Jan 20, 2023 17:21 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Suala la maendeleo ya kisayansi na kuvuka mipaka ya elimu halipasi kusahaulika

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya taarifa na mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza katika mazungumzo na wawakilishi wa Baraza Kuu la Muungano wa Jumuiya za Wanachuo wa Kiislamu barani Ulaya kuwa suala la maendeleo ya kisayansi na kuvuka mipaka ya elimu halipasi kusahaulika.

Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo hivi karibuni alipoonana na kuzungumza na wawakilishi wa Baraza Kuu la Muungano wa Jumuiya za Wanachuo wa Kiislamu barani Ulaya na kuongeza kuwa, jumuiya za Kiislamu ni moja ya utajiri wa Jamhuri ya Kiislamu na zenye majukumu ya kipekee na kusisitiza kuwa, majukumu muhimu ya jumuiya za Kiislamu ni kuendeleza njia thabiti, kuacha athari katika mazingira yanayozizunguka na kubainisha ujumbe mpya wa Jamhuri ya Kiislamu.

Kitengo cha habari cha Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kimeripoti kuwa, Ayatullah Khamenei amemuenzi kwa kumkumbuka marhum Hujjatul Islam wal Muslimin Dakta Ejei mmoja wa waasisi wa Muungano wa Jumuiya za Kiislamu za Wanachuo barani Ulaya na kupongeza harakati za vijana wanachuo kuwa zenye mitazamo mipya na ya kimapinduzi. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, Jumuiya za Kiislamu zimeundwa kwa lengo la kuimarisha misingi yake ya kifikra na kiitikadi na pia kuathiri mazingira yanayozizunguka, hata hivyo jumuiya za kiislamu nje ya nchi zina kazi na majukumu mengine pia ambayo ni kuarifisha fikra za msingi na kuu za Jamhuri ya Kiislamu.   

Katika mazungumzo hayo, Ayatullah Khamenei amelitaja suala la elimu na maendeleo ya kisayansi kuwa ni jambo ambalo limekuwa likizungumziwa kwa pamoja hapa nchini katika miaka ya hivi karibuni, na akapongeza kufanyika  mkutano wa kisayansi katika Kongamano la hivi sasa la Jumuiya za Wanachuo wa Kiislamu barani Ulaya. Ameongeza kuwa, suala la maendeleo ya kisayansi na kuvuka mipaka ya kielimu halipasi kusahaulika na kudhaniwa kuwa, kutiliwa maanani nyuga za kidini na kimapinduzi kunasababisha kughafilika katika masuala ya maendeleo ya kisayansi. 

Chanjo za COVID nchini Iran

Wizara ya Afya ya Iran inasema kuwepo kwa chanjo kadhaa za COVID hufanya mapambano dhidi ya aina mpya za kirusi hicho kuwa rahisi.

Shahnam Arshi, naibu mkurugenzi wa idara ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza katika Wizara ya Afya ya Iran anasema wataalamu wa Iran wamefanikiwa kutengeneza chanjo kadhaa za Corona ambazo tayari zimeidhinishwa kutumika hapa nchini zikiwemo COVIRAN Barekat, Noora, PastoCovac, Fakhra, na SpikoGen.

Iran imetangaza kuwa iko tayari kukabiliana na wimbi jipya la nane la janga la corona kwani aina tatu mpya za corona zinazojulikana kama BQ1, XBB, na BA2 zimegunduliwa hivi karibuni duniani.

Naibu waziri wa afya Hossein Farshidi amesema Ndani ya mwezi mmoja hadi miwili ijayo, wimbi jipya la janga hilo litafikia kilele chake, kulingana na Shahnam Arshi, naibu mkurugenzi wa idara ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza katika Wizara ya Afya ya Iran anasema wimbi jipya sio kali kama mawimbi ya hapo awali, lakini watu wanashauriwa kupata dozi ya nyongeza na kuzingatia usafi wa kibinafsi na kijamii, haswa kuzuia mikusanyiko na kuvaa barakoa katika maeneo ambayo hayana uingizaji hewa mzuri.

Ameongeza kuwa, hivi sasa, vituo vyote vya kuingia nchini, haswa mipaka, viko chini ya udhibiti na ufuatiliaji.

Hivi majuzi, watafiti wa kimatibabu walitangaza kwamba kuna hatari ya mojawapo ya aina ya corona zinazotokana na Omicron duniani ambazo ni sugu kwa kingamwili zote za matibabu zinazopatikana, na matokeo yanaonyesha kwamba matibabu mapya lazima yatambuliwe ili kukabiliana na aina hii ndogo.

Kulingana na utafiti mpya katika taasisi moja ya Ujerumani, aina mpya ya Omicron, BQ.1.1, ni sugu kwa matibabu yote yaliyoidhinishwa ya kingamwili.

Huduma za Afya za Iran barani Afrika

Hivi karibuni Wizara ya Afya iliandaa mkutano wa mtandao, ikilenga kutafuta njia za kupanua huduma za afya za Iran barani Afrika.

Mohammad Hossein Nicknam, Naibu Waziri wa Afya wa Iran amesema kupanua  uhusiano na Afrika ni moja ya vipaumbele vya serikali ya awamu ya 13 ya Iran.

