Jul 16, 2018 07:23 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Julai 16

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita, haswa kufikia tamati michuano ya Kombe la Dunia Russia....

 

Dondoo za Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya soka ya Ufaransa imetwaa Kombe la Dunia baada ya kuigaragaza Croatia mabao 4-2 katika mchezo wa fainali uliokuwa wa kusisimua Jumapili jioni. Ufaransa iliyoingia mechi hiyo ikisaka ubingwa wa dunia kwa mara ya pili tangu 1998, ilitangulia kwenye mechi na goli la kwanza dakika ya 18 kufuatia mkwaju wa Antoine Griezmann ulioelekezwa wavuni na Mario Mandzukic aliyejifunga. 

Wafaransa mjini Paris wakisherehekea ushindi wa Kombe la Dunia 2018

 

Uongozi wa Ufaransa ulidumu kwa dakika 10 pekee kwani winga matata wa Croatia anayeichezea Inter Milan Ivan Perisic, alifyatua kombora ndani ya sanduku na kukatiza sherehe za Ufaransa. Pande zote zilionyesha dalili za kutofungana hadi dakika ya 37 pale Perisic alipounawa mpira wa kupinda wa Antoine Griezmann na kusababisha penalti. Mfungaji Griezmann hakuchelea kuipa Ufaransa uongozi kwa kumduwaza kipa wa Croatia aliyeng'aa kwa kupangua matuta mechi za awali dhidi ya Denmark na Urusi. Magoli ya Paul Pogba na Kylian Mbappe kipindi cha pili yaliikabidhi Ufaransa Kombe la Dunia mbele ya rais wake Emmanuel Macron na maelfu ya mashabiki ugani Luzhniki.

Rais wa Russia, Vladimir Putin akipiga danadana

 

Baada ya kutolewa hatua ya makundi 2002, kufungwa na Italia 2006 kwenye fainali, kukumbwa na sakata kikosini 2010, na kutemwa na Ujerumani katika robo fainali 2014, hatimaye the Blues, chini ya Didier Deschamps wamefanikiwa jaribio lao Urusi 2018 kwa kuikung'uta Croatia mabao 4-2 muda wa kawaida. Licha ya kuwa katika timu iliyolazwa kwenye fainali, juhudi za nahodha wa timu hiyo Luka Modric hazikusahaulika kwani amekabidhiwa mpira wa dhahabu kwa kuwa mchezaji bora wa Kombe hili. Mwingine aliyetunukiwa ni kipa wa Ubelgiji Thibaut Coutois aliyenyakua tuzo ya glovu za dhahabu kwa kuwa mdajaki bora Urusi. Ingawa Uingereza ilimaliza nafasi ya nne, mfungaji wake Harry Kane alitia kapuni kiatu cha dhahabu kwani mabao ya Mbappe ya Griezmann hayakufikia sita aliyofunga Kombe hili. Katika barabara za Paris, mji mkuu wa Ufaransa na miji mingine, mbwembwe, nderemo, vifijo na hoi zilihinikiza mashabiki wakishangilia ushindi huo.

Wachezaji wa Ubelgiji wakisherehea bao

 

Siku ya Jumamosi Ubelgiji ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2 – 0 iliposhuka dimbani kuvaana na Uingereza katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wa michuano ya Kombe la Dunia. Thomas Meunier alifungua mlango wa magoli hayo dakika ya nne katika uga wa Saint Petersburg jijini Moscow na kuiweka Ubelgiji kifua mbele. Mchezaji matata wa klabu ya soka ya Chelsea Eden Hazard alihakikishia Ubelgiji ushindi wa medali ya shaba kupitia bao lake la ushindi alilolivurumisha wavuni kunako dakika ya 82.

Alireza Faghani, refa wa Iran akiendesha mechi ya Kombe la Dunia Russia

 

Mchuano huo uliendeshwa na Muirani Alireza Faghani, ambaye ni moja wa marefa waliojizolea sifa kedekede kwenye mashindano hayo ya dunia. Huku hayo yakirifiwa, mamia ya raia wa Nigeria wameripotiwa kukwama Russia baada ya kuuziwa tiketi feki. Shirika lisilo la kiserikali la Russia liitwalo “Alternative” limefichua kwamba Wanigeria wapatao 400 waliokwenda kushuhudia Kombe la Dunia nchini Russia, wamekwama nchini baada ya kugundulika kwamba waliuziwa tiketi feki. Kati ya hao, 60 wamelazimika kulala nje ya ubalozi wa Nigeria nchini humo huku hatima yao ikisalia kitendawili.

