Jan 30, 2019 08:33 UTC
  • Ruwaza Njema (9)

Assalaam Alaykum. Ni siku nyingine ambayo tumejaaliwa kukutana nanyi tena wapenzi wasikilizaji katika kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambapo kwa leo tutazungumzia tabia nyingine njema ya mbora wa viumbe, Mtume Mtukufu (saw) kuhusiana na jinsi ya kuamiliana vyema na Watu wa Kitabu yaani Wakristo wanaoishi katika kivuli cha serikali adilifu na inayofuata mafundisho ya Mwenyezi Mungu na namna alivyokuwa akifanya ibada zake, hivyo kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi.

Sheikh as-Swadouq (MA) ameandika kisa kinachofuata katika kitabu chake cha Aamali akinukuu Hadithi ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam Ali (as) kwamba alisema: 'Yahudi mmoja alikuwa akimdai Mtume wa Mwenyezi Mungu dinari kadhaa. Siku moja alienda kumdai Mtume (saw) deni lake naye Mtume akamwambia: Kwa sasa sina uwezo wa kukulipa. Yahudi akasema: Sitakuacha hadi unilipe deni langu. Mtume (saw) akasema: Mimi pia nitaendelea kubaki na wewe hapa. Aliketi na Yahudi yule hapo hadi wakaswali swala ya adhuhuri, alasiri, magharibi, ishaa na swala ya Asubuhi ya siku iliyofuata. Masahaba wa Mtume (saw) wakamkemea na kumtishia Yahudi huyo. Mtume (saw) aliwatazama kwa kuchukia na kuwaambia: Mnafanya nini? Wakamjibu: Je, utakamatwa mateka na Yahudi?! Mtume (saw) akajibu: 'Mola wangu Mtukufu hakunituma nimdhulumu yeyote, awe ni katika dini yangu au mwenye imani tofauti.'

*********

Wapenzi wasikilizaji, ni tabia njema iliyoje hii ya Mtume Mtukufu (saw) na ambaye wakati huo alikuwa ni mtawala wa moja kwa moja wa mji wa Madina, tena kwa Yahudi ambaye wakati huo alikuwa ni miongoni mwa wachache mjini hapo? Je, mnajua ni kwa kiwango gani jambo hili lilimuathiri Yahudi huyo? Endeleeni kuwa pamoja nasi ili tupate kujua yaliyotokea baada ya hapo. Imam Ali (as) anaendelea kusimulia kisa hiki katika Hadithi hiyo kwa kusema: 'Mchana ulipowadia, Yahudi huyo alisema: 'Ash'hadu an La Illaha Ila Allahu wa Ash'hadu anna Muhammadan Abduhu wa Rasuluh.' Kisha akatoa nusu ya mali yake ili itumike katika njia ya Mwenyezi Mungu. Alisema: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ninaapa kwamba sikukufanyia niliyokufanyia kutokana na dharau bali nilitaka kuona iwapo sifa zako zinaambatana na mambo tuliyoahidiwa katika kitabu cha Torati au la. Hakika nimesoma sifa zako katika Torati ambapo inasema: 'Muhammad bin Abdallah atazaliwa Makka na kuhajiri kwenda Madina. Si mjeuri wala mwenye tabia mbaya, hapazi sauti wakati wa ugomvi, hatukani mtu wala kutamka maneno machafu.' Na mimi huyu hapa ninashuhudia juu ya upweke wa Mwenyezi Mungu na utume wako. Ninatoa mali yangu yote na kukupa wewe ili upate kuitumia katika yale yote aliyoyaamrisha Mweyezi Mungu.' Imam Ali (as) anasema mwishoni mwa kisa hiki: 'Yahudi yule alikuwa na mali nyingi sana.'

Bwana Mtume Muhammad SAW ni ruwaza njema kwa viumbe wote

 

Wapenzi wasikilizaji, ibada ya Mtume Muhammad ni mfano bora na wa juu zaidi wa ibada zinazopaswa kutekelezwa na waja wote wa MwenyezI Mungu. Ni alama bora na ya kuvutia zaidi kuhusiana na ibada halisi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika hali zote mbili za kuhitaji na dhiki na vilevile furaha na faraja. Na hili ni fundisho muhimu na la msingi ambalo tunajifunza kutokana na Hadithi mbili zinazofuata katika sira ya Bwana wetu mpendwa al-Habib Muhammad al-Mustafa (saw).

Sheikh Tusi amenukuu katika kitabu cha Aamali, Hadithi ambayo imenukuliwa kutoka kwa Imam Baqir (as) kwamba Sahaba mwema wa Mtume (saw) Jabir bin Abdallah al-Answari (MA) alienda kwa Imam Ali bin al-Hussein Zeinul Abideen (as) na kumtaka aihurumie nafsi yake kutokana na kuzama kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu. Ifuatayo ni sehemu ya jibu alilolitoa Imam Zeinul Abideen (as) kwa sahaba huyo mwema wa Mtume (saw): 'Ewe sahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, Haujui kwamba babu yangu, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) licha ya kwamba Mwenyezi Mungu alimughufiria madhambi yake yaliyopita na yanayokuja lakini hakuacha kujitahidi katika kutekeleza ibada Yake? Na- Baba na mama yangu wawe fidia kwake – alizama katika ibada kiasi kwamba miguu na nyayo za miguu yake zilivimba na walipomwambia: Licha ya kwamba Mwenyezi Mungu amekusamehe dhambi zako zilizopita (za zamani) na zinazokuja bado unafanya ibada kiasi hiki? Aliwajibu: Je, nisiwe mja mwenye kushukuru?!' Kisha Imam Zeinul Abideen (as) akasema: 'Ewe Jabir! Nitaendelea kufuata njia ya baba zangu wawili, Muhammad na Ali, kama ruwaza njema kwangu hadi nitakapokutana nao (as).'

**********

Ndugu wasikilizaji, na imepokelewa katika vitabu kadhaa kikiwemo cha Aamali kupitia kwa Bakr bin Abdallah kwamba alisema: 'Omar aliingia kwa Mtume (saw) na kumkuta akiwa anaumwa na mwenye homa kali. Omar akasema: Nakuona ukiwa unaumwa sana. Mtume (saw) akasema: Pamoja na hayo, lakini hilo halikunizuia kusoma usiku Sura thelathini (za Qur'ani) zikiwemo zile saba ndefu. Omar akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mwenyezi Mungu tayari amekusamehe madhambi yako yaliyopita na yanayokuja, huku wewe unafanya juhudi hizi zote – yaani katika ibada? Mmtume (saw) akamjibu: Eeh Omar! Je, nisiwe mja anayeshukuru?'

************

Tunamwomba Mwenyezi Mungu atupe uwezo wa kuweza kumfuata Mtume wake na mbora wa viumbe wote, Muhammad (saw), Allahumma Ameen.

Tunakushukuruni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi wakati mwingine tutakapokutana tena panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.

 

Tags