May 07, 2022 01:17 UTC
  • Jumamosi, 7 Mei, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 5 Mfunguo Mosi Shawwal 1443 Hijria sawa na tarehe 7 Mei 2022 Miladia.

Miaka 214 iliyopita katika siku kama ya leo wananchi wa Uhispania walianzisha harakati dhidi ya vikosi vya jeshi la Mfalme Napoleon wa Ufaransa, vilivyokuwa vinakalia kwa mabavu nchi yao. Wakati huo Uhispania pia ilikuwa ikihesabiwa kuwa moja ya makoloni makubwa ya Ulaya na ilikuwa ikikalia kwa mabavu ardhi nyingi nje ya bara hilo. Lakini wananchi wa Uhispania walikuwa wameonja uchungu wa nchi yao kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya kigeni. Baada ya miaka mitano ya mapambano dhidi ya vikosi vamizi vya Ufaransa, walifanikiwa kuvifukuza vikosi hivyo mwezi Disemba mwaka 1813 kutoka nchini kwao. Wakati huo huo kutokana na kushindwa katika Amerika ya Kusini, Uhispania ililazimika kuziacha huru nchi kadhaa ilizokuwa ikizikoloni.  ***

Uhispania

 

Siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, alizaliwa Robert Browning, malenga na mwanafikra wa nchini Uingereza. Akiwa kijana mdogo Browning alikuwa na maandalizi ya kuwa malenga ambapo alitoa shairi lake la kwanza akiwa na umri wa miaka 12. Taratibu akaanza kupata umashuhuri katika jamii ya Uingereza kama malenga mkubwa. Robert Browning alikuwa akiwasilisha itikadi yake juu ya umoja wa Mungu duniani kupitia mashairi yake. Ameacha athari nyingi katika uwanja huo. Robert Browning alifariki dunia mwaka 1889. ***

Robert Browning

 

Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mei 1888, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilianzisha uvamizi katika ardhi ya Zimbabwe ya sasa. Mipango ya kuikalia kwa mabavu Zimbabwe ilibuniwa na mwanasiasa na mfanyabiashara aliyejulikana kwa jina la Cecile Rhodes, ambaye aliasisi shirika la Afrika Kusini la Kiingereza nchini humo. Kwa kusaidiwa na jeshi la Uingereza, Rhodes aliuwa kwa umati maelfu ya raia wazalendo na kuwakamata mateka wengine wengi, na hivyo kuweza kuidhibiti ardhi yote ya Zimbabwe na kuipachika jina lake la Rhodesia. ***

Zimbabwe

 

Na siku kama ya leo tarehe 5 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 60 Hijria Muslim bin Aqil, binamu wa Imam Hussein AS aliwasili katika mji wa Kufa, moja kati ya miji ya Iraq, kwa shabaha ya kuwalingania wenyeji wa eneo hilo kwenye njia ya haki na kumpa mkono wa utiifu mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw). Kabla ya hapo watu wa Kufa walikuwa wamemwandikia barua nyingi Imam Hussein AS wakimuomba aende kwenye mji huo na awaongoze kwenye harakati dhidi ya utawala wa kidikteta wa Bani Umayyah. Baada tu ya Muslim bin Aqil kuwasili katika mji wa Kufa aliwasomea wenyeji wa mji huo barua ya Imam Hussein A.S iliyowakaribisha kujiunga na harakati ya kiongozi huyo. Mwanzoni watu wa mji wa Kufa walikubali ujumbe wa Imam Hussein lakini baadaye walikengeuka. Mwishowe watu wa Kufa walimuacha peke yake Muslim bin Aqil na mjumbe huyo wa Imam Hussein akauawa shahidi na askari wa utawala wa Bani Umayyah. ***