Aug 08, 2018 21:59 UTC
  • Alkhamisi tarehe 09 Agosti 2018

Leo ni tarehe 25 Dhulwaada 1439 Hijria sawa na 09 Agosti 2018.

Miaka 717 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alizaliwa faqihi, mfasiri, mtaalamu wa teolojia na mwanafasihi wa Kiislamu, Masud bin Omar Taftazani huko Quchan kaskazini mwa Iran. Kwa kipindi kirefu cha umri wake, Taftazani alifanya safari katika miji ya Khorasan na Asia ya Kati kwa lengo la kutafuta elimu. Allamah Taftazani alianza kuandika vitabu akiwa bado kijana kutokana na uhodari na umahiri wake na baadhi ya vitabu vya msomi huyo mkubwa wa Kiislamu vingali vinafundishwa hadi hii leo. Miongoni mwa vitabu hivyo ni al Mutwawwal, al Irshad na Mukhtasarul Maani.

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, zikiwa zimepita siku tatu tangu Marekani iushambulie kwa bomu la nyuklia mji wa Hiroshima nchini Japan, Washington iliushambulia pia kwa bomu jingine la nyuklia mji wa bandari wa Nagasaki kwa amri ya Harry Truman, Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Jumla ya watu elfu themanini walifariki dunia dakika chache tu baada ya shambulizi hilo la bomu la nyuklia huko Nagasaki, na wengine walipoteza maisha baada ya kupita miezi na miaka, kutokana na athari mbaya za mada hatari za mionzi ya nunurishi au radioactive kwa kimombo. Maafa makubwa ya mashambulizi ya mabomu ya nyuklia ya Marekani huko Hiroshima na Nagasaki yaliyofanyika kwa lengo la kuilazimisha Japan isalimu amri kikamilifu mbele ya majeshi ya waitifaki, yalikuwa kengele ya hatari kwa walimwengu kwamba, nchi zinazomiliki silaha za atomiki hususan Marekani, hazisiti kufanya jinai za kutisha kama kuangamiza kizazi cha wanadamu kwa ajili ya kufikia malengo yao.

Mlipuko wa bomu la nyuklia

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, Hermamn Hesse mwandishi na malenga mashuhuri wa Ujerumani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1877 katika familia ya kidini na kuanza kazi ya utunzi wa mashairi katika kipindi cha kuinukia kwake. Akiwa na umri wa miaka 20, Hesse alitoa diwani yake ya kwanza wa mashairi. Mwaka 1912 mwandishi na malenga huyo mashuhuri wa Ujerumani alichukua uraia wa Uswisi na kuichagua nchi hiyo kuwa makazi yake ya kudumu. Mwishoni mwa umri wake alifanya safari katika baadhi ya nchi za mashariki na kuathirika na tamaduni, mafunzo na mienendo ya kiamaadili ya wananchi wa maeneo hayo. Mnamo mwaka 1946 malenga huyo alitunukiwa tuzo ya Nobel.

Hermamn Hesse

Miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Singapore ilijitenga na Malaysia. Japan iliiteka Singapore katika Vita vya Pili vya Dunia lakini mnamo mwaka 1945 uvamizi huo wa Japan ulikomeshwa na kwa mara nyingine tena nchi hiyo ikakoloniwa na Uingereza. Mwaka 1963 Singapore iliunganishwa na Shirikisho la Malaysia na mwaka 1965 ilijitenga na kuwa nchi huru.

Bendera ya Singapore

Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo Richard Nixon Rais wa zamani wa Marekani kutoka chama cha Republican alilazimika kujiuzulu baada ya kukumbwa na kashfa ya kufanya udanganyifu kwenye uchaguzi wa Rais, kashfa iliyojulikana kwa jina la "Watergate". Nixon alilazimika kung'atuka kwenye nafasi ya urais na kumpisha Gerald Ford aliyekuwa Makamu wa Rais ambaye aliendeleza kipindi hicho cha urais kwa muda wa miaka minne.

Richard Nixon Rais

Na tarehe 9 Agosti kila mwaka ilitangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Watu wa Asili (Indigenous). Siku hiyo ilitangazwa rasmi ili kukumbuka na kutetea haki za zaidi ya watu milioni 370 wa asili katika nchi 90 duniani. Siku hii imekuwa ikiadhimishwa kwa ajili ya kuwakumbuka maelfu ya wanaume na wanawake wa asili wanaoshikamana na mila, tamaduni na desturi zao. Watu wa asili (Indigenous) ni makundi na mataifa ambayo yanadai kuwa, yana mfungamano makhsusi wa kihistoria na kiutamaduni na jamii za ardhi au eneo lao la asili. Neno hili hutumika kumaanisha wakazi wa awali na wenyeji wa kila nchi 

Hii leo inakadiriwa kuwa, kuna watu  wa asili (Indigenous) karibu milioni 370 katika nchi 90 duniani. Hii ina maana kwamba, asilimia 5 ya jamii ya watu wote duniani inaundwa na watu wa asili (Indigenous). Hata hivyo watu hawa wanahesabiwa kuwa ni sehemu ya asilimia 25 ya watu masikini zaidi duniani.