Jun 04, 2020 02:29 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 4 Juni, 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe 12 Shawwal 1441 Hijria sawa na Juni 4 mwaka 2020.

 Siku kama ya leo miaka 411 iliyopita aliaga dunia alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Bahauddin Muhammad Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai. Sheikh Bahai ambaye alikuwa mtaalamu wa fiqhi, nujumu na hesabati alifariki dunia katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alizaliwa mwaka 952 Hijria katika mji wa Baalabak huko Lebanon katika familia ya Kiirani. Baba yake alikuwa miongoni mwa mashekhe wakubwa wa zama hizo. Sheikh Bahai ameandika vitabu vingi ikiwa ni pamoja na Tashrihul Aflak, Kashkul na Hablul Matin.

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Khordad 1342 Hijria Shamsia sawa na tarehe 5 Juni 1963 Milaadia, wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa dhidi ya utawala wa Shah, baada ya kusikia habari ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini MA. Imam alitiwa mbaroni na vibaraka wa utawala wa Shah siku kadhaa nyuma kufuatia hotuba yake ya kihistoria aliyoitoa katika mji wa Qum, ambayo ilifichua njama mbalimbali za utawala wa Shah dhidi ya taifa la Iran. Ni wazi kuwa mapambano ya umwagaji damu na ya kihistoria ya tarehe 15 Khordad, yalikuwa nukta ya kuanza mapinduzi ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah na kufungua njia ya mustakbali wa kisiasa na kijamii nchini.

 Maandamano ya Khordad mwaka 1342 Hijria Shamsia

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, serikali ya China ilishambulia na kuwaua wanachuo wengi katika uwanja wa Tiananmen huko Peking mji mkuu wa nchi hiyo. Siku hiyo na licha ya kuwepo onyo la serikali dhidi ya kufanyika maandamano hayo, lakini maelfu ya wanachuo walikusanyika katika uwanja huo ili kuishinikiza serikali iruhusu kuwepo uhuru wa shughuli za kisiasa, kupunguzwa uwezo wa chama cha kikomonisti, kuongezwa uwezo wa bunge na kuchaguliwa wabunge na wananchi moja kwa moja. Baada ya kuona kuwa maandamano ya wanachuo yalikuwa yanaongezeka badala ya kupungua, polisi na jeshi la China liliamua kuyavunja maandamano hayo kwa nguvu kwa kuua na kuwakandamiza wananfunzi.

Uwanja wa Tiananmen

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia Waathirika wa Unyanyasaji (International Day of Innocent Children Victims of Aggression). Siku hiyo ilitangazwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1982 kwa ajili ya kushughulikia mashaka ya watoto wanaosumbuliwa na unyanyasaji wa kimwili, kiakili na kiroho kufuatia hali mbaya ya watoto wa Palestina na Lebanon wanaosumbuliwa na ukatili wa utawala haramu wa Israel. Ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto una sura na aina mbalimbali na unasababishwa na uzembe wa wazazi, viongozi wa kitaifa na kimataifa na makatili wasio na chembe ya huruma wanaojali maslahi yao ya kimaada.