Apr 30, 2023 18:39 UTC
  • Iran yafungua kituo cha kisasa cha kutibu saratani, Kenya yazindua satalaiti

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya taarifa katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Iran yafungua kituo cha kisasa kabisa cha matibabu ya saratani Asia Magharibi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raisi hivi karibuni alizindua kituo cha kisasa kabisa cha matibabu ya saratani mjini Tehran na akasema serikali yake inalenga kuboresha maisha ya wananchi kuondoa udhaifu uliokuwepo.

Rais Raisi alifungua rasmi Kituo cha Kuzuia na Kutibu Saratani cha Barekat ambacho ni mojawapo ya vituo vya kisasa kabisa katika uga wa kuzuia na kutibu saratani katika eneo la Asia Magharibi.

Katika hotuba yake ya ufunguzu Raisi alisema kufunguliwa kwa kituo hicho ni "hatua muhimu katika mwelekeo wa kuondoa udhaifu nchini na kuhakikisha kuwa kuna vifaa vya hali ya juu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wananchi."

Kituo cha Kuzuia na Kutibu Saratani cha Barekat kimejengwa na Makao Makuu ya Utekelezaji wa Agizo la Imam Khomeini (MA). Kituo hicho cha kisasa kabisa kinatoa huduma zote zinazohusiana na uchunguzi, utambuzi na matibabu ya aina zote za saratani.

Raisi amepongeza juhudi za wataalamu na taasisi za afya kupunguza gharama huku pia akipongeza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kituo hicho kipya cha afya.

Rais amesema kituo hicho cha matibabu kinalenga kuondoa upungufu uliokuwepo na kutoa huduma za matibabu zenye ubora wa hali ya juu kwa gharama nafuu zaidi kwa wananchi huku akitoa wito wa kujengwa kwa vituo vya aina hiyo katika maeneo mengine nchini ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi.

Uzinduzi huo ulikuja wiki moja baada ya Rais Raisi  kufungua Hospitali ya Mahdi mjini Tehran ambayo imetajwa hospitali kubwa zaidi katika eneo la Asia Magharibi. Hospitali ya Mahdi ni mradi mkubwa zaidi wa matibabu nchini tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979, kwani  ina takriban vitanda 1,000 pamoja na vifaa vya matibabu vya hali ya juu ambavyo vitahudumia wagonjwa wa Iran na wa kigeni.

Iran imepata maendeleo makubwa katika nyanja ya tiba kwa miaka ya hivi karibuni, hususan katika maeneo ya utengenezaji wa dawa na vifaa vya matibabu pamoja na kutoa mafunzo kwa madaktari na wapasuaji katika vituo vya matibabu vya kisasa kote nchini.

 

@@@

Kenya imerusha satelaiti yake ya kwanza ya uchunguzi katika anga za mbali siku ya Jumamosi na hivyo imejiunga na nchi chache Afrika ambazo zimesahrusha satelaiti angani.

Satelaiti hiyo imerushiwa katika anga za mbali kwa kutumia roketi ya SpaceX Falcon 9 katika kituo cha kurushia satalaiti cha Vandenberg huko California nchini Marekani.

Satelaiti hiyo iliyotengenezwa na wahandisi tisa wa Kenya, itakusanya data za kilimo na mazingira, zikiwemo kuhusu mafuriko, ukame na moto misituni, ambazo mamlaka inapanga kuzitumia kudhibiti majanga na kukabiliana na uhaba wa chakula.

Roketi ya Falcon 9 iliyokuwa imebeba satelaiti ya Taifa-1, ilipaa saa 0648 GMT kutoka Vandenberg California, baada ya kuahirishwa mara tatu kutokana na hali mbaya ya hewa.

Shirika la Anga za Juu la Kenya limesema satelaiti hiyo imeundwa ushirikiano na kampuni ya anga ya Bulgaria ya Endurosat kwa gharama ya shilingi milioni 50 za Kenya ($372,000) kwa miaka miwili.

Shirika hilo linasema litafanya kazi kwa miaka mitano. Taarifa ya pamoja ya Wizara ya Ulinzi na Shirika la Anga za Juu la Kenya imesema satelaiti hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa "uchumi wa anga za juu unaochipua" nchini Kenya.

Satelaiti hiyo ya uchunguzi "imeundwa kikamilifu" na wahandisi wa Kenya na itatumika kutoa data kuhusu kilimo na usalama wa chakula, miongoni mwa sekta zingine, ilisema taarifa hiyo.

Kenya inakabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa baada ya misimu mitano ya kukosa mvua, na hivyo satelaiti hiyo itaweza kusaidia kukabiliana na majanga kama hayo.

Uzinduzi huo wa satelaiti utaongeza msukumo kwa mataifa ya Afrika kwa uvumbuzi wa kisayansi na maendeleo ya programu za anga.

Misri ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kutuma satelaiti angani mwaka 1998. Mnamo 2018, Kenya ilizindua satalaiti ya nano ambayo ilikuwa satalaiti yake ya kwanza.

Kufikia 2022, angalau nchi 13 za Kiafrika zilikuwa zimetengeneza satelaiti 48. Hayo ni kwa mujibu wa Kamapuni  Space in Africa yenye makao yake makuu nchini Nigeria inayofuatilia programu za anga za juu za Afrika. Nchi hizo ni pamoja na Ethiopia, Algeria, Angola, Afrika Kusini, Sudan, Rwanda, Morocco, Tunisia, Mauritius na Ghana.

