May 23, 2020 10:30 UTC
  • Hotuba ya Kiongozi Muadhamu kwa mnasaba na Siku ya Kimataifa ya Quds

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo (Ijumaa) katika hotuba yake kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds amezungumzia suala la kuanza awamu mpya ya mapambano ya Palestina baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kudhihiri mrengo wa muqawama sambamba kubadilika mlingano wa nguvu kwa maslahi ya wanamapambano na ametoa miongozo saba muhimu kuhusu jinsi ya kuendeleza Jihadi kubwa na takatifu ya sasa.

Amesisitiza kuwa: "Mwongozo wa asili kabisa ni kuendeleza mapambano na kupanua wigo wa Jihadi katika ardhi zote za Palestina, na bila shaka kirusi cha Uzayuni hakitadumu muda mrefu, na kwa hima, imani na ghera ya vijana, kitang'olewa na kuondolewa katika eneo la magharibi mwa Asia."

Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu ametuma salamu za za Idul Fitr kwa Waislamu wote duniani na kusema kuainisha Siku ya Quds ni ubunifu wenye busara wa Imam Khomeini ambao uliwaunganisha Waislamu ili wawe na sauti moja kwa ajili ya Quds tukufu na taifa madhulumu la Palestina.

Kiongozi Muadhamu ameashiria jinsi mataifa yalivyoipokea Siku ya Quds na kusema: "Sera kubwa ya mabeberu na Wazayuni ni kudunisha kadhia ya Palestina katika fikra za jamii za Waislamu ili waisahau; hivyo wadhifa wa dharura zaidi hivi sasa ni kukabiliana na uhaini huu na hapana shaka kuwa ghera, kujiamini na busara inayozidi kuongezeka ya mataifa ya Waislamu haitaruhusu kadhia hii isahaulike." 

Ayatullah Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei amesema kughusubiwa nchi ya Palestina na kuanzishwa donda la saratani la Kizayuni kumeandamana na mauaji mabaya zaidi na jinai. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuendelea udhalimu huu wa kihistoria kwa miongo kadhaa ni rekodi mpya ya ukatili na ushetani wa mwanadamu na kuongeza kuwa: "Mhusika na mhalifu mkuu wa maafa hayo ni madola ya Magharibi na sera zao za kishetani. Amesema: Lengo lao kuu na la makampuni ya Mayahudi lilikuwa kuanzisha serikali ya Kizayuni na kuipa kila aina ya uwezo zikiwemo hata silaha za atomiki na kuanzisha kituo cha kudumu katika eneo la magharibi mwa Asia sambamba na kuwa na uwezo wa kuingilia mambo ya ndani na kuzidhibiti nchi zingine."

Ameongeza kuwa: "Ni jambo la kusikitisha kuwa aghlabu ya tawala za Kiarabu pia baada ya muqawama wa awali, zilisalimu amri hatua kwa hatua na kusahau majukumu yao ya kibinadamu, Kiislamu, kisiasa pamoja na ghera ya Kiarabu na hivyo kumsaidia adui kufikia malengo yake."

Kiongozi Muadhamu amesema matokeo ya kusalimu amri huko ni kubadilisha mkondo wa mapambano na kuchukua mwelekeo usio na matokeo wa kufanya mazungumzo na maghasibu pamoja na waungaji mkono wao. Amesema katika mazingira kama hayo, kuchomoza Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran kulifungua awamu mpya katika mapambano ya Palestina na kwa kudhihiri mrengo wa muqawama, hali imekuwa ngumu zaidi kwa utawala wa Kizayuni na taba'an mustakabali utakuwa mgumu zaidi ya sasa.

Wakati huo huo Ayatullah Khamenei amesema kuwa medani ya mapambano ni hatari sana, yenye mabadiliko na inayohitajia kuwa macho daima. Amesisitiza kuwa, mghafala wa aina yoyote, uzembe na makosa katika mahesabu muhimu katika mpambano huu muhimu sana na unaoainisha mustakbali wa Umma, vitasababisha hasara kubwa.

Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa miongozo saba muhimu kwa watu wote wanaofuatilia sana masuala ya Palestina.

