Jul 22, 2017 02:27 UTC
  • Jumamosi, Julai 22, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 27 Mfunguo Mosi Shawwal 1438 Hijria, mwafaka na tarehe 22 Julai mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 404 iliyopita, Mikhail Ramanov alikalia kiti cha utawala wa Russia na kwa utaratibu huo, utawala wa miaka 304 wa familia ya Ramanov ukawa umeanza nchini humo. Miaka mitatu baada ya mashambulio ya vikosi vya Poland dhidi ya Russia, mmoja wa makamanda wa Kirusi alifanikwa kuvishinda vikosi hivyo na kuudhibiti mji wa Moscow. Baada ya jeshi la Poland kufukuzwa nchini humo, Mikhail Ramanov akashika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Katika kipindi cha utawala wa familia ya Ramanov, Russia ilipanuka lakini kwa upande wa uchumi haikupiga hatua kubwa. ***

Mikhail Ramanov

Katika siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, kulitokea vita maarufu vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Isonzo. Vita hivyo vilitokea sambamba na kujiri Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Vita vya Isonzo vilitokea katika maeneo ya milimani yaliyojulikana kwa jina hilo hilo nchini Italia. Vita hivyo vilikuwa baina ya jeshi la Italia lililokuwa katika safu ya waitifaki na Austria iliyokuwa upande wa Ujerumani. Watu wapatao 70,000 wengi wao wakiwa ni Wataliano waliuliwa katika vita hivyo. Pamoja na hayo, jeshi la Italia lilipata ushindi dhidi ya jeshi la Austria katika vita hivyo vya Isonzo. ***

Vita vya Isonzo

Tarehe 31 Tir mwaka 1331 Hijria Shamsia yaani miaka 65 iliyopita, Mahakama ya Kimataifa ya The Hague Uholanzi, ilitoa hukumu ya kutupilia mbali mashtaka ya Uingereza dhidi ya Iran kuhusiana na kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kufanywa kuwa mali ya taifa. Bunge la Taifa la Iran tarehe 29 Isfand mwaka 1329 Hijria Shamsia lillikuwa limeitangaza sekta ya mafuta ya Iran kuwa mali ya taifa na kwa utaratibu huo, likawa limekata mikono ya serikali ya Uingereza iliyokuwa ikinufaika na mafuta ya Iran. Uingereza ambayo ilikuwa ikipata faida kubwa kutokana na kupora utajiri wa mafuta wa Iran iliamua kushtaki katika Mahakama ya The Hague. Hata hivyo katika siku kama ya leo, mahakama hiyo ilitupilia mbali mashataka hayo ya Uingereza ***

Mahakama ya Kimataifa ya The Hague

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 22 Julai 1961, yalianza mapigano makali kati ya majeshi ya Ufaransa na Tunisia, baada ya vikosi vya Ufaransa kuushambulia mji wa kihistoria wa Bizerte ulioko kaskazini mashariki mwa Tunisia. Mara baada ya Tunisia kujitawala kutoka kwa mkoloni Mfaransa mwaka 1956, mkoloni huyo aliendelea kuikalia kwa mabavu bandari ya Bizerte, na kuifanya kuwa kambi ya jeshi la anga la nchi hiyo. Hata hivyo majeshi ya Tunisia yalifanikiwa kuikomboa bandari hiyo kwenye mapigano hayo makali yaliyopelekea Watunisia 750 kuuawa. ***

Bizerte

Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, jeshi la mtawala wa wakati huo wa Iraq, dikteta Saddam Hussein lilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya maeneo ya kusini ya Iran. Mashambulio hayo yalianza siku nne tu baada ya Iran kulikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lililokuwa limepasishwa takribani mwaka mmoja kabla, lilisisitiza juu ya usitishaji vita, liliuarifisha  utawala vamizi, likataka kulipwa fidia waathiriwa wa hujuma hiyo, kubadilishana mateka mataifa mawili ya Iran na Iraq na kurejea vikosi vya nchi mbili hizo katika mipaka ya kimataifa. Utawala vamizi wa Iraq hapo kabla ulikuwa umelikubali azimio hilo na ulikuwa ukiendesha propaganda dhidi ya Iran kutokana na kutolikubali azimio hilo. Lakini wakati Iran pia ilipotangaza kulikubali azimio hilo, jeshi la dikteta Saddam kwa mara nyingine tena likaishambulia ardhi ya Iran. ***

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, ndege za kivita za utawala wa Israel zilishambulia eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina, na kuua watu 16 na wengine 150 kujeruhiwa. Shambulio hilo la kushtukiza lililofanyika usiku, liliua watoto 9 wasiokuwa na hatia yoyote. Hali kadhalika miongoni mwa waliouawa shahidi katika shambulizi hilo ni Sheikh Swalah Shahadah, mmoja wa makamanda wa Brigedi ya Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya kiislamu ya Palestina HAMAS ambaye aliuawa akiwa pamoja na mkewe na binti yake.***

 Swalah Shahadah,

Na miaka 14 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 22 Julai 2003, waliuawa Uday na Qusay watoto wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq pambizoni mwa mji wa Mosul, kaskazini mwa Iraq. Uday na Qusay wakiwa wamefuatana na maafisa wa ngazi za juu wa Iraq walitoroka mjini Baghdad baada ya majeshi ya Marekani na Uingereza kuishambulia nchi hiyo mwezi Aprili 2003. Majeshi ya Marekani yalishambulia nyumba walimokuwa wamejificha watoto hao wa Saddam Hussein na kuwauwa pamoja na wasaidizi wao.***

Uday na Qusay

 

 

Tags