Unafiki wa nchi za Magharibi kuhusu haki za binadamu
Matukio ya ndani ya miezi miwili iliyopita nchini Iran yamezifanya nchi za Ulaya zichukue hatua za kihasama za kuiwekea vikwazo na kuitishia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Umoja wa Ulaya ulitangaza Jumatatu, Novemba 14 katika mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa jumuiya hiyo, kwamba utaweka vikwazo dhidi ya watu 29 na mashirika 3 ya Iran kutokana na kile ulichokiita "matumizi ya nguvu dhidi ya maandamano ya amani". Kituo cha habari cha Press TV ni miongoni mwa taasisi za Iran zilizowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya. Kuwekewa vikwazo Press TV, kituo cha habari cha lugha ya Kiingereza, kunaonyesha sura halisi ya madai ya uongo ya nchi za Ulaya katika kuziwekea vikwazo baadhi ya taasisi na maafisa wa Iran. Kwani kama kweli wana wasiwasi kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran, kwa nini wanaviwekea vikwazo vyombo vya habari vinavyoakisi ukweli na yanayojiri nchini Iran?
Sisi sote tunajua vyema kwamba, malalamiko au maandamano ya kudai au kupinga jambo fulani ni vitu vinavyotokea katika nchi yoyote duniani. Huko huko katika nchi za Ulaya hakuna siku inayopita bila ya kushuhudiwa maandamano ya wananchi wakipinga sera na utekelezaji wa serikali za nchi hizo kuhusiana na masuala mengi ya ndani au kimataifa. Katika maandamano hayo kunashuhudiwa mapambano na vuta nikuvute baina ya waandamanaji na polisi na askari usalama. Hata hivyo vyombo vya habari na maafisa wa nchi za Magharibi daima wamekuwa wakikuza na kutia chumvi matukio ya ndani ya Iran na hata kuchochea ghasia na fujo hapa nchini kwa jina la kutetea haki za binadamu na uhuru wa wanawake!
Tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, nchi za Magharibi zimekuwa na chuki na uadui mkubwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hazikuacha kufanya kila linalowezekana kutoa pigo na dharba kwa mfumo wa Kiislamu hapa nchini ulioundwa kwa msingi wa kupambana na ubeberu na udikteta na kusimamisha uadilifu, maadili mema na kujali maoni ya wananchi. Tangu wakati huo nchi za Magharibi zilianza kuyaunga mkono na kuyasaidia makundi na watu wote waliosimama kupinga na kuyapiga vita Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kwa madola hayo hakuna tofauti katika kuyaunga mkono makundi hayo na zinayasaidia na kuyauunga mkono hata yale yaliyohusika na uhalifu, mauaji na jinai dhidi ya wananchi wa kawaida.

Tangu Februari 12, 1979, siku moja tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, nchi za Magharibi zimekuwa zikiyaunga mkono kikamilifu makundi yanayotaka kujitenga au kurejesha utawala wa kifalme hapa nchini. Mikoa ya mpakani ya Iran ndiyo inayotumiwa zaidi kwa ajili ya kuzusha ghasia na harakati za makundi yanayotaka kujitenga. Kilele cha uhasama huo wa madola ya Magharibi kilionekana vyema zaidi katika uungaji mkono wao kwa kundi la kigaidi la MKO ambalo limeua raia wasiopungua elfu 17 wakiwemo maafisa wa ngazi za juu wa kisiasa hapa nchini. Makao makuu ya kundi hilo la kigaidi yako nchini Ufaransa. Kila mwaka, kundi hili la kigaidi huandaa mkutano kwa pesa zinazotolewa na nchi za Magharibi na kuhudhuriwa na wanasiasa wa Marekani na Ulaya. Sasa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anajitokeza hadharani na kudai kutetea uhuru nchini Iran licha ya rekodi mbaya ya serikali yake ya kuyahami na kuyasaidia makundi ya kigaidi dhidi ya Iran!
Chuki na uadui wa nchi za Ulaya na Marekani zinazodai kutetea uhuru haviishii katika kuyaunga mkono makundi ya kigaidi nchini Iran. Jina la dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein linajulikana duniani kote. Saddam hakusita kufanya uhalifu wa aina yoyote dhidi ya watu wa Iraq na Iran. Hapa kuna jambo la kuzingatia. Leo hii, Marekani inadai kuupindua utawala wa Saddam, ilhali nchi za Ulaya na hata Marekani yenyewe zilikuwa na nafasi kubwa zaidi katika kumchochea dikteta huyo wa Iraq kuivamia ardhi ya Iran na kuimarisha mamlaka yake katika miaka ya 1980 na 1990. Marekani na nchi za Ulaya zilitoa kila aina ya misaada ya kifedha na silaha kwa utawala wa Saddam katika vita vilivyoanzishwa dhidi ya Iran baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Serikali za Ulaya zilitoa silaha za aina mbalimbali na misaada ya hali na mali kwa jeshi la Saddam ili kuishambulia Jamhuri changa ya Kiislamu. Misaada ya nchi za Magharibi kwa utawala wa Saddam Hussein haikuwa na mipaka. Wafaransa walilipa jeshi la utawala wa Baath wa Iraq ndege za kivita aina ya Super Étendard ili kulenga meli za mafuta za Iran katika Ghuba ya Uajemi. Ujerumani na Uholanzi zilitoa silaha za kemikali zilizopigwa marufuku na malighafi za kutengeneza silaha za kemikali kwa utawala wa Saddam. Kichekesho ni kuona Kansela na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani wakidai kutetea uhuru nchini Iran, na Bunge la Bundestag limeidhinisha msururu wa vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Bundestag imeidhinisha mpango wa vipengee 25 kwa anwani ya kulinda haki za binadamu ili kuiwekea mashinikizo zaidi Iran, ilhali dunia bado haijasahau na haitasahau uungaji mkono kamili wa nchi hiyo na jinsi ulivyomuwezesha Saddam Hussein kwa kumpa mabomu 6,000 ya kemikali yaliyotumiwa kushambulia raia wasio na hatia wa Iran. Siku kadhaa zilizopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock aliandika kwenye ukurasa wa Twitter kwamba, Ulaya inafanyia kazi mpango wa vikwazo dhidi ya Iran. Amesisitiza kuwa, wanajaribu kuitisha mkutano maalumu kuhusu Iran katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.