Maafisa kutoka wizara za afya na mambo ya nje, Shirika la Hilali Nyekundu, Shirika la Utoaji Damu, pamoja na mabalozi wa Iran katika nchi za Afrika, walihudhuria mkutano huo kwa njia ya mtandao.

Nicknam akizungumza katika kikao hicho amesema imeamuliwa kuwa kamati inayojumuisha sekta zinazohusika katika ushirikiano wa afya na Afrika iundwe ili kufuatilia suala hilo,

Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran hadi sasa imezindua vituo vya matibabu katika nchi saba za Afrika ambazo ni Ivory Coast, Sierra Leone, Ghana, Kongo, Kenya, Mali na Niger.

Waziri wa Afya wa Iran Daktari Bahram Einollahi alisema mwezi Aprili kwamba Iran hadi sasa imezipatia nchi 10 za Afrika chanjo za corona zilizotengenezwa nchini Iran.

Bidhaa za nano nchini Iran

Takwimu mpya zinaonyesha uzalishaji wa bidhaa na vifaa vilivyotengenezwa kwa msingi wa teknolojia ya nano nchini Iran uliongezeka mara sita katika kipindi cha miaka tisa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kamati ya Maendeleo ya Nanoteknolojia katika Ofisi ya Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia Sayansi, Teknolojia na Uchumi Unaotegemea Elimu, bidhaa  1,376 za nanoteknolojia zimetengenezwa nchini katika kipindi hicho.

Takwimu hizo zinaonyesha kampuni 271 zinazozalisha bidhaa za nanoteknolojia na kampuni 64 zinazotengeneza vifaa kwa kutumia teknolojia ya nano zilisajiliwa nchini Iran hadi mwisho wa 2022.

Kulingana na ripoti hiyo, katika mwaka uliopita wa kalenda ya Kiirani (uliomalizika Machi 2021), thamani ya mauzo ya nje ya Iran ya bidhaa za nanoteknolojia ilifikia dola milioni 62.

Dawa ya ukimwi

Na Shirika  linaloshughulika na uidhinishaji Dawa na Chakula nchini Marekani (FDA) limeidhinisha dawa inayodaiwa kuwa inaweza kutibu ugonjwa wa Ukimwi miongoni mwa watu wazima kwa kuitumia mara mbili kwa mwaka.

Wagonjwa wanapewa dawa hiyo mara mbili kwa mwaka kwa njia ya kudungwa au kumeza tembe. Dawa hiyo inagharimu dola 42,250 za Kimarekani kwa awamu hizo mbili.

Watumiaji pia wanahitajika kutoa dola 39,000 kila mwaka kugharamia “dozi za utunzaji”.

Wakati huu, dawa sawa na hiyo inayojulikana kama Cabenuva (cabotegravir and rilpivirine) kutoka kampuni ya dawa ya Uingereza ya GSK, inagharimu dola 40,000 hadi dola 50,000  kwa mwaka.

Mnamo 2021, dawa hiyo, inayopeanwa kwa kudungwa mgonjwa, ilikuwa ya kwanza kuidhinishwa na FDA kama tiba ya ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya HIV.

@@@

Na mustakabali wa teknolojia barani Afrika umetabiriwa kuwa wa kusisimua na wenye mwendo wa kasi. Kutokana na ongezeko la idadi ya watu na tabaka la kati linalokua, Afrika iko tayari kuwa mhusika mkuu katika soko la kimataifa la teknolojia.

Kulingana na jarida la Africa Business Insider, Mnamo 2023, tunatarajia kuona ukuaji na uvumbuzi zaidi katika sekta ya teknolojia barani Afrika. Kadiri bara hili linavyoendelea kukua na idadi ya watu kuongezeka, mahitaji ya teknolojia na huduma za kidijitali yataongezeka pia.

Hali hii inatoa fursa kubwa kwa wajasiriamali wa Kiafrika na kampuni za kimataifa za teknolojia zinazotaka kuingia sokoni.
Hapa kuna nyanyja tano za teknolojia zinazotarajiwa kustawi zaidi barani Afrika mnamo 2023.

Kwanza bara hilo linatabiriwa kushuhudia  kuongezeka kwa matumizi ya akili ya mashine au artificial intelligence. Pili ni kuendelea kukua kwa sekta ya biashara ya mtandaoni. Aidha Afrika mwaka 2023 inajarajiwa kushuhudia upanuzi wa mtandao wa intaneti ya kasi ya juu na mitandao ya simu. Hali kadhalika bara la Afrika linatabiriwa kuwa na ustawi mkubwa katika sekta ya suluhisho mpya za malipo ya kidijitali na ubunifu wa teknolojia za kifedha. Kuongezeka kwa matumizi ya vyanzo vya nishati mbadala, kama vile jua na upepo ni sekta nyigine ya teknolojia ambayo imetabiriwa kustawi kwa kasi barani Afrika mwaka huu.

@@@

Naam la ziada sina kutoka makala hii ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa umeweza kunufaika. Basi hadi wakati mwingine panapo majaliwa yake Mola, kwaherini.

 

Tags