"Kutobanwa maudhui ya Palestina katika masiala ya Kipalestina au Kiarabu tu" ndio mwongozo wa kwanza wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika uwanja huu. Amesema mapambano kwa ajili ya kukomboa Palestina mbali na kuwa ni Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, faradhi na jambo linalotakikana, lakini pia ni suala la kibinadamu; na wale wanaodhani kuwa mapatano ya Wapalestina kadhaa na watawala wa nchi kadhaa za Kiarabu ni ruhusa ya kutupiliwa mbali suala hili la Kiislamu na kibinadamu wametumbukia katika makosa makubwa katika kulifahamu suala hilo na wakati mwingine wanafanya usaliti.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Akifafanua mwongozo wake wa pili, Ayatullah Khamenei amesema: Lengo la mapambano haya ni kukomboa ardhi yote ya Palestina kuanzia Mto (Jordan) hadi Bahari (ya Mediterania) na kurejea Wapalestina wote katika ardhi yao; hivyo kupunguza malengo hayo kwa kutosheka tu na suala la kuundwa dola katika sehemu ndogo tu ya ardhi hiyo si alama ya kupigania haki wala si kielelezo cha kutilia maanani ukweli wa mambo, kwa sababu hii leo mamilioni ya Wapalestina wemefikia upeo wa juu wa fikra, tajiriba na kujiamini kiasi kwamba, wanaweza kusimamia mapambano hayo ya Jihadi na kuwa na matumaini ya nusra ya Mwenyezi Mungu na ushindi wa mwisho. 

Katika mwongozo wake wa tatu, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo ulazima wa jamii ya Waislamu wenye ghera na wanaoshikamana na mafundisho ya dini kutawakali kwa Mwenyezi Mungu katika Jihadi hii kubwa na takatifu na kutegemea nguvu zao za ndani na kujiepusha kuyategemea madola ya kidhalimu ya Magharibi, jumuiya tegemezi za kimataifa na baadhi ya nchi vibaraka na zisizo na heshima za kanda hii ya Asia magharibi na kusema: Hii leo dunia inahesabu wahanga wa virusi vya corona mmoja baada ya mwingine katika maeneo yote ya dunia lakini hakuna mtu anayejiuliza kwamba, ni nani muuaji na mhusika wa mauaji ya mamia ya maelfu ya mashahidi, mateka na watu waliotoweka katika nchi ambako Marekani na Ulaya zimeanzisha vita, na nani mhusika wa jinai hizi zote, kughusubiwa uharibifu na dhulma zinazofanyika Palestina?  

Ayatullah Khamenei ametoa mwongozo wake wa nne akiwalenga viongozi wa kisiasa na kijeshi katika Ulimwengu wa Kiislamu na kusema: Siasa za Marekani na Wazayuni ni kuhamishia mapigano nyuma ya kambi ya mapambano na muqawama na kuanzisha vita vya ndani ili kuishughulisha kambi ya mapambano na kuupa fursa uutawala wa Kizayuni wa Israel, kama kazi ilivyofanyika huko Syria, Yemen na Iraq kwa kuanzishwa kundi la Daesh. Amesema njia ya kuzuia sera hii habithi ni irada na kusimama imara vijana wenye ghera na ari katika Ulimwengu wa Kiislamu na kutilia maanani maagizo ya hayati Imam Khomeini aliyesema kuwa, pazeni sauti zenu zote dhidi ya Marekani na vilevile adui Mzayuni.

Katika mwongozo wake wa tano, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria siasa za Marekani ikisaidiwa na vikaragosi vyake vya kikanda kwa ajili ya kuhalalisha uwepo wa Israel katika kanda hii ya Asia magharibi na kukubalika dola hilo haramu kama uhakika na kusema: Kuna ulazima wa kupambana na uhakika unaoangamiza na unaosababisha madhara; na kama ambavyo hii leo wanadamu wenye uelewa wanaona kuwa ni wajibu kupambana na corona, kupambana na kirusi cha siku nyingi cha Uzayuni pia ni jambo la dharura, na haitachukua muda mrefu kung'oa kabisa mzizi  wa kirusi hicho cha uzayuni katika eneo la magharibi mwa Asia kwa hima, imani na ari ya vijana.