Rais wa Russia (kulia) na Rais wa FIFA Gianni Infantino wakinyanyua Kombe la Dunia

 

Kwengineko, Wakenya katika mitandao ya kijamii wamelaani vikali hatua ya Bunge kuwatuma makumi ya wabunge na maseneta kwenda kutizama mechi kadhaa za mwisho za Kombe la Dunia, kwa gharama za walipa kodi. Bunge limesema lengo la kuwatuma wabunge hao ni kutathmini jinsi nchi nyingine zimefanya ili kufika fainali za Kombe la Dunia, ili Kenya nayo iweze kushiriki michuano hiyo ya kimataifa katika siku zijazo.

Iran yaibuka kidedea mchezo wa Wushu Brazil

Timu ya taifa ya mchezo wa wushu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa pande wa vijana imeibuka kidedea kwa kuzoa medali lukuki katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo uliofanyika Brasilia, mji mkuu wa Brazil. Wanamichezo hao wa Iran wametia kibindoni medali 26, zikiwemo dhahabu 11. Siku ya Jumamosi, wanamichezo hao wa Kiirani walinyakua medali 9 zaidi, ikiwemo moja ya dhahabu, 4 za fedha na 4 za shaba.

Mchezaji wa wushu wa Iran akionesha medali aliyotunukiwa

 

Medali ya dhahabu ilitwaliwa na Sayyid Mohammad Hosseini katika mtindo wa Daosho, kategoria ya wachezaji wa wushu wenye umri kati ya miaka 15 na 18. Katika mtindo wa Daosho au ukipenda Taolu, wachezaji hupambana kwa kutumia upanga. Duru ya 7 ya mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama World Junior Wushu Championships yalianza Julai 9 na kumalizika Julai 16. Wushu ni mchezo ulioibukia China mwaka 1949, unaojumuisha masumbwi, kupambana kwa kutumia upanga, mieleka na taekwondoh.

Iran yatwaa taji la Karate Asia

Timu ya taifa ya karate ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya bara Asia ya mchezo huo nchini Jordan yaliyofunga pazia lake siku ya Jumapili. Makarateka wa Kiirani walionyesha kujituma katika mipambano yote na hatimaye jitihada zao zikazaa matunda. Wametuzwa medali ya dhahabu kwa kuibuka kidedea katika mashindano hayo ya kikanda. Siku ya Jumapili katika mpambano wa fainali, Wairan waliwalemewa Wasaudia na kuibuka washindi wa alama 3-0. Siku ya Jumamosi, mwanakarate wa Iran Majid Hassannia alimepelea mchakamchaka Msaudi Saud al-Basher na kumshinda kwa alama 6-2 katika katogoria ya kumite kwa makarateka wenye kilo zisizozidi 55, katika mpambano wa aina yake uliopigwa katika Ukumbi wa Michezo wa Prince Rashed Martial Arts Center of King Hussein Sports City mjini Amman, na kutwaa dhahabu.

Majid Hassanninia, karateka nyota wa Iran

 

Wakati huo huo, timu ya karate ya Iran ya wabinti inayowajumuisha Elnaz Taghipour, Najmeh Ghazizadeh na Shadi Ja’afari, imemaliza ya tatu na kutunukiwa medali ya shaba. Binti wa Kiirani Hamideh Abbasali alishinda medali ya dhahabu katika safu ya kumite kwa wachezaji wenye kilo zaidi ya 68, alimpomsagasaga Wen Tzu-hsuan wa Tapei-China na kumbwaga kwa alama 8-0. Duru ya 15 ya Asian Karate Senior Championships iliyosimamiwa na Shirikishola Karate Asia (AKF) ilianza Julai 11 na kufikia tamati Jumapili ya Julai 15. 

