Mar 12, 2023 07:46 UTC
  • Hakika ya Uwahabi 14

Yale tuliyoyajadili katika vipindi vilivyopita kimsingi yalihusiana na mambo tunayoyajua kuhusiana na pote linalojulikana kama Mawahabi kwa msingi wa nyaraka za kihistoria, fikra na itikadi zao. Pote hili pia lina maulama na viongozi ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakitoa fatwa kuhusiana na masuala tofauti katika ulimwengu wa Kiislamu. Leo tunakusudia kujadili baadhi yao na fatwa walizotoa katika uwanja huo.

Tuaanza kwa jina la Mwenyezi Mungu ambaye amewatenganisha wajuzi na majahili, Mungu ambaye ameteremsha Aya zake kwa ajili ya kuzingatiwa na wale wanaotumia vyema akili zao.

Yale tuliyoyajadili katika vipindi vilivyopita kimsingi yalihusiana na mambo tunayoyajua kuhusiana na pote linalojulikana kama Mawahabi kwa msingi wa nyaraka za kihistoria, fikra na itikadi zao. Pote hili pia lina maulama na viongozi ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakitoa fatwa kuhusiana na masuala tofauti katika ulimwengu wa Kiislamu. Leo tunakusudia kujadili baadhi yao na fatwa walizotoa katika uwanja huo. Karibuni.

**************

Miaka 20 kabla ya kuasisiwa utawala wa Mawahabi huko Saudi Arabia yaani mwaka 1330 Hijiria, Abd al-Aziz bin Baz alizaliwa mjini Riyadh, ambao ni mji mkuu wa hivi sasa wa nchi hiyo inayoongozwa kiukoo. Alifundishwa masomo ya awali ya Uislamu na walimuu wa Kiwahabi huko Najd na alipoteza uwezo wake wa kuona kutokana na maradhi aliyopata akiwa na umri wa miaka sita. Licha ya ugonjwa huo lakini aliendelea kujifunza masomo hayo hadi alipojulikana na kuwa mashuhuri mbele ya Mawahabi ambao walimfanya kuwa mufti wao mkuu ndani na nje ya Saudia. Abd al-Aziz bin Baz alifanywa kuwa marejeo ya maualama na wanazuoni wengine wa Saudia na kila walipokabiliwa na tatizo lolote la kidini na kisheria walikuwa wakimrejea yeye kwa ajili ya kutatuliwa tatizo hilo. Alijulikana mbele ya Mawahabi kama mufti mkuu.

Abd al-Aziz bin Baz

Abd al-Aziz bin Baz ni miongoni mwa maulama wa Kiwahabi waliotoa fatwa ya kuwakufurisha Mashia. Kwa mtazamo wake, na bila shaka kwa mtazamo wa mamufti wengi wa Kiwahabi, Mashia wamekumbwa na shirki kubwa na kutoka kwenye Uislamu kutokana na kutawasali na Maimamu wao watoharifu (as) na kuwaomba shufaa. Kutokana na fatwa hiyo ya kijahili, ulimwengu umeshuhudia maauji makubwa na ya kutisha yakifanyika dhidi ya wafuasi wa madhehebu ya Shia katika pembe mbalimbali za dunia, madhehebu ambayo ni ya Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw).

Vipimo vinavyotumiwa na Mawahabi kwa ajili ya kuwatoa Waislamu halisi kwenye dini ni vingi. Wao wanakuchukulia kumswalia na kumtumia salamu Mtume (saw) pamoja na kumuandalia maadhimisho ya kuzaliwa kwake na vile vile viongozi wengine mashuhuri wa dini kuwa ni bida' na kuvichukulia vitendo hivyo kuwa ni alama ya shirki. Mbali na hayo itikadi potovu ya Mawahabi kuwa Mungu ana mwili imewapelekea Mawahabi kuwakufurisha Waislamu wengine wasioamini hivyo. Kwa msingi huo hawawakufurishi Mashia tu bali mamufti wa Kiwahabi na wafuasi wao wanawachukulia Masuni wote wanaopinga dhana ya kuwa Mwenyezi Mungu ana kiwiliwili, wanaomswalia na kumtumia salamu Mtume (saw) na pia kushirikia katika sherehe za maulidi yake kuwa ni mushirikina wanaopaswa kukufurishwa na kumwagwa damu yao.

