Jumapili, tarehe 25 ,Agosti 2019
Leo ni Jumapili tarehe 23 Dhulhija 1440 Hijria sawa na Agosti 25 mwaka 2019
Katika siku kama ya leo miaka 924 iliyopita sawa tarehe 25 Agosti mwaka 1095, vilianza Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu. Watu wa msalaba walianzisha vita hivyo kidhahiri wakiwa na lengo la kuteka Baitul Muqaddas, ingawa shabaha halisi ya wapiganaji hao ilikuwa ni kudhibiti ardhi kubwa za Waislamu na kuwanyonya na kuwakoloni wafuasi wa dini hiyo. Katika vita hivyo wafuasi wa kanisa walichora alama za msalaba kwenye mabega na mavazi yao, na kwa sababu hiyo vita hivyo vimekuwa maarufu kwa jina la Vita vya Msalaba. Baada ya vita vingi na Waislamu, wapiganaji wa msalaba hatimaye waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Baitul Muqaddas mnamo mwaka 1099, ambako waliua raia wengi na kupora mali zao. Mji huo ulikombolewa mwaka 1187 na wapiganaji wa Kiislamu waliokuwa wakiongozwa na Salahuddin Ayyubi.
Miaka 152 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia msomi mashuhuri wa Uingereza Michael Faraday. Faraday alizaliwa mwaka 1791 mjini London na licha ya kuwa hakuwa na elimu ya juu lakini alifanikiwa kupata maendeleo muhimu katika fizikia na kemia kwa kutumia majaribio na tajiriba. Tarehe 24 Novemba miaka 184 iliyopita, Michael Faraday aligundua chombo cha mkondo wa umeme kinachojulikana kwa kitaamu kama ''Electric Current''. Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme.
Miaka 78 iliyopita katika siku kama hii ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, ikiwa ni wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, majeshi ya nchi waitifaki yaliivamia na kuikalia kwa mabavu Iran. Wasiwasi ulikuwa umezikumba nchi za Marekani, Ufaransa na Uingereza kufuatia kusonga mbele vikosi vya Ujerumani katika ardhi ya Umoja wa Kisovieti. Kwani nchi hizo zilikuwa zikitambua kwamba, endapo Ujerumani itaushinda Umoja wa Kisovieti maslahi yao katika eneo la Mashariki ya Kati yangekuwa hatarini. Ni kutokana na sababu hiyo ndiyo maana madola hayo yakapeleka huko Umoja wa Sovieti silaha na vifaa vingi vya kijeshi kupitia ardhi ya Iran. Licha ya Iran kutangaza kutounga mkono upande wowote katika vita hivyo, Umoja wa Sovieti ulianza kuishambulia Iran kutoka upande wa magharibi na mashariki, huku majeshi ya Uingereza yakitelekeza mashambulio kama hayo kwa upande wa kusini.
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sheikh Abbas Qummi, aalim na mpokeaji hadithi mtajika wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria katika mji mtakatifu wa Qum huko kusini mwa Tehran. Sheikh Abbas Qummi alianza kusoma elimu ya dini akiwa huko huko Qum na baadaye alielekea katika chuo kikuu cha kidini katika mji wa Najaf nchini Iraq ili kukamilisha masomo yake. Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Sheikh Abbas Qummi alipata elimu kutoka kwa maulamaa watajika wa hauza hiyo ya kielimu. Sheikh Abbas Qummi alirejea Iran baada ya muda ambapo alitumia muda wake wote kuandika vitabu na kufuatilia masuala ya kidini. Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwanazuoni huyo ni Mafatiihul Jinan na Manazilul Akherah.