Dec 26, 2022 08:04 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (48)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 48 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitaendelea kuzungumzia umuhimu wa kuwa na izza na heshima na athari za kujitawala kisiasa katika Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Kama unavyokumbuka mpendwa msikilizaji, katika kipindi kilichopita tulianza kuzungumzia kujitawala na kujitegemea kisiasa katika utamaduni wa kisiasa wa Uislamu na tukakumbusha kuwa, kujitawala kisiasa kunaupa umma wa Kiislamu moyo wa kukomboka na kuwa huru, heshima na uwezo wa kuyakabili madola mengine na kuhuisha pia ndani ya nyoyo za Waislamu utamaduni wa muqawama na kusimama imara.

Matunda mengine muhimu ya kujitawala kisiasa ni kupata moyo wa kuwa na izza na kukataa kudunishwa na kudhalilishwa. Hapana shaka, sharti la kuifikia izza na heshima ni kuwa na azma thabiti, kuvumilia shida, vitisho, mashaka na misukosuko, ambayo vinara wa ukafiri duniani waliyatia na wataendelea kuyatia mataifa yenye fikra huru; ambapo tukiachilia mbali mifano kadhaa muhimu iliyotokea huko nyuma katika historia, kwa sasa tunaweza kuliashiria taifa shujaa la Palestina, taifa lisilotetereka la Yemen na wananchi waliosimama imara wa Syria, ambao licha ya kufikwa na masaibu mazito ya uvamizi, moto wa vita, mauaji ya halaiki na jinai za madola ajinabi, wangali wamesimama imara na hawako tayari kulegeza msimamo na kudhalilishwa, jambo ambalo limewafanya kuwa kigezo na mfano wa kujivunia wa kutetea izza na heshima kwa mataifa yanayongonyeshwa duniani na vizazi vijavyo vya jamii ya wanadamu.

Ni jambo lisilo na shaka kuwa, miongoni mwa nukta muhimu zaidi na yenye kutoa msukumo wa kutetea izza na heshima ni kushikamana na utamaduni wa Tauhidi, wa Uislamu halisi na wa asili, ambao unawapa ilhamu wafuasi wake wanaoshikamana na njia iliyonyooka, kama aya ya nane ya Suratul-Munafiqun inavyosema: "Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui". 

Kusema kweli, tofauti ya waumini wa kweli na wanafiki wanaojionyesha kidhahiri tu kuwa ni Waislamu ipo katika usuli na msingi mkuu wa itikadi juu ya Mungu pekee wa haki, ambaye ni dhihirisho la vielelezo na nembo zote za "izza" na utukufu.

Kwa ufafanuzi wa wazi zaidi ni kwamba, izza na uwezo wa kimaada ulioshuhudiwa katika historia ni wa kidhahiri tu na unaolegalega, kwa sababu umeshuhudiwa ukiporomoka pale ulipokumbana na misukosuko ya kisiasa na kijamii. Lakini izza na nguvu zitokanazo na Mwenyezi Mungu ni thabiti na za uhakika; na hakuna tukio au sababu inayoweza kuziyumbisha kwa namna yoyote ile; na kila pale Yeye Mola mwenye izza anapotaka kutuonyesha udhaifu wa madhihirisho ya nguvu za kibinadamu, huzisambaratisha na kuzitokomeza tawala zao kwa matukio na sababu ndogo kabisa. Mfano wa hilo tunaweza kuashiria kifo chenye kutoa ibra na mazingatio cha Namrud, dikteta wa zama za Nabii Ibrahim AS, ambaye alizivunja nguvu zake na kumwangamiza kwa kuingiwa na mbu tu ubongoni mwake. Au tunaweza kuashiria pia kisa cha mtawala dikteta wa Misri Firauni, ambaye alipofikia kilele cha nguvu za madaraka alifika hadi ya kuwaambia watu: "Mimi ndiye Mola wenu Mlezi mkuu kabisa"; na pia akawaelekea na kuwaambia: "Sijui kama mnaye mungu asiyekuwa mimi". Lakini Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla alimgharikisha kwenye mawimbi makali ya Mto Nile na kisha akakiacha kiwiliwili chake kielee juu ya maji kama gogo ili liwe funzo na mazingatio kwa wengine katika historia, wanaojivunia nguvu zao bandia.