Bado kuna sababu nyingine kadhaa zinazotumiwa na Mawahabi kuwakufurisha Waislamu. Mufti Mkuu wa Mawahabi, Abd al-Aziz bin Baz, ana fatwa ya kushangaza mno ambayo inakufurisha na kuwajibisha kuuawa maulama na wasomi wa kidini bila kujali madhehebu wala dini zao. Kwa mtazamo wake, sayari ya ardhi ni thabiti bali ni jua ndilo linaizunguka na kila mtu anayeamini kinyume na hivyo ni kafiri ambaye anapaswa kuuawa. Fatwa hii inawakumbusha hata wale walio na kumbukumbu ndogo tu ya historia, fikra finyu na za mgando zilizotawala ulimwengu katika zama za karne za kati. Abd al-Aziz bin Baz hatimaye aliaga dunia mwaka 1999.

************

Baada ya kuaga dunia Ibn Baz, Muwahabi mwingine kwa jila Abdulaziz Aal-Sheikh, alifanywa kuwa mufti mkuu wa Mawahabi wa Saudi Arabia. Aal-Sheikh ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Muhammad bin Abdul Wahhab, mwanzilishi wa Uwahabi, alizaliwa mwaka 1943 na kufikia sasa ametoa fatwa nyingi za kushangaza na zenye kuibua utata mkubwa katika limwengu wa Kiislamu.

Abdulaziz Aal Sheikh

Alipoulizwa katika kipindi kimoja kilichokuwa kikipeperushwa hewani moja kwa moja kuhusiana na mapambano ya Imam Hussein (as), Imam wa tatu wa Mashia, na ambaye ni mjuu mpendwa wa Mtume Mtukufu (saw) ambaye aliuawa kinyama katika jangwa la Karbalaa nchini Iraq ya leo kwa amri ya Yazid bin Muawiyya, Aal Sheikh aliharamisha mapambano hayo na kusema kuwa hakupenda kuulizwa suala hilo. Alidai kuwa masuala hayo yalihusiana na mambo yaliyotokea maelfu ya miaka iliyopita na kwamba muda wa kuyajadili pia ulikuwa umepitwa na wakati. Pamoja na hayo lakini mufti huyo wa Kiwahabi anasema kuwa masuala yote ya zama hizi yanapasa kutekelezwa kwa msingi wa suna zilizotekelezwa malefu ya miaka iliyopita. Kwa msingi huo, anaamini kuwa ni haramu kutoa zaka ya fitri katika sura ya pesa taslimu na kwamba inapasa kutolewa katika mfumo uliofuatwa mwanzoni mwa kudhihiri Uislamu yaani, mchele, tende na shahiri.

Kama wanavyoaamini wale wanaofuata fikra ya kuwa wanadamu hawana hiari yoyote katika matendo na machaguo yao bali wanalazimika kufanya wanayoyafanya kutokana na amri ya Mungu, Aal Sheikh anaamini kuwa iwapo wanasiasa fasidi na wasiofaa watapata fursa ya kuketi kwenye viti vya utawala, hakuna mtu yeyote aliye na haki ya kuwauliza au kuhoji walivyofika katika nafasi hizo bali ni Mwenyezi Mungu tu ndiye aliye na haki ya kufanya hivyo na ikilazimu awauzulu mwenyewe. Vile vile kwa mtazamo wake, kutokana na kuwa hakukuwepo na maandamano katika zama za Mtume, kufanya maandamano katika zama hizi ni bida' na uzushi kwenye dini. Ni kwa msingi huo ndipo akalaani vikali kufanyika maandamano ya aina yoyote ile dhidi ya watawala wa Aal Saud nchini Saudi Arabia na hata kuamini kuwa ni haramu kwa Waislamu kufanya maandamano yoyote duniani kwa ajili ya kulaani na kukemea hatua zinazochukuliwa na majarida na shakhsia wa nchi za Magharibi katika kudhalilisha na kumvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw).

Fatwa nyingine ya Abdulaziz Aal Sheikh iliyoibua mijadala na utata mwingi duniani, ni amri yake ya kutaka kubomolewa makanisa yote nchini Saudi Arabia. Fatua hiyo ilikabiliwa na malalamiko pamoja na ukosoaji mkubwa wa maaskofu wa Kikristo nchini Ujerumani, Austria na Russia na kufuatiwa na maandamano ya Wakristo wanaoishi Saudia.

***********

Mbali na mamumfi wakuu hao wa Saudi Arabia, mamufti wengine wa Kiwahabi pia wana fatwa za kushangaza ambazo zinamsikitisha kila mwanadamu aliye na akili salama.

