Nov 06, 2022 12:26 UTC
  • Teleskopu ya Iran ambayo ni miongoni mwa bora zaidi duniani

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya taarifa katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Katika hatua kubwa kwa jumuiya ya wanasayansi ya Iran, wanaastronomia wa Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali cha Iran (INO) wameweza kupata mafanikio makubwa.

Wanaastronomia  wa Iran wameweza kuunda teleskopu ya kiwango cha kimataifa ya mita 3.4 inafanya kazi na tayari imepata picha zake za kwanza kutoka anga za mbali.

Akizungumza na jarida la Kimataifa la Science Mkurugenzi wa Mradi wa INO Habib Khosroshahi, mwanaastronomia katika Taasisi ya Utafiti wa Sayansi ya Msingi (IPM) mjini Tehran amesema, "Tumekuwa tukisubiri wakati huu kwa muda mrefu.",

Mradi huu wa Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali (observatory) cha  Iran ulianzishwa takriban miaka 20 iliyopita, ukilenga uundaji wa teleskopu ya  kiwango cha kati ili kutoa huduma za utafiti kwa watumiaji wa kitaifa. Kutokana na eneo lake la kijiografia, teleskopu hiyo inatarajiwa kuvutia watumiaji wa kimataifa. Kampeni ya kuchagua eneo la kujenga teleskopu ilihitimishwa kwa kuchaguliwa Mlima Gargash ulioko mita 3600 juu ya usawa wa bahari katikati mwa Iran, kilomita 100 kaskazini mwa jiji la Isfahan.

Khosroshahi amesema, "Kwa ubora huu wa ajabu wa picha, mwanzoni mwa uzinduzi wa teleskopu hii, tulionyesha kuwa vifaa vya udhibiti vyenye makumi ya maelfu ya vipuri, hufanya kazi kwa pamoja na itawawezesha wanaastronomia wetu kuchunguza maeneo yote ya anga za mbali yanaoweza kufikiwa na kituo hiki cha kisasa.”

Gerry Gilmore, mwanaastronomia katika Chuo Kikuu cha Cambridge na mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya kimataifa ya Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali cha Iran, alisema  wakati wanasayansi wa Iran walipoanzisha mradi huu, ilikuwa ndoto tu. Hakuna mtu nchini Iran aliyejaribu chochote kwa kiwango hiki hapo awali.

Picha iliyopigwa na teleskopu hiyo (upande wa kulia juu)

Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali cha Iran kilifungua kuba lake mnamo tarehe 27  Septemba na usiku uliofuata teleskopu katika kituo hicho ikapiga picha ya Arp 282, ambayo ni mjumuiko wa galaksi zilizo umbali wa miaka milioni 319 ya mwanga (mwakanuru) kutoka sayari ya dunia.

Katika ujenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali cha Iran wanaastronomia nchini Iran walilazimika kuvuka vikwazo ambavyo aghalabu ya wanaastronomia  wenzao duniani hawakabiliani navyo. Vikwazo hivyo vilipunguza uagizaji wa teknolojia ya juu, na vizuizi vya kusafiri kwao nje ya nchi. Pamoja na hayo wengi duniani wameshangaa kutokana na uwezo wa Iran wa kuunda teleskopu ambayo ni miongoni mwa teleskopu bora zaidi duniani pamoja na kuwa Marekani imeiwekea nchi hii vikwazo.

 

Timu ya wavumbuzi wa Iran ilinyakua medali ya dhahabu katika Maonyesho ya 46 ya Kimataifa ya Uvumbuzi (INOVA 2022), ambayo yalifanyika Osijek, Kroatia, mnamo Oktoba 12-15.

Tukio hilo liliandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wavumbuzi (IFIA) na Mashirika ya Haki Miliki ya Uvumbuzi Duniani (WIIPA).

Timu elfu moja kutoka nchi 40 zikiwemo Ujerumani, Marekani, Japan, China, Korea Kusini, Uswizi, Uswidi, Norway, Ufaransa, Singapore, Kanada, Indonesia na Iran zilishiriki katika mashindano ya INOVA.

Timu ya Iran ilifanikiwa kushinda medali ya dhahabu katika kitengo cha utangazaji na utalii.

Iran inashika nafasi ya 11 duniani katika uga wa haki miliki, kwa mujibu wa ripoti ya Viashiria vya Haki Miliki Duniani (World Intellectual Property Indicators) 2021.

