Filamu ya "Muhammad Rasulullah" yaoneshwa nchini Uturuki
Tarehe 28 mwezi wa Oktoba filamu ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu ambayo imetengenezwa nchini Iran ilionyeshwa katika kumbi 300 za sinema nchini Uturuki baada ya kutarjumiwa kwa lugha ya Kituruki na kuambatana na maandishi ya lugha ya Kiingereza.
Tukio hilo limekaribishwa sana nchini Uturuki na idadi kubwa ya watu imejitokeza kutazama filamu hiyo. Kanali nyingi za televisheni za Uturuki zimeripoti tukio hilo la kuonyeshwa filamu hiyo ya Kiirani kwa mara ya kwanza nchini humo. Jambo la kuvutia zaidi ni kwamba, filamu hiyo iliyotengenezwa na mkurugenzi na mtayarishaji wa filamu wa Iran, Majid Majidi, imeshika nafasi ya juu zaidi na kuzishinda filamu mbili za Kimarekani ambazo pia zinazoneshwa kwa mara ya kwanza nchini Uturuki.
Muswada wa filamu hiyo, ikiwa ni pamoja na maelekezo ya uigizaji wake (screenplay) umeandikwa na Majid Majidi na Kambuzia Partovi na utengenezaji wake umechukua kipindi cha miaka saba. Awamu ya awali na kabla ya utengenezaji wa filamu hiyo ambayo ilijikita zaidi katika uchunguzi na utafiti, ilichukua kipindi cha miaka 3. Filamu ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu imetengenezwa katika kijiji cha filamu cha Mtume Adhimu kilichoko umbali wa kilomita 55 kutoka katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran. Katika kijiji hicho cha filamu kumetengenezwa mifano ya miji ya Makka na Madina ya kipindi cha miaka 1400 iliyopita na sifa za miji hiyo mitakatifu ya kipindi hicho. Upigaji picha na uchukuaji wa filamu hiyo umefanywa na mtaliano Vittorio Storaro, na muziki wake umetengenezwa na I.R Rahman ambao wote wawili ni wasanii maarufu duniani na washindi wa tuzo ya Oscar. Miongoni mwa wachezaji katika filamu hiyo ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu ni Ali Ridha Shujaa Noury, Mahdi Pakdel, Sara Bayat na Mina Sadat.
Filamu ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu ni filamu ya kihistoria inayosimulia maisha ya Mtume Muhammad (saw) katika kipindi cha karne ya sita Miladia. Filamu hiyo inaanza kwa kueleza sifa za mazingira ya kijamii ya zama za kuzaliwa kwa mtukufu huyo na kumalizika wakati Mtume alipokuwa na umri wa miaka 12. Imepangwa kuwa, filamu hiyo itakuwa na sehemu tatu tofauti zinazohadithia vipengee tofauti vya maisha ya Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo sehemu nyingine mbili za filamu hiyo zitatengenezwa baadaye.
تصاویری از فیلم محمد رسول الله
Mkurugenzi na mtayarishaji wa filamu hiyo, Majid Majidi, anasema kuwa, kabla na baada ya utengenezaji wake alishauriana na maulamaa na wanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu mbili za Shia na Suni na kwamba maoni yao yamekuwa ya kuridhisha na ukosoaji wao mwingi ulikuwa wenye faida na manufaa. Majidi anasema, anatarajia kwamba hata wale ambao hawakuwa na mtazamo mzuri kuhusu filamu hiyo wataitazama na kumpa nasaha na miongozo yao. Amesema anaheshimu maoni na ukosoaji huo na kwamba, atautumia na kuutilia maanani katika kazi zake.
Majid Majidi anasema kuwa: Kuna filamu chache sana zinazosimulia maisha ya Mtume Muhammad (saw) na kwamba hiyo peke yake ni miongoni mwa sababu zinazozusha mjadala mkubwa kuhusu utengenezaji wa filamu hiyo. Mtaalamu huyo wa filamu wa Iran anasema: Baada ya kuoneshwa kwa mara ya kwanza filamu ya The Message (الرسالة) iliyotengenezwa na Moustapha Akkad miaka 40 iliyopita, hadi sasa hakujaonyeshwa filamu nyingine kama hiyo. Ni jambo la kawaida kwamba, baada ya kipindi hicho kirefu, kutakuwepo ukosoaji na maoni tofauti kuhusu filamu yoyote inayohusiana na maisha ya Mtume Muhammad (saw). Mkurugenzi huyo wa filamu wa Iran anasisitiza kuwa anakaribisha ukosoaji wa wataalamu na wasomi wa Kiislamu na kwamba utatajirisha zaidi na kuboresha kazi ya kumuarifisha Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa walimwengu kupitia tasnia ya filamu. Anaendelea kusema kuwa, sanaa ni wenzo mwafaka na wenye taathira kubwa kwa ajili ya kuarifisha sura sahihi na nzuri ya Uislamu na kujibu madai ya wale wanaoidhihirisha dini hiyo kwa sura bandia na isiyo ya kweli.
Kama tulivyosema mwanzoni kwa kipindi hiki, filamu ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu imeonyeshwa kwa mara ya kwanza nchini Uturuki katika ukumbi wa filamu uliohudhuriwa na waandishi habari, wacheza filamu, watayarishaji na waandishi wa miswada ya filamu wa Uturuki na wawakilishi wa ofisi ya mwambata wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Istanbul. Matukio ya filamu hiyo yamewaathiri sana hadhirina na wengi wao walishindwa kuzuia machozi yao. Mmoja kati ya watazamaji wake amesema anatarajia filamu ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu itaendelea kuoneshwa kwa kipindi cha mwaka mzima nchini Uturuki ili idadi kubwa ya watu iweze kufaidika na yaliyomo. Anaendelea kusema kuwa yeye kama Mwislamu ameathirika sana na matukio ya filamu hiyo na kwamba ujumbe muhimu zaidi aliopata baada ya kuitazama ni upole, huruma, ukarimu na usamehevu wa Mtume Muhammad (saw).