@@@

Rwanda imetangaza kuwa, inatumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani katika kupambana na ugonjwa wa malaria.

Kwa utaratibu huo Rwanda inakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kkutumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani katika juhudi za kupambana na malaria.

Ndege hizo zinanyunyiza dawa za kuua mbu katika maeneo ya mabonde,kwa mujibu wa Taasisi ya Taifa ya Afya (RBC).

Tangu kuanzishwa kwa matumizi ya teknolojia hiyo mwaka 2021, ugonjwa wa malaria ulipungua kwa zaidi ya asilimia 90% katika maeneo yanayofanyiwa majaribio.

Bwana Kamali Paul, ambaye ni msimamizi wa ugonjwa wa malaria katika kampuni ya Charis, anasema wanatumia ndege hizo kwa sababu teknolojia yake inaruhusu kunyunyiza dawa katika eneo kubwa sana na kwa muda mfupi

Kampeini ya kunyunyiza dawa za kukabiliana na mbu imeleta hali ya afueni miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo waliozungumza na duru za habari waliokuwa wamezongwa na malaria.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa malaria, bado inatambuliwa kuwa tishio kwa bara la Afrika, haswa kutokana na kuongezeka usugu wa maradhi hayo kwa matibabu, licha ya chanjo zinazotolewa za kukabiliana na malaria.

Malaria husababishwa na vimelea na huambukizwa kwa binadamu kupitia mbu jike aina ya Anopheles. Ingawa ugonjwa huo unaweza kuzuilika na kutibika, unaweza kusababisha kifo usipotibiwa.

Takwimu zinaonyesha kuwa, zaidi ya nusu ya vifo vyote vya malaria duniani kote vinatokea katika nchi nne za Afrika ambazo ni: Nigeria (31.3%), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (12.6%), Tanzania (4.1%) na Niger (3.9%).

 

@@@

Dawa bandia, feki au za kughushi ni tatizo kubwa katika nchi nyingi za Afrika. Utafiti unaonyesha kuwa nchi nyingi zinazoendelea zina kiwango kikubwa cha dawa zisizo na viwango.

Kwa mfano, hadi asilimia 88.4% ya dawa za malaria katika baadhi ya masoko ya Afrika zimeripotiwa kuwa bandia. Kutumia dawa zisizo na ufanisi husababisha vifo kati ya 64,000 na 158,000 vinavyohusishwa na ugonjwa wa malaria kila mwaka katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kuwapa watu dawa ambayo haitafanya kazi mwilini au haijatengenezwa vizuri kusaidia ugonjwa husika ni hatari. Zaidi ya watoto 250,000 duniani kote hufa kutokana na dawa feki kila mwaka. Katika mwaka uliopita pekee zaidi ya watoto 300 walikufa baada ya kutumia dawa feki za kikohozi au dawa za maumivu.

Juhudi zinaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa serikali kuhusu dawa bandia.

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, hadi asilimia 50 ya dawa katika eneo la Afrika magharibi hazikidhi vigezo vinavyostahili au ni bandia. Hayo yamo katika ripoti maalumu ya Umoja wa Mataifa kuhusu biashara haramu ya bidhaa za matibabu.

Aidha kwa mujibuu wa Umoja wa Mataifa ni kuwa, kote eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, hadi dola milioni 44.7 zinatumiwa kila mwaka kutibu watu waliotumia dawa bandia za malaria au zisizokidhi vigezo na viwango vinavyostahili.

Mbali na hatari ya bidhaa bandia na dawa zilizotengenezwa vibaya, ambazo hazifanyi kazi kama inavyotakiwa na mbaya zaidi kusababisha maambukizi ya magonjwa hatari, ripoti zinaonya pia kuhusu dawa halali kutumiwa kwa njia zisizoidhinishwa na wataalamu.

Hivi karibuni pia, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, hadi asilimia 50 ya dawa katika eneo la Afrika magharibi hazikidhi vigezo vinavyostahili au ni bandia. Hayo yamo katika ripoti maalumu ya Umoja wa Mataifa kuhusu biashara haramu ya bidhaa za matibabu.

Inaelezwa kuwa, biashara hiyo inaweza kusababisha dawa za kuua wadudu kutofanya kazi au maambukizi ya magonjwa hatari, huku pia ikidhoofisha kikamilifu uaminifu katika mifumo ya afya na tiba.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu madawa ya kulevya na uhalifu (UNODC) imeeleza kuwa, kati ya Januari 2017 na Disemba 2021, takribani tani 605 ya bidhaa za matibabu zilikamatwa katikka eneo la Afrika magharibi katika operesheni za kimataifa, ingawa kuna kasoro katika kuripoti kuhusu biashara hiyo haramu na huenda idadi ya dawa hizo ikiwa juu zaidi ya kiwango hiki kilichosajiliwa.

 

@@@

Naam Wapenzi wasikilizaji na hadi hapo tunafika mwisho wa makala yetu ya sayansi na teknolojia kwa leo. Ni matumaini yangu kuwa mumeweza kunufaika.

 

 

Tags