May 21, 2020 06:04 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 21 Mei, 2020

Leo ni Alhamisi tarehe 27 Ramadhan mwaka 1441 Hijiria, inayosadifiana na tarehe Mosi Khordad mwaka 1399 Hijria Shamsia sawa na 21 Mei mwaka 2020 Miladia.

Tarehe Mosi Khordad mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsiya ni siku ya kumuenzi Muḥammad Saddruddin Qawam Shirazi maarufu kama Ṣadr al-Muta'allihīn na Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa. Alizaliwa tarehe 9 Jamadil Ula mwaka 980 Hijria Qamaria mjini Shiraz. Awali alielekea katika mji wa Qazvin uliokuwa katika zama hizo mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo ya walimu wakubwa kama Sheikh Bahai. Alisoma Fikihi, Usul, hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na kusoma mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Amma elimu nyingine kuhusu maumbile, hisabati, nujumi na nyota alitabahari nazo kupitia kwa Hakim Abul Qasim Mir Fendereski, mmoja wa maulamaa wakubwa wa zama zake. Mulla Sadra ametoa mchango mkubwa sana kwa falsafa ya Kiislamu. Mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu amevirithisha vizazi vya baada yake zaidi ya vitabu 40 huku kitabu cha  Hikmat Al Muta'alyahfi-l-asfar al-‘aqliyya al-arba‘a  kikiwa maarufu zaidi kuliko vitabu vyake vingine. Mwanafasafa na mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 1050 Hijria mjini Basra Iraq akiwa na umri wa miaka 70 na akazikwa katika mji huo huo. 

Mulla Sadra

Siku kama ya leo miaka 2236 iliyopita, yaani sawa na tarehe 21 Mei mwaka 216 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as), jeshi la mtawala wa Carthage chini ya uongozi wa Hannibal, lilishindwa vibaya huko kaskazini mwa Italia. Hivyo vilikuwa vita vya pili baina ya utawala wa Carthage na Roma kwa anwani ya vita vya 'Punic.' Kwa kutumia tembo na wapandaji tembo mahiri Hannibal alishiriki vita hivyo kabla ya kushindwa vibaya. 

Hannibal

 

Siku kama ya leo miaka 881 iliyopita sawa na 27 Ramadhani mwaka 560 Hijria Qamaria Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arif na msomi mkubwa wa Kiislamu alizaliwa huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka na Baghdad na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".

Ibn Arabi

Siku kama ya leo miaka 331 iliyopita sawa na tarehe 27 Ramadhani mwaka 1110 Hijria Qamaria alifariki dunia Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja wa maulama wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Vitabu vya msomi huyo ni kati ya vitabu muhimu vya marejeo vya maulama wa Kiislamu. Allamah Majlisi alikuwa na uhodari mkubwa katika elimu za dini ya Kiislamu ambapo alifanikiwa kuandika vitabu kadhaa. Katika maisha yake alijishughulisha na kazi ya kuswalisha swala ya Ijumaa, swala za jamaa, kufundisha na kuendeleza hadithi za Mtume Muhammad (saw). Vitabu alivyoviandika Allamah Muhammad Baqir Majlisi ni zaidi ya 600, muhimu zaidi kikiwa ni kitabu cha 'Biharul-Anwaar', 'Hayatul-Quluub' na 'Zaadul-Maad.

 

Allamah Muhammad Baqir Majlisi

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, Andrei Sakharov, mwanafizikia mashuhuri wa Russia alizaliwa. Alihitimu taaluma ya fizikia katika chuo kikuu cha Moscow mwaka 1941 na kisha akaanza kufanya utafiti wa kina kuhusiana na nishati ya nyuklia. Alikuwa na nafsi muhimu katika utengenezaji wa bomu la hydrogen nchini Russia. Sakharov pia alikuwa muungaji mkono mkubwa wa harakati za kutokomeza silaha za nyuklia na ndio maana akatunukiwa zawadi ya amani ya Nobel hapo mwaka 1975. Miaka mitano baadaye Sakharov alibaidishiwa katika mji wa Gorky, mashariki mwa Moscow kutokana na upinzani wake dhidi ya siasa za utawala wa kikomonisti wa Russia. Hata hivyo ubaidishaji huo ulifikia kikomo mwaka 1986 baada ya Mikhail Sergeyevich Gorbachev kutwaa madaraka. Mwanzoni mwa mwaka 1989 Sakharov alichaguliwa kuwa mbunge katika bunge la Russia lakini akaaga dunia baadaye mwezi Disemba mwaka huohuo.

Andrei Sakharov,

Miaka 40 iliyopita tarehe Mosi Khordad mwaka 1359 Hijria Shamsia mzingiro wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulianza. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani ilipoteza maslahi yake haramu nchini Iran kwa lengo la kuwashinikiza wananchi Waislamu na wanamapambano wa Iran. Aidha lengo la mzingiro huo wa kiuchumi lilikuwa ni kuulazimisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ukubali kuwa na uhusiano wa kawaida na Marekani. Kufuatia uamuzi huo wa utawala wa Marekani, Imam Khomeini MA, muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alitangaza bayana kuwa uhai wa kiuchumi wa mataifa hautegemei madola makubwa na akilihutubu taifa la Iran alisema: "Msitishwe hata kidogo na mashinikizo hayo ya kiuchumi kwani iwapo watatuwekea vikwazo vya kiuchumi watakuwa wametupa fursa ya sisi wenyewe kujitegemea kiuchumi. Watu wanaotishwa na vikwazo vya kiuchumi ni wale wanaoona kuwa uchumi ndio msingi wa kila kitu na dunia ndio mwanzo na mwisho wao."

Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 21 mwezi Mei mwaka 1991 aliuawa Rajiv Gandhi Waziri Mkuu wa zamani wa India. Gandhi alikuwa mwana wa Indra Gandhi Waziri Mkuu wa zamani wa India. Alizaliwa Agosti 20 mwaka 1944 huko Mumbai (Bombay) na kukulia nyumbani kwa babu yake Jawaharlal Nehru waziri Mkuu wa kwanza wa India. Baadaye Rajiv Gandhi alipata masomo katika Chuo Kiku cha Cambridge Uingereza na kisha kujiunga na Shirika la Ndege la India baada ya kuhitimu masomo ya urubani. Rajiv aliingia katika siasa baada ya kifo cha mdogo wake wa kiume ambaye alikuwa akitajwa kuwa mrithi wa Indira Gandhi. Rajiv alichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mdogo.  Mwaka 1983 Rajiv Gandhi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama cha Kongresi ambacho kilikuwa chama tawala na kukipanga upya. Rajiv alishindwa katika uchaguzi wa bunge la wawakilishi na mwaka 1989 alijiuzulu  baada ya kuwa Waziri Mkuu wa India kwa miaka 5. Rajiv Gandhi alikuwa na nia ya kushiriki katika uchaguzi huo wa bunge la India hata hivyo tarehe 21 Mei mwaka 1991 akiwa na umri wa miaka 47 aliuawa katika mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wa kampeni za uchaguzi kusini mwa India.  

 

Rajiv Gandhi