Mfano mwingine wenye mazingatio makubwa uliozungumziwa na Qur'ani katika sura ndogo ya al-Fil unahusu jeshi kubwa na lenye nguvu la Abraha, aliyejizatiti kivita kwa madhumuni ya kwenda kuibomoa Nyumba ya Mwenyezi Mungu ya Al-Kaaba ili kwa dhana yake aifute moja kwa moja imani ya Tauhidi. Lakini Mwenyezi Mungu Muweza Asiyeshindika aliliteremshia jeshi la Abraha kikosi cha ndege waitwao Abaabil waliobeba changarawe za udongo mgumu, wakawavurumizia kwenye ubongo askari waliopanda tembo wa jeshi la Abraha na kuwaangamiza. Katika aya ya mwisho ya Suratul-Fil, Qur'ani imezungumzia jinsi hali za watu hao zilivyokuwa baada ya kuangamizwa kwa kusema: "Akawafanya kama majani yaliyo liwa!" 

Ni vyema tukakumbusha hapa kuwa, lengo la Mola kuzungumzia kuporomoka kwa wenye nguvu za mali na madaraka au tamaduni na staarabu zilizokuwa zikitajika si kusimulia hadithi na visa, lakini madhumuni ya kufanya hivyo ni kuzifanya tawala na mataifa yapate ibra na mazingatio na kuwa na yakini kwamba, atakapo Yeye Mola, hakuna nguvu zozote za kibinadamu zinazoweza kuhimili irada yake, maana zitasambaratika na kutoweka. Tufahamu pia kuwa, maana ya irada ya Mwenyezi Mungu ya kwamba atakapo jambo liwe linakuwa, si watu wa mataifa kutokuwa na wajibu wowote wa kufanya ili wajitawale na kufikia maisha ya izza na heshima na kwamba wakae tu ili kungojea majabari na madhalimu waangamizwe kwa nguvu za Mwenyezi Mungu. Kama ingekuwa ni hivyo, katika aya nyingi za Qur'ani, Mwenyezi Mungu Mtukufu asingetoa amri ya Jihadi na kupigana vita, wala kuwataka Waislamu wajizatiti na kujiimarisha kijeshi kwa ajili ya kupambana na watawala majabari na madikteta. Aidha asingewaamuru Mitume wake waikabili na kupambana nayo mifumo ya kitaghuti na watawala wake. Kwa hivyo sambamba na irada na msaada wa Mwenyezi Mungu, mataifa yenyewe ya Waislamu, nayo pia yanatakiwa yasimame kupigania kujitawala na kuwa na maisha yenye izza na heshima na kupambana kwa uwezo wao wote kulinda mipaka ya heshima, izza na utukufu wao.

Mbali na harakati za kusimamia izza, kujitegemea na kujitawala kisiasa zilizoendeshwa na Mitume waliotangulia na kufuatiwa na harakati ya Bwana Mtume Muhammad SAW, ambapo maandiko mbalimbali ya kuaminika ya historia yamebainisha jinsi mtukufu huyo alivyopigana vita na madhihirisho ya ukafiri, shirki na unafiki; na pia vita vya kihistoria alivyopigana Imam Ali AS na maadui wa Uislamu wakati wa uongozi wake, historia imeshuhudia pia harakati iliyotoa ilhamu na kuacha kumbukumbu ya milele ya Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein AS, ambayo imedhihirisha kwa uwazi kabisa uhakika kwamba, kufikia kilele cha izza na heshima kunahitaji Jihadi, kufa Shahidi na kuvumilia tabu, machungu na mateso. Kwa hivyo inapasa Waislamu wafahamu kuwa kupigania kujitawala na kuwa na izza na kukataa kudunishwa na kudhalilishwa ni miongoni mwa nguzo za utamaduni wa kisiasa wa Uislamu, ambazo hazipasi kutetereshwa kwa namna yoyote ile katika mahusiano yao ya kimataifa. Na kwa maelezo hayo basi mpendwa msikilizaji, niseme pia kwamba, sehemu ya 48 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 49 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/