Oct 09, 2022 02:21 UTC
  • Jumapili, 09 Oktoba, 2022

Leo ni Jumapili tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1444 Hijria sawa na tarehe 9 Oktoba 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1497 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Masoudi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW. Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu. ***

Wiki ya Umoja

 

Tarehe 12 Rabiul Awwal mwaka wa kwanza Hijria, Mtume Muhammad (saw) aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti wa kwanza kabisa katika Uislamu katika kijiji cha Quba kilichoko pambizoni mwa Madina. Mtume (saw) aliweka jiwe la msingi la msikiti huo wa kihistoria wakati aliposimama kwa siku chache katika eneo la Quba akiwa njiani kutoka Makka na kuelekea Madina. Mtukufu huyo alisimama kwa muda katika kijiji cha Quba akimsubiri Ali bin Abi Twalib na jamaa wa familia ya Mtume. ***

Muonekano wa sasa wa msikiti wa Quba

 

Katika siku kama ya leo tarehe 12 Rabiul Awwal miaka 1203 iliyopita, alifariki dunia Imam Ahmad bin Hanbal mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Baghdad, Iraq ya leo. Ahmad bin Hanbal alizaliwa mwaka 164 Hijria, katika mji wa Baghdad na kupata elimu ya kidini katika mji huo kutoka kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Shafii. Imam Hanbal alifanya safari katika miji kadhaa kama vile Kufa, Basra, Makka, Madina, Sham na Yemen kwa minajili ya kukusanya hadithi za Bwana Mtume SAW. Ahmad bin Hanbal ndiye mwasisi wa madhehebu ya Kisuni ya Hanbal na mwandishi wa kitabu mashuhuri cha hadithi cha al Musnad. ***

Imam Ahmad bin Hanbal

 

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, yaani tarehe 9 Oktoba 1962, nchi ya Uganda ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kuanzia mwaka 1890 Uganda ilikuwa chini ya makampuni ya Kiingereza yaliyokuwepo Afrika Mashariki, na baada ya kupita miaka kadhaa, ikatawaliwa rasmi na Uingereza. Baada ya kutawaliwa na mkoloni Muingereza, wananchi wa Uganda walipigania uhuru na hatimaye walifanikiwa kujipatia uhuru wao mwaka 1962 katika siku kama ya leo. Uganda yenye ukubwa wa kilomita mraba 235,880 kijiografia ipo mashariki mwa Afrika na inapakana nan chi za Sudan, Kenya, Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.***

Bendera ya Uganda

 

Miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Ernesto Che Guevara mwanamapinduzi mashuhuri wa Amerika ya Latini pamoja na wenzake kadhaa. Che Guevara alizaliwa mwaka 1928 nchini Argentina. Fikra ya Ernesto Che Guevara ya kuendesha mapambano dhidi ya ubepari ilizidi kupanuka baada ya kushuhudiwa umaskini na ubaguzi uliotokana na siasa za kipebari za Marekani za kuyanyonya mataifa ya Amerika ya Latini. Ernesto che Guevara alifahamiana na Fidel Castro huko Mexico na viongozi hao wawili ndio walioongoza mapinduzi ya Cuba hadi kupatikana ushindi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Cuba mwaka 1959, Che Guevara alielekea Bolivia na kuasisi kundi la wapiganaji wa msituni. Alianza kupambana na serikali ya nchi hiyo iliyokuwa tegemezi kwa Marekani. Lakini katika siku kama ya leo mwaka 1967, wanajeshi wa Bolivia wakisaidiwa na shirika la ujasusi la CIA waligundua maficho ya Che Guevara na kumuuwa kwa kummiminia risasi. ***

Ernesto Che Guevara

 

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Majid Abu Sharar, shakhsiya mwingine wa Palestina aliuawa na utawala haramu wa Israel huko nchini Italia. Abu Sharar ambaye alikuwa afisa wa kampeni wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO aliuawa na vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mosad mjini Roma, Italia. Israel imekuwa ikitumia njia ya kuwauwa kigaidi shakhsiya mbalimbali wa Palestina kama moja ya njia zake kuu za kusitisha mapambano ya ukombozi ya Wapalestina. ***

Majid Abu Sharar

 

Na leo tarehe 9 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Posta. Posta ndio chombo cha kale zaidi na kikubwa cha mawasiliano baina ya wanadamu wa nchi na maeneo mbalimbali ya dunia. Taasisi hiyo ya posta ni miongoni mwa asasi za kijamii zilizobakia hai hadi leo. Kutumiana ujumbe na barua ni miongoni mwa haja za kijamii za wanadamu tangu kiumbe huyu alipoanza maisha ya kijamii na posta ndiyo iliyokuwa chombo cha kukidhi mahitaji hayo kwa miaka mingi. ***

Siku ya Posta Duniani

 

Tags