Dondoo za Kombe la Kagame

Siku ya Ijumaa Julai 13, klabu ya soka ya Azam FC, ilifanikiwa kutetea ubingwa wake wa Kombe la Kagame baada ya kuwafunga Simba mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali uliomalizika usiku huu kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam. Mabao ya Azam FC katika mchezo hu yalifungwa na mshambuliaji Shaaban Idd pamoja na nahodha Aggrey Morris huku bao la Simba likifungwa na mshambuliaji Meddie Kagere.

Rais Paul Kagame wa Rwanda, mlezi wa Kombe la Cecafa

 

Ushindi wa Azam FC unaifanya timu hiyo sasa kuifikia rekodi ya Simba ya kutetea ubingwa huo ambayo waliiweka mwaka 1992 wakitetea ubingwa waliouchukua mwaka 1992. Azam FC walitwaa ubingwa huu mwaka 2015 na wameutetea mwaka 2018 baada ya michuano hiyo kutofanyika katika miaka ya 2016 na 2017. Aidha mshambuliaji wa timu hiyo Shaaban Idd ambaye ameshasajiliwa na timu ya Tenerife ya Hispania na atasafiri kwenda kujiunga nayo muda wowote kuanzia sasa, amefanikiwa kuibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 8 katika mechi 5 kuanzia hatua ya makundi hadi leo fainali. Azam FC sasa wametwaa kombe hilo kwa mara ya pili huku Simba ambao ndio mabingwa wa historia wa kombe hilo wakibaki na mara 6.

Klabu ya Simba iliyoshindwa kufurukuta mbele ya Azam

 

Baada ya klabu ya soka ya Simba kufungwa mabao 2-1 na Azam FC kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Kagame Ijumaa usiku, kocha wa Simba, Masoud Djuma, amesema mashabiki hawatakiwi kulalamika kwa kutokuwepo baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza. Masoud ameyasema hayo kufuatia baadhi ya mashabiki waliokuwepo uwanjani kuonyesha kutoridhishwa na kiwango cha wachezaji waliopewa nafasi ambao wengi wao ni wale waliosajiliwa katika kipindi hiki cha usajili huku wachezaji wazoefu wakiachwa. Aidha ameongeza kuwa wachezaji wapya na wale ambao hawakupata nafasi kwenye ligi msimu uliopita ambao amewatumia kwenye michuano ya CECAFA, wameonyesha kiwango kikubwa na sasa anaweza kuamini ana kikosi kipana kwa ajili ya michuano mbalimbali msimu ujao.

Endapo Simba ingetwaa ubingwa Ijumaa, ingekuwa ni mara yake ya saba kwani tayari ni mabingwa mara sita, wakishikilia rekodi ya kuchukua kombe hilo mara nyingi zaidi.  Kwengineko, wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga, wataondoka nchini Jumatatu hii kuelekea Nairobi tayari kuumana na Gor Mahia kwenye michuano hiyo. Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya timu hiyo ambaye pia ndio Mwenyekiti wa Kamati ya usajili, Hussein Nyika, amesema kikosi cha Yanga kinaondoka siku mbili kabla ya mchezo wao wa Julai 18 kwenye uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi. Amesema kikosi chake kiko tayari kuwakabili Wakenya hao waliopo nao kwenye kundi moja pamoja na timu za USM Alger na Rayon Sports. Yanga inashika nafasi ya mwisho kwenye kundi lao ikiwa na pointi moja huku USM Alger ikiongoza kundi kwa kuwa na pointi 4. Gor na Rayon zina pointi mbili kila mmoja.

Chelsea yapata mkufunzi mpya

Siku moja baada ya klabu ya Chelsea kutangaza kuwa imemfuta kazi kocha wake Antonio Conte baada ya kudumu naye kwa miaka miwili akiwapa mataji ya EPL na Kombe la FA, The Blues imemtangaza rasmi kocha wa zamani wa Napoli, Maurizio Sarri kuwa kocha wao mpya kwa mkataba wa miaka mitatu.

Mashabiki wa Chelsea uwanjani Stamfford Bridge

 

Sarri anajiunga na Chelsea baada ya kuitumikia Napoli kwa miaka mitatu. Sarri nafasi yake katika klabu ya Napoli ilitangazwa mapema kuchukuliwa na Carlo Ancelotti.

.....................................TAMATI........................