Kashfa kubwa zaidi ya kimaadili yaitikisa tena Hollywood
Sekta ya filamu ya Hollywood huko Marekani imetengeneza filamu nyingi zinazozungumzia maudhui ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono na vilevile kashfa za ufuska na kadhalika.
Hata hivyo kwa siku kadhaa sasa Hollywood imekuwa ikisimulia kisa cha kweli, na si ndoto na njozi za filamu, kuhusu mienendo ya utovu wa maadili na ufuska wa baadhi ya vigogo wake. Katika siku hizi vyombo vya habari vimekuwa vikisimulia hakika ya kutisha mno iliyowahusu wagonjwa na watu wenye maradhi hatari ambao si wa tabaka la chini na la watu wenye mashaka wasio na mlingano wa kinafsi, bali watu ambao kidhahiri wana majina makubwa na matajiri katika sekta ya kutengeneza filamu ya Marekani.
Alkhamisi ya tarehe 5 mwezi huu wa Oktoba waandishi habari wawili wa gazeti la New York Times walichapisha matokeo ya uchunguzi wao kuhusu moja kati ya vinara wa sekta ya filamu ya Hollywood, Harvey Weinstein ambaye ni miongoni mwa waasisi wa kampuni ya inayojulikana kwa kuzalisha na kusambaza filamu na michezo ya televisheni ya Marekani ya Miramax na mtayarishaji filamu muhimu zaidi katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita katika sekta ya filamu ya Marekani na dunia. Ripoti na uchunguzi huo wa New York Times imevutia sana mazingatio ya mashabiki wa filamu kote duniani na hilo limetajwa kuwa tukio muhimu zaidi la Hollywood katika siku hizi.

Waandishi hao wa habari wamechunguza kwa mapana na marefu historia ya mtayarishaji huyo wa filamu na mafaili yake ya zamani na ya sasa katika mahakama za nchi hiyo na kufikia natija kwamba, katika kipindi cha miaka 30 iliyopita kinara huyo wa Hollywood, yaani Harvey Weinstein amewaudhi, kuwanyanyasa na kuwafanyia ukatili wa kijinsia na kingono wafanyakazi wenzake na watu waliokuwa karibu yake. Matokeo ya uchunguzi huo yanaonesha kuwa, kesi kadhaa zinazomkabili kinara huyo wa filamu za Hollywood zingali mahakamani na kwamba, nyingine zimefungwa kwa mapatano ya pande mbili. New York Times limesisitiza kuwa, kwa uchache Harvey Weinstein amewanyamazisha kimya na kuhitimisha kesi nane kwa kuwalipa fidia ya fedha watu waliokuwa wamemfungulia mashtaka mahakamani.
Katika habari yake ya hivi karibuni New York Times limemnukuu mtayarishaji huyo mashuhuri wa filamu ambaye pia ni miongoni mwa wafadhili wakubwa wa chama cha Democratic akikiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuhusu tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia na ukatili wa kingono na kusema kuwa, anasikitika kuwa katika miaka iliyopita aliamiliana na wenzake kwa njia ambayo iliwasababishia mashaka makubwa na kwamba anaomba radhi.
Baada ya kuchapishwa uchunguzi huo wa New York Times kuhusu kashfa ya utovu wa maadili, ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono, kumefichuliwa kashfa nyingine nyingi za kutumia vibaya madaraka ndani ya Hollywood. Baada ya Harvey Weinstein, vigogo mashuhuri za sekta hiyo kama Ben Affleck, Oliver Stone na Roy Price pia wameandamwa na vyombo vya habari ambavyo vimefichua utovu wao wa maadili. Kuanikwa kwa kashfa na ufuska wa vinara na vigogo hao wa Hollywood siku chache tu baada ya kufichuliwa maovu ya Weinstein, kumewaacha bumbuazi watu wote hususan wanaharakati na mashabiki wa filamu. Inatazamiwa kuwa, kuendelea kwa mwenendo huu yumkini kukaanika na kuweza wazi zaidi uhusiano wenye maradhi na maafa makubwa yaliyoenea katika sekta ya burudani ya filamu nchini Marekani.
Harvey Weinstein ambaye ametayarisha filamu kama "Shakespeare in Love" na "Gangs of New York" amefukuzwa katika Kampuni ya Filamu ya Weinstein baada ya kufichuliwa kashfa hii ya ukatili wa kingono.

