Jan 27, 2020 08:08 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Jan 27

Soma habari za spoti za ndani na nje ya Iran ndani ya siku saba zilizopita kwa kina......

Futsal: Mabinti wa Iran waanza vizuri

Timu ya taifa ya wasichana ya mchezo wa futsal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanza vyema mashindano ya Mabingwa wa Futsal Wenye Chini ya Miaka 19 ya Asia Mwaka huu 2020 kwa kushinda mechi zake zote za kwanza. Siku ya Jumapili, akina dada hao wa Iran waliigaragaza Turkmenistan mabao 12-0, ambapo mshambuliaji Roghayeh Sume'eh alifunga hattrick mara mbili. Maral Torkman na Fahimeh Arzani walifunga mawili kila mmoja, huku Nasrin Qomi na Negar Yaqoubi wakifunga moja moja kila mmoja. Kabla ya hapo, akina dada hao wa Kiirani waliichabanga Tajikistan mabao 15-0 katika mchuano wa ufunguzi, kabla ya kuibamiza Afghanistan mabao 16-1 katika mchuano uliofuata.

Timu ya taifa ya wasichana ya mchezo wa futsal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliposhinda kombe

 

Timu ya taifa ya wasichana ya mchezo wa futsal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatazamiwa kuvaana na Uzbekistan siku ya Jumanne kabla ya kutoana udhia na Jamhuri ya Kyrgyzstan siku ya Jumatano. Mashindano hayo ya kibara 'U19 Girl’s Futsal Championship 2020' yanaandaliwa na Shirikisho la Soka Asia ya Kati (CAFA) kwa kushirikiana na mashirikisho ya kandanda ya timu zinazocheza.

Ligi Kuu ya Karate-1, Iran yazoa medali

Timu ya taifa ya karate ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa medali mbili za dhahabu na shaba moja katika mashindano ya Ligu Kuu ya Karate 1 ya Paris nchini Ufaransa. Siku ya Jumapili, Muirani Bahman Asgari alishinda medali ya dhahabu baada ya kumchachafya Mfaransa Logan Da Costa kwa alama 4-0 katika fainali ya karete mtindo wa Kumite, ya makarateka wenye kilo zisizozidi 75. Kabla ya kutinga fainali alikuwa amewapeleka mchakamchaka raia wa Azerbaijan, Rafaei Aghayev, Mjapani Ken Nishimura, Muitaliano Luigi Busa na raia wa Ukraine, Stanislav Horuna. Dhababu nyingine ya Iran ilitwaliwa na Hamideh Abbasali, baada ya kumzidi mshindani wake wa Uturuki, Meltem Hocaoglu Akyol katika Kumite ya Wanawake wenye kilo zaidi ya 68.

Baadhi ya makarateka wa Iran

 

Saleh Abazari aliishindia Iran medali ya shaba baada ya kumsagasaga Tareq Hamedi wa Saudi Arabia, katika karate kategoria ya Kumite kwa wachezaji wenye kilo 84 na zaidi. Makarateka 700 kutoka nchi 92 duniani wameshiriki mashindano hayo ambayo yanatumika pia kusaka tiketi za kufuzu Michezo ya Olimpiki ya Tokyo Japan baadaye mwaka huu.

Soka; Klabu Bingwa Afrika

Na sasa tutupie jicho matokeo ya baadhi ya mechi za mzunguko wa tano za kuwania Taji la Klabu Bingwa Barani Afrika, zilizopigwa wikendi. Mabingwa mara tano wa Afrika, klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Ijumaa ililazimishwa sare tasa na Zamelek ya Misri iliyokuwa ikiupigia nyumbani jijini Cairo. Ulikuwa mchuano wa kusisimua katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, ambapo Waarabu hao wa Misri walihitaji ushindi ili kuwa na yakini ya kuwa katika nane bora.

Licha ya sare hiyo, Zamalek inajikita katika nafsi ya pili ya Kundi A ikiwa na alama 8, huku Mazembe wakiongoza kundi hilo kwa alama 11 katika mechi zake tano ilizocheza hadi sasa. Mabingwa hao wa zamani, wameshinda mechi tatu kati ya 5 walizocheza.

Klabu ya TP Mazembe walipotwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika miaka 3 iliyopita

 

Siku ya Jumamosi, kitimutimu kingine kilishuhudiwa baina ya Zesco United ya Zambia na Clube Desportivo de Agosto ya Angola katika uwanja wa Levy Mwanawasa jijini Ndola. Mechi hii iliishia kwa sare ya bao 1-1. Kipindi cha kwanza kilimalizika bila nyavu kutikiswa. Hata hivyo Wazambia walitangulia kuliona lango la Waangola kwa bao la dakika 50 lililofungwa na Winston Kalengo. Dakika 19 baadaye, Ary Palel wa Desportivo de Agosto ya Angola alifanya mambo kuwa suluhu bin sukluhu kwa bao lake lililokwenda shule.

Katika mechi ya Kundi B iliyowakutanisha Waarabu wawili, Etoile (Etual) du Sahel ya Tunisia ambayo ina alama tisa, ilikuwa katika Uwanja wa Al Salam jijini Cairo, kumenyana na wenyeji wao Al-Ahly ambayo wana alama saba. Al-Ahly ambao ni moto wa kuotea mbali walipata ushindi hafifu wa bao 1-0, lililofungwa na Junior Ajayi kunako dakika ya 32.  Al-Ahly wanaongoza kundi hilo kwa alama 10 kwa ushindi huo, ikifuatiwa na Al-Hilal yenye alama 9, alama sawa na Du Sahel ya Tunisia.