Kwa mfano, mufti mmoja wa Kiwahabi aliyejiita Allama Abul Baraa anasema kuwa ni haramu kwa mwanamke kuwasha nyumbani kiyoyozi bila ya mumewe kuwepo nyumbani hapo na kusisitiza kwamba: "Mwanamke anapowasha kiyoyozi hali ya kuwa mumewe hayuko nyumbani, huenda jirani akang'amua kuwa yuko pake yake nyumbani na hivyo kufanya zina na ufuska." Hii ni katika hali ambayo mufti mwingine wa Kiwahabi kwa jila la Abdul Bari az-Zamzami, ambaye ni mkuu wa jumuiya ya utafiti wa kifikhi ya nchini Morocco anatoa fatwa inayosema kuwa mabinti ambao hawajafanikiwa kuolewa, wanapasa kuvalia mavazi yanayoacha miili yao nusu-uchi ili kwa njia hiyo waweze kuwavutia vijana upande wao.

Abdul Bari az-Zamzami

Jassim as-Saudi, mufti mashuhuri wa Kiwahabi wa Bahrain anasema kama tunavyomnukuu katika fatwa ya kushangaza: "Ikiwa lengo ni kutatua matatizo ya bajeti na kuimarisha uchumi wa Bahrain, inajuzu kuuza pombe na kufanya biashara ya ngono kadiri ya mahitaji"! Katika upande wa pili, mmoja wa wanachama wa Baraza la Fatwa la Kuwait anasema: " Hata zafarani ni aina ya dawa za kulenya hivyo inajuzu kuzitumia."

Katika mfano mwingine, tunaweza kusema kuwa katika hali ambayo baadhi ya mamufti wa Kiwahabi wanadai kuwa baiskeli ni chombo cha shetani na ni haramu kukipanda, Dea' Abdullah, Imam wa jamaa wa msikiti wa Nur al-Islah mjini Washington Marekani huku akikiri kuwahi kuwa na mahusiano ya kingono na wanaume wanne wanaojihusisha na ufuska wa uhusiano wa watu wa jinsia moja, amedai kuwa Uislamu unaruhusu vitendo kama hivyo. Amesema ameelekeza juhudi zake zote katika kile amekitaja kuwa kuuarifisha Uislamu kwa mtazamo wa kisasa na kuufanya uendane na mambo ya kisasa. Amedai kuwa kuhalalishwa uhusiano wa aina hiyo ni moja ya alama za maendeleo ya Uislamu!

Dea' Abdullah

Pamoja na mambo yote tuliyotangulia kuyasema, ni vyema tufahamu kwamba miongoni mwa mamufti wa Kiwahabi, wapo wale ambao wametambua kwa kiasi fulani, baadhi ya makosa waliyoyafanya wao wenyewe na ya waliowatangulia, na kuyakiri hadharani. Adil bin Salim al-Kalbani (Adil al-Kalbani), imamu wa zamani wa Masjidul Haram na mmoja wa mamufti mashuhuri wa kitakfiri, alisema katika kipindi kimoja cha televisheni, baada ya kupita miaka kumi ya kuwakufurisha Mashia, kwamba hawawachukulii tena Mashia kuwa makafiri. Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya MBC ya Saudi Arabia, alisema: "Mtu yeyote anayesema La Ilaha illa Allah na akasimama kuelekea Qibla chetu huyo ni Muislamu."

Adil bin Salim al-Kalbani

Essam al-Emad ni Muwahabi mwingine wa zamani aliyejirudi na kukosoa itikadi na fikra za Mawahabi. Alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Abd al-Aziz bin Baz, ambaye, chini ya ushawishi wa Muhammad bin Abd al-Wahhab, alikuwa adui mkubwa wa Mashia na hasa Imam Ali (as). Baada ya kusoma vitabu vya Seyyid Qutb, alitambua makosa ya Uwahabi kuhusu Imam huyo mtukufu (as), na hatimaye akajiunga na madhehebu ya Shia. Essam al-Emad ameandika vitabu kadhaa dhidi ya Uwahabi, kimojawapo kikiwa ni Zilzal. Maudhui ya kitabu hiki ni mijadala yake na mufti mmoja mashuhuri wa Kiwahabi anayeitwa Uthman al-Khamis. Kitabu hicho ambacho kinaonyesha udhaifu wa fikra za Mawahabi na itikadi zao, kimewavutia vijana wengi wa Kiarabu na kuwaongoza kwenye njia sahihi ya Uislamu.

Essam al-Emad
kitabu cha Zilzal kilichoandikwa na Essam al-Emad

Na kufikia hapo ndio tunahitimisha makala yetu hii kwa leo. Basi hadi wakati mwingine panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.