Kashfa ya ukatili wa kingoni na ufuska wa Harvey Weinstein huko Hollywood imekuwa na mwangwi mkubwa ndani na nje ya Marekani. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametangaza kwamba, nchi yake itampokonya kinara huyo wa filamu za Hollywood tuzo muhimu na ya juu ya Ufaransa ya "Légion d’Honneur" kutokana na ufuska na utovu wa maadili. Baadhi ya nyota wa vigogo wa Hollywood ambao pia ni marafiki wa Harvey Weinstein wamechukua msimamo dhidi ya rafiki na mwenzao wa zamani. George Clooney, Meryl Streep, Kate Winslet, Judy Dench, Jennifer Lawrence na Patricia Arquette ambao ni miongoni mwa nyota wa filamu waliowahi kufanya kazi ya Harvey Weinstein, wamelaani tabia za ufuska na utovu wa maadili wa mtayarishaji huyo mashuhuri wa filamu.
Miongoni mwa watuhumiwa wa kashfa za Hollywod ni mchezaji mashuhuri na mkurugenzi wa filamu wa Marekani, Ben Affleck. Nukta ya kuashiria hapa ni kwamba, Affleck alikuwa miongoni mwa watu waliozungumzia utovu wa maadili wa Weinstein lakini haukupita muda na yeye mwenyewe akaanza kuandamwa na kashfa za ufuska wa ukatili wa kingono. Ben Affleck ambaye nchini Iran anajulikana kwa kusimamia filamu iliyo dhidi ya Iran ya Argo, mwaka 2003 alimfanyia ukatili wa kingono mcheza filamu na
mtangazaji wa televisheni. Baada ya kufichuliwa kashfa hiyo, Ben Affleck alijitokeza hadharani na kuomba radhi lakini hatua hiyo haikuweza kuondoa dhana na mtazamo mbaya kuhusu kigogo huyo wa sekta ya filamu ya Marekani. Vilevile kuna ushahidi mkubwa wa kuwepo urafiki baina ya Ben Affleck na Harvey Weinstein. Wawili hawa walishirikiana katika kutengeneza filamu ya Shakespeare in Love ambayo mwanamke aliyekuwa mwigizaji wake mkuu alipewa fursa ya kucheza katika nafasi hiyo muhimu baada ya kutumiwa kingono na Harvey Weinstein na baadaye akakwea ngazi za juu katika sanaa hiyo. Kama tunavyoona hapa, uchunguzi wa kina ndani ya baadhi ya filamu mashuhuri za Hollywood unaweza kufichua mahusiano hatari na ufuska mkubwa unaofanyika katika sekta ya filamu nchini Marekani.
Katika upande mwingine kufichuliwa kwa kashfa hii kunapata umuhimu mkubwa kwa kutilia maanani kwamba, Weinstein alihusika katika kutengeneza filamu mashuhuri ambazo zimeshinda tuzo 50 za Oscar. Vilevile katika uchaguzi uliopita wa rais nchini Marekani, Weinstein alikuwa mfadhili wa mgombea wa chama cha Democratic, Hillary Clinton. Katika kampeni zake za uchaguzi, Clinton alijinadi kama mtetezi wa haki za wanawake na alifanya jitihada kubwa za kulishawishi tabaka la wanawake na kupata kura zao dhidi ya Donald Trump ambaye alijulikana kwa kuwadhalilisha na kuwafanyia ukatili wa kingono wanawake. Baada ya tu ya kufichuliwa kashfa ya ukatili wa kingono wa Harvey Weinstein, Hillary Clinton alitoa taarifa akisema: "Kashfa ya pili ya Weinstein imetutia woga na wahka mkubwa. Mienendo yake dhidi ya wanawake haikubaliki na haiwezi kusamehewa. Ushujaa wa wanawake (wa kujitokeza hadharani kuanika maovu ya Harvey Weinstein) na kuwatetea wengine kwa ajili ya kusaidia jitihada za kukomesha mienendo kama hiyo, ni suala lenye umuhimu mkubwa", mwisho wa kunukuu.

Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama ni miongoni mwa watu walioguswa na kashfa ya ukatili wa kingono katika sekta ya filamu ya nchi hiyo Hollywood. Obama ameandika kwamba: "Mimi na Michelle tumechukizwa sana baada ya kusikia habari za kashfa ya Harvey Weinstein".
Jambo linalomtofautisha Weinstein na waovu wengine ni kwamba, wakati alipokuwa na nguvu na mamlaka makubwa aliwanasa katika mtego wake wanawake wengi, na vilio na malalamiko ya sasa dhidi ya kigogo huyo wa Hollywood yamegubika sekta ya filamu ya Marekani na mustakbali wake.
Hadi sasa nyota zaidi ya 40 wa filamu za Hollywood huko Marekani na Ulaya wamejitokea hadharani na kusimulia visa vya jinsi walivyobakwa, kudhalilishwa na kufanyiwa ukatili wa kingono na mtayarishaji huyo mkubwa wa filamu wa Marekani.

Kujitokeza hadhara wanawake wengi waliofanyiwa ukatili wa kingono na mtayarishaji huyo wa filamu ni kielelezo cha uhakika na ukweli wa madai yanayohusu ubaguzi mkubwa wa kijinsia na kukanyagwa haki za wanawake nchini Marekani. Kashfa hiyo pia inasisitiza kwamba, ukatili na manyanyaso dhidi ya wanawake nchini Marekani hususan katika Hollywood bado vinaendelea. Wanawake wametoa mchango mkubwa katika sekta ya filamu ya Marekani lakini inasikitisha kuona kuwa, makampuni yanayomilikiwa au yaliyoko chini ya ushawishi wa wanaume yanaamiliana na wanawake kama watu wa tabaka la duni na la chini ya wanaume. Vilevile yunapaswa kuashiria hapa kwamba, kunyamaza kimya kwa idadi kubwa ya wanawake waliofanyiwa ukatili na manyanyaso hayo ya kingono ni ushahidi wa uhakika kwamba, aghlabu ya wacheza filamu wanawake wa Hollywood wamepata mafanikio katika sekta hiyo baada ya kudhalilishwa na kukubaliana na matakwa ya kutia aibu ya vigogo waovu wa sekta hiyo.