FC Platinum ya Zimbabwe ambayo haina matumaini ya kusonga mbele katika michuano hii, ilikuwa inajaribu kupata ushindi wake wa kwanza dhidi ya Al-Hilal ya Sudan ambayo ina alama sita, katika uwanja wa Barbourfields mjini Bulawayo siku ya Jumamosi. Na kama iliyotazamiwa walitandikwa bao moja bila jibu licha ya kuupigia nyumbani.

Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayo inaongoza Kundi C kwa alama 10, siku ya Jumamosi iliwaacha wengi wengi vinywa wazi baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na mgeni wa Petro de Luanda ya Angola, katika Uwanja wa Novemba 11. Sasa Sundowns wana alama 11 huku De Luanda ya Angola wakiwa katika nafasi ya tatu kwa alama 3.

Wydad Casablanca ya Morocco iliikaribisha USM Alger la Algeria, katika uwanja wa Mohammed 5 mjini Casablanca na mchuano huo kuishia kwa Casablanca kupata ushindi mnono wa mabao 3-1. Mabao ya klabu hiyo yalipatikana katika kipindi cha kwanza kupitia wachezaji Walid al-Karti (7), Badie Aouk (24) na Kazadi Kasengu kabla ya kupigwa kipenga cha kutamatisha kipindi cha kwanza.

Esperance de Tunis ya Tunisia na Raja Casablanca zilivaana siku ya Jumamosi, kutafuta nani zaidi katika Kundi D. Katika mechi hiyo ngumu iliyochezwa mjini Rades, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.

Nembo ya Shirikisho la Soka Afrika linaloandaa Klabu Bingwa

 

Kwengineko, AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikuwa mwenyeji wa JS Kabylie ya Algeria katika Uwanja wa Mashahidi jijini Kinshasa. Na kwa kuwa mcheza kwao hutuzwa, Wakongomani walicharaza wageni mabao 4-1, yaliyovurumishwa na Djuma Shabani, Bangala Litombo, Ernest Luzolo na Kalala Mayele.

Bao la kufutia machozi la wageni lilifungwa na Rezki Hamloune. De Tunis inongoza Kundi D kwa alama 11, Raja Casablanca pointi 8, Vita Club alama 4, alama sawa na Kabaylie inayovuta mkia.    

Dondoo za Hapa na Pale

Inaelekea kuwa, sasa tuzo zinamtafuta hadi uvunguni mwanariadha nyota wa mbio za marathon nchini Kenya Eliud Kipchoge. Siku ya Ijumaa, Kipchoge alitangazwa mwanamichezo bora katika hafla ya kufana iliyofanyika katika Uwanja wa Mombasa Sports Club. Kipchoge pia alitangazwa pia kuwa mwanamichezo bora wa kitengo cha wanaume huku bingwa wa dunia, Hellen Obiri akitwaa tuzo ya wanawake. Miongoni mwa wanamichezo Kipchoge aliwaangusha ni bingwa wa dunia mbio za mita 1,500, bingwa wa Olimpiki na wa dunia mbio za mita 3000 kuruka vizuizi na maji, Conseslus Kipruto. Baada ya kutwaa tuzo hiyo, Kipchoge alikuwa na haya ya kusema, "Nafurahia sana kushinda tuzo hii, inamaanisha watu wametambua niliyofanya Vienna kwa kukimbi chini ya saa mbili katika marathon. Napenda kuwaambia watu kuwa hazikua mbio ya ushindi ila kutuma ujumbe ya kwamba hakuna lisilowezekana dunia."

Mwanariadha Eliud Kipchoge

 

Hii ni katika hali ambayo, kwa mwaka wa pili mfululizo, mwanariadha huyo nyota wa Kenya ameteuliwa kuwania tuzo ya mwanamichezo bora duniani ya Laureus ambayo mshindi atajulikana mnamo Februari 17, mwaka huu 2020 jijini Berlin, Ujerumani. Mwezi uliopita, ikiwa ni wiki moja tu baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima katika masuala ya Sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Laikipia nchini Kenya, Kipchoge alituzwa tena Shahada ya Heshima ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Exeter nchini Uingereza. Kadhalika Mfalme huyo wa mbio za Marathon hivi karibuni aliwabwaga wanaspoti mahiri duniani na kunyakua taji la BBC la kuwa Mwanaspoti Bora wa mwaka Duniani. 

Na aliyekuwa nyota wa mchezo wa mpira wa kikapu wa wa timu ya L.A Lakers ya Marekani Kobe Bryant amefariki dunia pamoja na wenzake wanne kwenye ajali ya helikopta iliyotokea Calabasas jimboni California usiku wa Jumapili ya tarehe 26 Januari. Bryant amepoteza msisha pamoja na bintiye wa miaka 13, Gianna Maria Onore. Chanzo cha ajali hiyo hakijaweza kubainika hadi tunaenda mitamboni. Bryant ambaye ameaga dunia akiwa miaka 41 aliichezea timu hiyo ya Los Angeles kwa karibu miongo miwili, hadi alipostaafu mchezo wa basketboli mnamo Aprili mwaka 2016. Alipulizwa siku moja katika mahojiano amejifunza nini katika miaka 20 ya kucheza mpira wa kikapu alisema.

Mwendazake Kobe Bryant

Kifo chake kimewagusia shakhsia na viongozi mbalimbali wa kisiasa na kijamii ndani na nje ya Marekani.

............................TAMATI...................