Mwongozo muhimu zaidi wa Ayatullah Khamenei, ni mwongozo wake wa sita ambapo ametaka 'kudumishwa kwa mapambano na kuenezwa uwanja wa jihadi katika arshi zote za Palestina.'

Huku akisisitiza kuwa watu wote wanapasa kulisaidia taifa la Palestina katika jihadi hiyo takatifu, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajivunia kutangaza kwamba itatekeleza wajibu wake katika uwanja huo kadiri ya uwezo wake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Wakati fulani ilibainika kwamba mwanamapambano wa Palestina ana dini, hamasa na ushujaa wa kutosha lakini mikono mitupu isiyo na silaha. Hivyo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mipango ya dharura ilifanyika na uwiano wa nguvu ukawa umebadilika Palestina; kwa kadiri kwamba, hii leo Ukanda wa Gaza unaweza kusimama imara mbele ya hujuma ya kijeshi ya adui Mzayuni na kumshinda.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba, mabadiliko hayo yatabadilisha uwiano wa nguvu katika ardhi zinanazokaliwa kwa mabavu na kuifanya Palestina ikaribie hatua ya kuanzisha hujuma, na kwamba Mamlaka ya Ndani ya Palestina ina wajibu mkubwa katika uwanja huo. Amesema: 'Huwezi kuzungumza na adu katili isipokuwa kwa njia ya nguvu na msimamo madhubuti. Alhamdulillah, uwanja wa kuthibiti jambo hilo tayari unaoonekana wazi katika taifa shupavu na kakamavu la Palestina, ambapo hii leo vijana wa taifa hilo wana kiu ya kulinda heshima yao.'

Ameongeza kwamba Hamas na Jihadul Islami huko Palestina na Hizbullah nchini Lebanon wamewafikishia wote ujumbe ambapo ulimwengu umeshuhudia wazi jeshi katili na linalotenda jinai la utawala ghasibu wa Israel likilazimishwa kuondoka kwa madhila katika ardhi za kusini mwa Lebano chini ya mapigo makali ya Hizbullah na kulazimika kupiga magoti na kuomba usitishaji vita. Hilo ni jambo ambalo jeshi hilo kamwe halitalisahau na hiyo ndio maana ya kuwa na mikono iliyojaa (silaha) na msimamo wenye nguvu.

Ayatullah Khamenei: Hamas na Jihadul Islami na Hizbullah zimeidhalilisha Israel.

Akiashiria hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na serikali moja ya Ulaya ya kuitangaza harakati shupavu na ya mapambano ya Hizbullah kuwa kundi lisilo la kisheria, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Mfumo usio wa kisheria ni kama utawala wa Marekani ambao unazalisha makundi ya kigaidi kama Daesh na utawala mwingine kama huo wa Ulaya ambao ulichangia mauaji ya maelfu ya watu katika maeneo ya Baneh nchini Iran na Halabcheh nchini Iraq kupitia silaha za kemikali, jambo ambalo litaufanya uaibike milele.

Katika mwongozo wake wa saba, Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa Palestina ni ya Wapalestina wote na kwamba inapaswa kuendeshwa kwa irada na matakwa yao. Kwa mara nyingine Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia mpango wa Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya kufanyika kura ya maoni kwa kushirikishwa makundi yote ya kidini na kikabila ya Palestina na kusema: 'Mpango huo unathibitisha wazi kwamba madai yanayokaririwa mara kwa mara na vyombo vya habari vya Magharibi kuhusu chuki dhidi ya Mayahudi hayana msingi wowote na ni uongo mtupu.'

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kwamba kile kinachopaswa kufutwa ni mfumo wa kizayuni na uzayuni.

Mwishoni mwa hutoba yake amewakumbuka mashahihi wa Quds wakiwemo Sheikh Ahmad Yasin, Fat'hi Shuqaqi, Sayyid Abbas Musawi na kamanda mkubwa wa Uislamu na uso usiosahaulika wa mapambano ya Kiislamu, Shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani pamoja na Mujahid mkubwa wa Kiiraki, Shahidi Abu Mahdi al-Muhandes na mashahidi wengine wa Quds,       

Tags