Iran yazindua roboti mpya ya muundo wa Humanoid
Iran yazindua roboti mpya ya muundo wa Humanoid
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa utaweza kunufaika na niliyokuandalia.
Roboti hiyo iliyopewa jina la Surena IV ilizinduliwa Disemba 14 katika sherehe ambayo ilifanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia Dkt. Sorena Sattari. Roboti ya kwanza katika kizazi cha Surena ilizinduliwa mwaka 2008. Surena I ilikuwa na urefu wa sentimeta 165 na kilo 60 na ilikuwa ina uwezo wa kuzungumza kifarsi na kucheza mpira. Baada ya hapo Surena pili iliundwa ikiwa na urefu wa sentimeta 145 na uwezo mkubwa wa kuzunguka na iliweza kuvuma sana katika vyombo vya habari vya kimataifa na kutajwa kuwa nembo ya roboti za Iran. Wanasayansi Wairani waliendeleza mradi huo na Machi 2017 walizindua kizazi cha tatu cha roboti ya Surena ambayo ilikuwa na kasi zaidi ya roboti mbili zilizoitangulia mbali na kuwa uwezo wake wa kiakili pia ulikuwa umeimarika. Surena IV ina uwezo mkubwa wa kuzunguka digrii 43 katika hali ambayo Surena ya kwanza ilikuwa na uwezo wa kuzunguka digrii 8 tu. Aidha urefu wake ni mita 1.7 na uzito wake ni kilo 68 huku kasi yake ikiwa ni 0.7 kwa saa. Hali kadhalika roboti hii mpya ya Surena IV ina uwezo wa kupanda na kushuka sambamba na kutekeleza harakati mbali mbali na pia inaweza kuwasiliana kwa njia bora zaidi na mwanadamu. Katika sherehe za uzinduzi wa roboti hiyo, imeweza kujibu maswali kadhaa iliyoulizwa bila tatizo lolote.
Taasisi ya Kimataifa ya Uhandisi wa Kielektriki na Kielektroniki (IEEE) ambayo ni taasisi kubwa zaidi ya kitaaluma duniani, imeitambua roboti ya Surena kuwa kati ya roboti maarufu zaidi duniani kwa mujibu wa utendaji kazi wake.
Roboti hiyo ya kizazi cha nne ni sehemu ya roboti zilizotengenezwa Iran aina ya humanoid ambazo zimepewa jina la Jenerali Surena wa Iran ya kale katika zama za utawala wa Waparth ambaye aliishi katika karne ya 1 kabla ya Miladia (BC).
@@@
Mohammad Javad Azari Jahromi, Waziri wa Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, wizara yake imezindua mfumo wa Posta, unaojulikana kama Post-Plus na kuongeza kuwa, kuanzia sasa usafirishaji wa vifurushi vya posta utafanyika kwa kutumia ndege zisizo na rubani yaani droni ambazo zina uwezo wa kufika kila pembe ya nchi. Jahromi aliyasema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa Twitter mnamo Disemba 12 na kubainisha kuwa, usafirishaji wa haraka wa dawa zinazosambazwa mahospitalini na kwenye maeneo ya visiwa pamoja na kuwawezesha watu kutumiana na kufikishiana vitu kwa kasi ya juu ni miongoni mwa mambo ambayo wananchi wa Iran wataweza kuyafanya kuanzia sasa. Aidha amebainisha kwamba: Kwa sasa ni nchi chache tu duniani ambazo zimeweza kuanzisha mfumo huo. Waziri wa Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano wa Iran aidha amesema, shirika la taifa la posta limepatiwa magari, injini na baiskeli za umeme ambazo zimetengezwa hapa hapa nchini na akaongeza kuwa, kwa mnasaba wa kuanzishwa shughuli za mfumo wa Posta+, utumaji barua kote nchini Jumamosi ya tarehe 14 Desemba ulifanyika bila malipo.
