Ijumaa, tarehe 22 Mei, 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 28 Ramadhan mwaka 1441 Hijiria, inayosadifiana na Pili Khordad 1399 Hijria Shamsia sawa tarehe 22 Mei mwaka 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1167 iliyopita 28 Ramadhani mwaka 272 Hijria Qamaria aliaga dunia Abu Ma'ashar Balkhi mmoja wa wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya hadithi wa Kiirani. Alielekea Baghdad mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Katika zama zake Abu Ma'ashar Balkhi alikuwa mnajimu mashuhuri kabisa wa Kiislamu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawalid as-Saghirah.

@@@
Siku kama hii ya leo miaka 135 iliyopita sawa na tarehe 22 mwezi Mei mwaka 1885 aliaga dunia mwandishi na malenga mtajika wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 83 kwa jina la Victor Hugo. Hugo alikuwa mfuasi wa mageuzi kwa maslahi ya wale waliokandamizwa na kudhulumiwa. Alizaliwa mwaka 1802 miladia na alianza kughani mashairi tangu akiwa kijana. Akiwa na umri usiopindukia miaka 25 Hugo alikuwa mwanachama katika akademia ya Ufaransa na wakati huo huo akawa mbunge katika bunge la Ufaransa. Victor Hugo aliamua kuachana na masuala ya siasa wakati wa utawala wa Napoleon wa Tatu kutokana na kupinga kwake siasa za kibeberu za mtawala huyo na kuelekea uhamishoni kwa miaka 20.
Siku kama hii ya leo miaka 34 iliyopita Omar Tilmisani mmoja wa viongozi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1904 katika eneo la Tilmisan nchini Algeria. Mwaka 1924
Tilmisani alihitimu masomo yake ya shahada katika taaluma ya sheria na mwaka 1928 akawa mwanachama wa Ikhwanul Muslimin baada ya kuasisiwa harakati hiyo. Tilmisani ambaye alimpita kwa miaka miwili Hassan al Banna kiongozi wa harakati hiyo anahesabiwa kuwa mmoja wa makada wakongwe wa harakati hiyo. Hatimaye Omar Tilmisani aliaga dunia tarehe 22 Mei 1986 akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kupatwa na maradhi ya ini na figo.
@@@
Siku ya leo miaka 29 iliyopita pili Khordadi mwaka 1370 Hijria Shamsia Waislamu duniani walilalamikia vikali hatua ya utawala wa chama cha Baath cha Iraq ambao ulivunjia heshima maeneo matakatifu ya Kiislamu nchini humo. Baada ya wananchi Waislamu wa Iraq kuanzisha muamko kupinga jinai nyingi za utawala wa Baath, Saddam Hussein dikteta wa wakati huo Iraq alitoa amri ya kuuawa bila huruma wananchi na kuhujumiwa maeneo matakatifu ya Kiislamu nchini humo. Kitendo hicho cha utawala wa baath kiliibua hasira za Waislamu hasa Waislamu wa madhehebu ya Shia ambao walifanya maandamano kupinga jinai hizo. Jinai hizo zilitendeka ukiwa umesalia muda mfupo kabla ya wananchi wa Iraq kupata ushindi dhidi ya Saddam. Katika kipindi hicho, Marekani na waitifaki wake walimsaidia Saddam kuua na kuwakandamiza wananchi. Hata baada ya wananchi kutafuta hifadhi katika maeneo matakatifu, Jeshi la Saddam liliwahujumu wakiwa katika maeneo hayo.Baada ya kupinduliwa utawala wa Saddam, kulipatikana makaburi mengi ya umati na hivyo kikabainika kiwango cha jinai za Saddam dhidi ya wananchi.
Miaka 9 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 2 Khordad mwaka 1390 Hijria Shamsia, Nasser Hijazi mchezaji na kocha mashuhuri wa soka nchini Iran aliaga dunia. Nasser Hijazi alizaliwa mwaka 1949 sawa na mwaka 1328 Hijria Shamsia mjini Tehran. Aliwahi kuwa golkipa wa Klabu ya Esteghlal na Timu ya Taifa ya Iran. Alijiunga na timu ya taifa ya Iran katika Kombe la Dunia la FIFA mwaka 1978 na alikuwa kipa nambari moja wa timu hiyo. Hijazi aliendelea kuwa kipa wa timu ya taifa ya Iran hadi mwaka 1980. Mnamo mwaka 1986 akiwa na umri wa miaka 36 alistaafu kama mchezaji na akaelekea nchini Bangladesh na kuwa kocha wa Klabu ya Mohammedan. Akiwa kocha wa Mohammedan timu hiyo iliweza kufanikiwa na kuwa kati ya vilabu bora nane vya bara Asia. Aliporejea Iran Hijazi alikuwa kocha mwenye mafanikio wa timu kama vile Bank Tejerat na Shahredari Kerman, Mashine Sazi Tarbiz, Zobahan na Sepahan Isfahan. Hali kadhalika alikuwa kocha wa timu za Nasaji Mazandaran, Esteghlal Tehran, Esteghlal Rasht na Esteghlal Ahvaz. Nasser Hijazi anatazamwa kama mmoja kati ya wachezaji mashuhuri na waliopendwa zaidi nchini Iran. Mwaka 1999 Shirikisho la Soka Asia lilimtambua kama kipa wa pili bora wa karne barani Asia. Mwaka 1988 aliugua na kulazwa hospitalini na hatimaye tarehe Pili Khordad akaaga dunia.