watatu wa ngazi za juu wa Palestina waliuawa kigaidi na Shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD. Viongozi hao walikuwa Ali Hassan Salamah, afisa wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliyeuawa Beirut baada ya kutegwa bomu ndani ya gari lake, Samir Touqan mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya PLO huko Cyprus na Ali Nasser Yassin, shakhsia mwingine wa Palestina aliyekuwa mwakilishi wa PLO nchini Kuwait. Jinai hiyo ilidhihirisha tena jinsi utawala katili wa Israel unavyotumia ugaidi katika maeneo mbalimbali dunia kwa ajili ya kufikia malengo yake haramu.
Tarehe 5 Dei mwaka 1382 Hijria Shamsia yaani siku kama hii la leo miaka 13 iliyopita mtetemeko wa ardhi uliokuwa na nguvu ya 6.8 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika mji wa Bam huko kusini mwa Iran na maeneo ya kandokando yake. Mtetemeko huo wa kutisha wa ardhi uliharibu sehemu kubwa ya mji huo na kusababisha vifo vya watu elfu 41. Makumi ya maelfu ya watu wengine pia walijeruhiwa. Maafa ya mtetetemo huo wa ardhi yalikuwa makubwa mno kwa kadiri kwamba, baadhi ya jumuiya na taasisi za kimataifa zilijiunga na wananchi na serikali ya Iran katika kutoa misaada ya dharura kwa waathiriwa. Mbali na hasara za nafsi na vifo vya maelfu ya watu, mtetemeko wa ardhi wa Bam ulisababisha pia hasara kubwa za kiuchumi na kuharibu jengo la kale la Arge Bam.
Na siku kama ya leo miaka 1002 iliyopia alifariki dunia Ali Bin Hussein Baghdadi maarufu kama Sayyid Murtadha Alamul Huda fakihi na alimu mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 355 Hijiria huko Baghdad na alijifunza elimu za fasihi ya Kiarabu, mantiqi na mashairi na kwa miaka 30 alihukumu mjini Baghdad. Sayyid Murtadha ameacha vitabu vingi na miongoni mwa vitabu hivyo ni Tanzihil Anbiyah, Taqribul Usul pamoja na kitabu cha maashairi chenya beti elfu 20.