Sep 16, 2019 11:32 UTC
  • Wanasayansi Wairani waunda mashine ya kutibu wenye mshtuko wa moyo

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia matukio muhimu ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani.

Mashine ya kutibu moyo

Wanasayansi Wairani wamefanikiwa kuunda mashine inayoweza kuwatibu haraka wagonjwa waliopata mshtuko wa moyo.

Hayo yamedokezwa hivi karibuni na msimamizi wa mradi huo Sarvar Yousefinasab Nobari ambaye amongeza kuwa wametumia mashine yenye safu za graphene kutengeneza maabara ndogo kwenye chipu na inaweza kumpima haraka mtu aliyepata mshtuko wa moyo kwa kutumia damu na matokeo kupatikana katika kipindi cha chini ya dakika 20. Kipimo hicho hutumika kubaini kilichomsibu mgonjwa aliyepata mshtuko wa moyo na kiwango cha uharibifu ili kuharakisha matibabu.

Bi Yousefinasab Nobari amesema chombo walichovumbua kinaweza kubebwa kirahisi na utumizi wake ni sahali mbali na kutoa vipimo vilivyo na kiwango cha juu cha usahihi. Amesema mashine hiyo ndogo waliofanikiwa kuunda itaanza kuzalishwa kwa wingi hapa Iran katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya kupokea leseni zinazohitajika.

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imeweza kupiga hatua kubwa sana katika uga wa sayansi na teknolojia, ukiwemo  uga wa kuunda vifaa vya tiba.

Vyuo vikuu vya Iran vyaongoza Asia Magharibi

Orodha ya hivi karibuni ya vyuo vikuu bora zaidi duniani ya Times Higher Education imebaini kuwa vyuo vikuu 40 vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kati ya vyuo vikuu bora zaidi duniani.

Taasisi ya Elimu ya Juu ya Times Higher Education katika ripoti yake ya mwaka 2019 imeorodhesha vyuo vikuu 40 ambayo ni kati ya vyuo vikuu bora duniani mwaka huu.

Nafasi ya kwanza miongoni mwa vyuo vikuu vya Iran imeshikwa na Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha Noshirvani katika mji wa Babol kaskazini mwa Iran.

Vyuo vingine vilivyoshika nafasi za juu katika orodha hiyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba cha Tehran, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Iran na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Gilan.

Aidha kieneo nchi zinazoifuata Iran ni Uturuki ikiwa na vyuo vikuu 34  kisha Misri 30, Saudi Arabia 7 na Imarati vinne.

Orodha ya Taasisi ya Elimu ya Juu ya Times hutegemea vigezo vya elimu, mipango ya baadaye, utafiti, viwango, na pato kutokana na teknolojia katika kuorodesha vyuo vikuu bora.

Kwa mujibu wa orodha ya mwaka huu vyuo vikuu bora duniani ni Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza, Chuo Kikuu cha Teknolojia cha California nchini Marekani, Chuo Kikuu cha Cambridge cha Uingereza,  Chuo Kikuu cha Stanford cha Marekani, Chuo Kikuu cha MIT cha Marekani na Chuo Kikuu cha Princeton cha Marekani.

Utalii wa kitiba Iran

Iran imepiga hatua kubwa mwaka huu katika sekta ya utalii wa kitiba ambapo katika kipindi cha miezi minne ya kwanza ya mwaka wa Hijria Shamshia yaani kutoka Machi 21 hadi Julai 22,  watalii wa kitiba wapatao laki sita wamefika Iran kupata huduma za afya. Idadi hiyo ya muda wa miezi minne ni sawa na idadi nzima ya watalii wa kitiba waliofika Iran mwaka uliopita.