Aghlabu ya wakosoaji na waandishi wa masuala ya filamu waliohudhuria tukio la kuoneshwa filamu ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu nchini Uturuki wanasema, kuna uwezekano ikavunja rekodi ya uuzaji mkubwa zaidi na kutazamwa na idadi kubwa ya watu katika kumbi za sinema za nchi hiyo.
Katika tahariri yake ndefu, gazeti la Türkiye limepongeza filamu hiyo na kuandika kwamba: Katika filamu yake ya kuvutia, Majid Majidi ameonyesha kwa mara ya kwanza picha ya maisha ya utotoni ya Mtume Muhammad (saw)... Kwa kutumia ufundi na uhodari mkubwa, Majidi amefanikiwa kusimulia maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa njia ya filamu na kuwasimulia watazamaji wake vipengee vya maisha ya mtukufu huyo ambavyo hadi sasa hawajawahi kuvishuhudia. Tahariri ya gazeti la Türkiye inaendela kusema: Filamu hiyo imeonesha kwa ufundi wa hali ya juu baadhi ya viungo cha mwili wa Mtume (saw) bila ya kudhihirisha sura yake. Tahariri hiyo inamalizia kwa kuandika kuwa: "Japokuwa filamu ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu haikuwashirikisha wachezaji filamu magwiji na maarufu sana, lakini kwa hakika imefanikiwa sana kudhihirisha sifa za kipekee, aali na maadili ya Mtume wetu..".
Magazeti ya Sabah na Karar yameakisi tukio la kuonyeshwa filamu hiyo katika kurasa zao za mbele. Mwandishi wa gazeti la Sabah anasema katika kichwa cha habari kilichobeba anwani ya: "Filamu ya Mtume Muhammad (saw) katika Kumbi la Sinema" kwamba: "Nimeshindwa kuzuia machozi yangu katika kipindi chote cha masaa matatu ya kutazama filamu hiyo". Mwandishi wa gazeti hilo anaendelea kuandika kuwa: Filamu hiyo imechunguzwa kikamilifu na Jumuiya ya Masuala ya Dini ya Uturuki kabla ya kuoneshwa kwa mara ya kwanza nchini humo na kusema: Filamu hiyo haioneshi sura ya Mtume Muhammad na kwamba pale mtukufu huyo alipoulizwa swali basi haikuletwa sauti yake bali maneno yake yalinukuliwa au kuoneshwa kwa maandishi.
Mkosoaji wa filamu wa Uturuki, Ihsan Qabil ambaye alikuwa miongoni mwa waliotazama filamu hiyo anasema: Filamu ya Iran ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu ndiyo athari na kazi muhimu zaidi uliyotengenezwa kuarifisha shakhsia ya Mtume wa Muhammad (saw) baada ya ile ya The Message iliyotengenezwa na Moustapha Akkad katika miaka ya 70. Ihsan Qabil pia amepongeza muziki wa filamu hiyo na kusema, ni mchanganyiko wa muziki wa Kiajemi na Kimagharibi. Muziki wa filamu hiyo umetengenezwa na msanii wa India, I.R Rahman ambaye alisilimu na kuwa Mwislamu muda mfupi kabla ya kutayarisha muziki wa filamu hiyo.
Qabil anamalizia kwa kuandika kuwa: Mkurugenzi wa filamu ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu, Majid Majidi ni miongoni mwa watengeneza filamu wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu na kwamba filamu yake ni kazi yenye thamani kubwa.
Kwa upande wake mwandishi wa kanali ya televisheni ya Quds Press ya Uturuki, Ramadhan Bursa anasema ukosoaji mwingi uliotolewa kuhusu filamu hiyo umetawaliwa zaidi na mitazamo na jazba za kisiasa. Bursa anaendelea kuandika kuwa: Majid Majidi alichukua uamuzi wa kutengeneza filamu ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu baada ya kitendo cha kuoneshwa katuni na vibonzo vya kumdhalilisha Mtume (SAW) katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kuzusha hasira kubwa miongoni mwa Waislamu. Wakati huo ndipo Majidi alipoelewa kwamba, Mtume Muhammad hajaeleweka ipasavyo katika ulimwengu wa Magharibi na kutangaza kuwa, atatengeneza filamu hiyo kwa ajili ya kumuarifisha.
Ramadhani Bursa anasema: Kwa mtazamo wake yeye ukosoaji na yanayosemwa katika nchi za Saudi Arabia na Misri kuhusu filamu hiyo hayahusiani kabisa na muhtawa na yaliyomo. Anasisitiza kuwa, ukosoaji huo umetekwa zaidi na uhusiano wa kisiasa wa serikali za nchi hizo na Iran na kwamba, mivutano ya kisiasa ya pande hizo mbili imewafanya wakosoaji watekwe na jazba za kisiasa na kuihukumu filamu ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kutumia mitazamo na jazba hizo.
Licha ya mitazamo hiyo inayotawaliwa na jazba za kisiasa, watu wengi nchini Uturuki wamevutiwa sana na na filamu hiyo na waandaaji wamelazimika sasa kuionesha katika kumbi 900 za sinema badala ya 300 kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.
Filamu ya Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu iilianza kuoneshwa pia nchini Russia Ijumaa ya tarehe 18 Novemba na mipango inafanyika ya kuoneshwa katika nchi za Mashariki ya Kati, India na barani Ulaya.