Viashiria vya Haki Miliki Duniani ni ripoti ya kila mwaka iliyochapishwa na Shirika la Haki Miliki Duniani (WIPO), inayotoa viashirio mbalimbali vinavyohusu kategoria haki miliki. Inatumia data kutoka kwa ofisi za Haki Miliki za Kitaifa na kikanda, WIPO, Benki ya Dunia, na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). WIPO imechapisha ripoti hizo kila mwaka tangu 2009.

Iran inashika nafasi ya 21 kwa idadi ya maombi ya hataza, ya 3 kwa alama za biashara, na ya 12 kwa miundo ya viwandani, ambayo inajumuisha programu na vifaa vyenye uvumbuzi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei aliutaja mwaka wa sasa wa Irani (Machi 2022-Machi 2023) kuwa mwaka wa "Uzalishaji wa Kutegemea Teknolojia na Utengenezaji Ajira. Kuimarisha kampuni zinazotegemea maarifa ya kiteknolojia ziko kwenye ajenda kuu ya Iran.

Msingi huo, makao makuu ya kimkakati ya maendeleo ya teknolojia yaliundwa na miradi 362,000 ya kiteknolojia na miradi 154 ya kibiashara imepata msaada mwaka huu, sambamba na uzinduzi wa miradi 23 ya kitaifa.

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani WHO inakadiria kuwa watu milioni 10.6 waliugua kifua kikuu (TB) mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.5 kutoka mwaka 2020, na watu milioni 1.6 walikufa kutokana na TB kati yao watu 187,000 wakiwa na Virusi Vya UKIMWI.

Taarifa ya shirika hilo kutoka Geneva Uswisi imesema ripoti hiyo ya mwaka 2022 ya Kifua Kikuu imeonesha kuwa hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mingi kuwa na ongezeko wa wagonjwa wa kifua kikuu na wengine asilimia 3 wamepata usugu wa dawa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ametaja janga la COVID-19 kuwa kichocheo cha watu wengi kukosa dawa za kujitibu kifua kikuu.

 “Kama kuna kitu tumejifunza kutokana na janga la CORONA ni kwamba kwa mshikamano, kufanya maamuzi, uvumbuzi na utumiaji sawa wa zana, tunaweza kushinda vitisho vikali vya kiafya. Hebu tutumie masomo hayo kwenye eneo la kifua kikuu. Ni wakati wa kumkomesha muuaji huyu wa muda mrefu. Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kukomesha TB.”

Ugonjwa wa Kifua kikuu ni muuaji wa pili wa magonjwa ya kuambukiza duniani, baada ya COVID-19.

Ugonjwa huu husababishwa na bakteria ambao mara nyingi huathiri mapafu, lakini unaweza kuzuilika na kutibika.

Huduma za afya kwa ujumla ziliathiriwa sana wakati wa janga la COVID-19, lakini athari zake kwa wagonjwa wa TB imekuwa mbaya sana, hali ambayo imekuwa mbaya zaidi kutokana na migogoro inayoendelea huko Ulaya, Afrika pamoja na Mashariki ya Kati.

Kuendelea kwa changamoto za kutoa na kupata huduma muhimu za TB kumesababisha watu wengi waliokuwa na ugonjwa huo kutogunduliwa na kutibiwa.

 

Na Tarehe 14 Oktoba 2021 Mheshimiwa Rais Samia akizungumza katika kilele cha Mbio za Mwenge kitaifa kwenye Viwanja vya Magufuli, Wilayani Chato, Mkoani Geita, alisema Serikali inatarajia kujenga chuo bora zaidi cha kisasa cha Teknolojia ya Habari na Mawasilino (TEHAMA) ili kuongeza kasi, ubunifu na ufanisi katika matumizi ya teknolojia hiyo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Korea imekubali kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasilino  nchini Tanzania. Majaliwa amesema kuwa lengo la chuo hicho ni kuwasaidia vijana kuendeleza ubunifu wao na kuonesha namna wanavyoweza kuunda vifaa mbalimbali “Mpango wa Rais wetu wa kuwapa vijana shughuli za kufanya katika eneo la Sayansi na Teknolojia ni mpango ambao unaungwa mkono na Serikali ya Korea.” Waziri Mkuu amesema hayo Oktoba 27, 2022 baada ya kumaliza mazungumzo ya kiserikali na Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Han Duck-Soo katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu uliopo Seoul.