Wakati huo huo Waziri wa Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran imefanikiwa kusambaratisha hujuma kubwa sana ya kiintaneti (cyber-attack) dhidi yake ambayo ilikuwa imeratibiwa na serikali ya kigeni. Amesema hujuma hiyo ambayo ilikuwa imeratibiwa kwa ustadi mkubwa na kufadhiliwa kiserikali ilikuwa inalenga kuvuruga mfumo wa huduma za intaneti zinazotolewa na serikali ya Iran. Amesema hujuma hiyo iliweza kutambuliwa na kusambaratishwa na ngao ya kiintaneti nchini.
Waziri Azari Jahromi hakutoa maelezo zaidi kuhusu ni serikali ipi ya kigeni iliyofadhili au kutekeleza hujuma hiyo lakini amsema taarifa zaidi zitatolewa baadaye. Mwezi Novemba pia, Iran ilitangaza kufanikiwa kuzima wimbi la mashambulizi kupitia intaneti ambayo yalikuwa yametekelezwa na utawala haramu wa Israel kwa lengo la kuvuruga mitandao ya mawasiliano nchini. Hamid Fatahi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano la Iran alisema uhasama huo utafuatiliwa kupitia vyombo vya sheria katika uga wa kimataifa. Alisema wataalamu wa Iran walizima hujuma hizo za mitandaoni kikamilifu. Naye Waziri wa TEHAMA nchini Iran alisema utawala wa Kizayuni wa Israel una faili chafu la kutumia silaha ya mitandao ya intaneti dhidi ya Iran na mfano wa hilo ni shambulizi la miaka ya nyuma kupitia kirusi cha Stuxnet. Mwezi Juni pia Iran ilitangaza kuwa mashambulizi ya kiintaneti ya Marekani dhidi ya mfumo wa makombora wa Iran yalishindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa na maadui.
@@@
Wanasayansi Wairani katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad Tawi la Khorramabad magharibi mwa Iran wamefanikiwa kuunda gari ambalo halihitajii nishati za fosili yaani petroli, diseli au gesi asilia na badala yake gari hilo linategemea nishati safi na jadidika. Mtafiti mwandamizi katika mradi huo, Bi. Hajar Baqeri Toulabi amewaambia waandishi habari kuwa, gari hilo linaweza kutumia umeme au nishati tatu jadidika ambazo ni maji, upepo au hewa na nishati ya jua. Aidha amesema gari hilo linaweza kuenda kasi ya hadi kilomita 80 kwa saa. Gari hilo ambalo limepewa jina la "Q" limeundwa kwa pamoja na Hajar Baqeri Toulabi na Ali Abbasi Zadeh. Hayo yanajiri wakati ambao mwezi uliopita, Wizara ya Nishati ya Iran ilitangaza kuwa, uzalishaji wa nishati jadidika nchini Iran umeongezeka sana na hivyo kufanikiwa katika kuzuia uchafuzi wa mazingira.
@@@
Na Hivi karibuni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzannia Profesa Joyce Ndalichako alisema kuna haja ya kulipa uzito mkubwa suala la namna watoto wanavyotumia teknolojia ili kuwaepusha na mambo yasiyo muhimu kwao. Akizungumza Disemba 4 wakati wa ufunguzi wa kongamano la saba la utafiti kuhusu elimu ya awali, makuzi na maendeleo ya watoto alisema dunia ya sasa ni ya sayansi na teknolojia na kuongeza kuwa hivi sasa kuna changamoto ya teknolojia kufundisha watoto. Amebaini kuwa zipo teknolojia ambazo kuna haja ya kuwa nazo makini huku akitoa wito wa kubuniwa teknolojia ambazo ni sahihi na ambazo zinawajenga watoto. Kongamano hilo lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Aga Khan na kuwashirikisha watafiti kutoka mataifa mbali mbali zikiwemo nchi za Afrika Mashariki, lilijadili njia za kuboresha elimu ya awali.
@@@
Naam na hadi hapo ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya Sayansi na Teknolojia kwa leo. Hadi wakati mwingine panapo majaliwa yake Mola, Kwaherini.