Ijumaa tarehe 7 Agosti mwaka 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 17 Dhulhija 1441 Hijria sawa na Agosti 07 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita sawa na Agosti 7 1960 nchi ya Ivory Coast ilifanikiwa kujipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno waliidhibiti nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika katika karne ya 16, lakini ulipofika mwaka 1891 Ufaransa iliidhibiti nchi hiyo, licha ya upinzani mkubwa wa wananchi wa Ivory Coast. Hatimaye ulipofika mwaka 1960, Ivory Coast ikiwa pamoja na nchi nyingine kadhaa za Kiafrika zilizokoloniwa na Mfaransa zilijipatia uhuru wao.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita mwafaka na tarehe 7 Agosti 1982, yalitiwa saini makubalino ya kuondoka vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) mjini Beirut Lebanon kati ya Marekani, Lebanon na PLO. Makubaliano hayo yalitiwa saini kufuatia shambulio kubwa lililofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Lebanon mwezi Juni 1982 kwa shabaha ya kuwafukuza wapiganaji wa PLO nchini Lebanon. Ijapokuwa kuondoka wanamgambo wa PLO nchini Lebanon kulitoa pigo kubwa kwa harakati hiyo, lakini miaka ya baadaye Wazayuni maghasibu walikabiliwa na kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano wa harakati ya muqawamah ya Lebanon, na kulazimika kuondoka kwa madhila katika ardhi ya nchi hiyo mwaka 2000.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita mwafaka na tarehe 17 Mordad 1371 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Alhaj Sayyid Abul Qassim al Mussawi al Khoui, faqihi na marjaa mkubwa wa Kiislamu duniani, akiwa na umri wa miaka 96. Mwanachuoni huyo mashuhuri alizaliwa katika mji wa Khoui ulioko kaskazini magharibi mwa Iran na akiwa katika umri wa ubarobaro, alifuatana na baba yake mjini Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. Katika zama za umarjaa wake, Ayatullahil Udhma al Khoui alitoa fatwa inayosisitiza udharura wa kuilinda Palestina na kuikomboa Quds Tukufu kutoka mikononi mwa Wazayuni maghasibu. Alimu huyo mkubwa ameacha vitabu vingi vikiwemo 'Jawaahirul Usuul', 'Muntakhabu Rasaail', 'al Bayaan Fii Tafsiiril Qurani' na "Misbahul Faqaha".
Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita vikosi vya jeshi la Georgia vikisaidiwa na serikali ya Marekani vililishambulia eneo linalopigania kujitenga la Ossetia ya Kusini huko kaskazini mwa nchi hiyo. Mamia ya raia wasio na hatia wala ulinzi waliuawa na kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo. Siku moja baadaye, wanajeshi wa Russia waliingilia kati na kuamua kuwaunga mkono wapiganaji wanaopigania kujitenga wa Ossetia ya Kusini na kulilazimisha jeshi la Georgia kurudi nyuma. Vikosi vya jeshi la Russia vilifanikiwa kuiteka bandari muhimu ya Patumi na kusonga mbele karibu na Tiblis mji mkuu wa nchi hiyo. Jeshi la Russia liliondoka huko Georgia Agosti 12 kwa upatanishi wa Rais wa Ufaransa, na Moscow ikayatambua rasmi kuwa huru maeneo mawili yaliyokuwa yakipigania kujitenga yaani Ossetia ya Kusini na Abkhazia.