Hayo yamedokezwa na Mohammad Panahi, naibu mwenyekiti wa Jumuiya ya Kustawisha Utalii wa Kitiba Iran ambaye ameongeza kuwa, mwaka uliopita sekta ya utalii wa kitiba iliweza kuiletea Iran pato la dola bilioni 1.2. Panahi amesema aghalabu ya watalii wa kitiba wanaofika Iran ni kutoka nchi za Ghuba ya Uajemi, Iraq, Syria, Jamhuri ya Azerbaijan na pia Wairani wanaoishi nje ya nchi hasa kutoka Canada na Ujerumani. Amesema watalii hao wa kitiba hufika Iran kupata matibabu kama vile upasuaji wa moyo, upasuaji wa mifupa, kutibiwa tatizo la ugumba na utasa na pia upasuaji wa plasitiki ambao ni aina maalumu ya upasuaji unaojumuisha utengenezaji mpya, urekebishaji au ubadilishaji wa mwili wa binadamu. Amesema sababu kubwa ya ongezeko la watalii wa kitiba ni kushuka thamani ya sarafu ya Iran ya Rial mkabala wa sarafu za kigeni kwani jambo hilo limepunguza gharama kwa watu wanaotoka nje ya nchi. Aidha amesema sababu nyingine kubwa ni umahiri na uhodari wa madaktari wa Iran pamoja na vifaa bora vya tiba hapa nchini.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, utalii wa kitiba ni aina ya utalii unaohusu wagonjwa kusafiri katika nchi zingine kwa ajili ya kupata matibabu. Huu ni utalii unaokua kwa kasi sana duniani. Kwa mujibu wa mitandao mbali mbali ya utalii wa afya, nchi kumi zinazoongoza kwa utalii wa matibabu duniani ni Japan, Korea Kusini, Marekani, Taiwani, Ujerumani, Singapore, Malaysia, Sweden, Thailand na India.

Alibaba kufadhili ujuzi wa kidijitali Afrika

Kampuni kubwa ya biashara ya China Alibaba  hivi karibuni ilizindua programu yake ya kwanza ya biashara ya kuvuka mipaka kwenye mtandao kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza wa Afrika.

Wanafunzi 22 kutoka Rwanda Septemba 10 waliwasili katika mji wa Hangzhou nchini China, yaliyopo makao makuu ya Alibaba, ikiwa inaadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo. Akizungumza kwenye sherehe za ufunguzi mkurugenzi wa Chuo cha Biashara katika Chuo kikuu cha Ualimu cha Hangzhou, Zeng Ming amesema chuo hicho sio cha biashara ya jadi bali kinazingatia uchumi kwenye mtandao wa internet. Amefafanua kuwa wanafunzi wa kigeni wanaweza kuchukua kozi zinazohusiana na intaneti, biashara ya kimataifa na biashara ya kuvuka mipaka kwenye mtandao na pia kupata uzoefu wa kwanza wa maendeleo ya uchumi wa kidijitali wa China.

Mradi huo ni sehemu ya makubaliano ya ushirikiano kati ya serikali ya Rwanda na Alibaba chini ya mpango wa pili wa Jukwaa la Biashara kwenye Mtandao Duniani.

Nchi za Afrika ziwekeze katika teknolojia ya kidijitali

Banki ya Dunia imesema nchi za Afrika zinatakiwa kufanya maamuzi thabiti kuhusu mageuzi ya kidigitali, kwa kuwekeza kwenye miundo mbinu ya kidigitali, ili ziweze kufikia malengo ya Umoja wa Afrika ya huduma za intaneti kwa wote na kwa gharama nafuu.

Hayo yamesemwa kwenye Kongamano la 5 la uwekezaji barani Afrika lililofanyika mjini Brazzaville kuanzia Spetemba 10-12 ambapo imebainika kuwa huduma za internet yenye kasi, zinasaidia kutoa nafasi za ajira kwa makundi yote ya elimu. Ripoti yenye kauli mbiu ya teknolojia za kidigitali kwa wote barani Afrika imezinduliwa katika mkutano huo na kusisitiza umuhimu wa kuwapa wafanyakazi ujuzi wa kidigitali na kutatua tatizo la kuwa na ujuzi wa kimsingi wa teknolojia za kidigitali.

Kwenye mkutano huo wa siku tatu ulioandaliwa kwa pamoja na serikali ya Jamhuri ya Kongo, Wizara ta Fedha ya China, Benki ya Maendeleo ya China na Benki ya Dunia, Benki ya Dunia imesema nchi za Afrika zinatakiwa kuchukua hatua sasa.