Serikali na Bunge la Ujerumani zinajionyesha kuwa watetezi wa watu wa Iran, ilhali ziliruhusu uhalifu mkubwa zaidi wa haki za binadamu wakati wa vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Saddam, dikteta wa Iraq dhidi ya watu wa Iran na wakazi wa mikoa ya kaskazini mwa Iraq. Zaidi ya watu elfu 17 waliuawa moja kwa moja kwa silaha za kemikali zilizotolewa na Ujerumani kwa utawala wa Saddam. Vilevile zaidi ya wanajeshi na raia 127,000 wa Iran walijeruhiwa kwa sumu ya silaha hizo za kemikali za Ujerumani. Baadhi ya waliojeruhiwa kwa silaha hizo walipelekwa kupewa matibabu katika nchi za Ulaya, ikiwemo Ujerumani yenyewe. Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, theluthi moja ya jumla ya makampuni 445 ya nchi za Magharibi ambayo yalihusika katika kulizatiti jeshi la Saddam Husssein katika nyanja mbalimbali, hasa kwa silaha za kemikali, yalikuwa ya Ujerumani, ambayo mbali na kuuza silaha, yalitoa mafunzo kwa vikosi vya jeshi la Iraq katika vita juu ya jinsi ya kutumia silaha za kemikali dhidi ya Iran.

Ripoti ya Iraq yenye kurasa 12,000 kwa Umoja wa Mataifa kuhusu silaha za nchi hiyo ina mambo muhimu ya kuzingatiwa kuhusu Ujerumani. Katika ripoti hiyo imeelezwa kwa kina ni aina gani ya mikataba ya mauzo ya silaha iliyosainiwa kati ya makampuni ya kijeshi ya Ujerumani na Iraq. Katika ripoti hiyo ambayo gazeti la "Die Tageszeitung," limechapisha baadhi ya vipengee vyake vya siri, Ujerumani inatajwa kuwa mdhamini muhimu zaidi wa maghala ya silaha ya Saddam Hussein. Baadaye, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya The Hague ilitangaza uhalifu wa mashambulizi ya silaha za kemikali za Saddam kuwa ni mauaji ya kimbari dhidi ya binadamu. Hata hivyo hukumu hiyo ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai haikutaja mchango wa nchi za Ulaya, hasa Ujerumani, katika kuupa utawala wa Saddam silaha za kemikali zilizotumika kuua raia wasio na hatia. Baadhi ya majina ya makampuni ya Ujerumani yaliyotajwa katika ripoti ya Iraq kwa Umoja wa Mataifa ni: "Daimler, Mann, Siemens, Benz, Kyoclp, Hoechst, Klochner, Carlsbad". Kampuni ya Karl Korb, ambayo ilishirikiana na Iraq tangu mwaka 1977, ilikuwa ikisimamia ujenzi wa viwanda viwili vikuu vya dawa za kuua wadudu na sabuni huko Baghdad, na katika ripoti ya Iraq yenye kurasa 12,000 kwa Umoja wa Mataifa, kampuni hiyo ilikuwa moja ya wadhamini wakubwa wa silaha za kemikali kwa utawala wa Iraq. Kampuni hiyo ilianzisha viwanda 6 tofauti vya kutengeneza silaha za kemikali nchini Iraq. Viwanda hivyo, vilitengeneza gesi ya haradali na asidi ya prussic na gesi za za sarin na tabun. Kwa mujibu wa ripoti ya Iraq, kampuni ya Preussage pia ilikuwa mmoja wa wauzaji wakubwa wa mada za kemikali zilizotumiwa kuzalisha gesi ya neva ya sarin.

"Edo Ulfkat", mwandishi wa habari wa gazeti maarufu la "Frankfurter Allgemeine" la Ujerumani, ambaye alikuwa ripota wa gazeti hilo katika maeneo ya vita ya Iraq wakati wa vita anasema: "Maafisa wa Ujerumani walifurahishwa sana kumpa Saddam gesi hizo ili zitumiwe dhidi ya Iran." Serikali ya Ujerumani ambayo ni mshirika wa Saddam Hussein katika mauaji ya maelfu ya watu wa Iran na Iraq, sasa inadai kutetea haki za wanawake nchini Iran. Mtazamo wa nchi za Ulaya kuhusu haki za binadamu ni wenzo na propaganda tupu za kutimizia sera na siasa zao za kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Walimwengu wanahoji kwamba, kwa nini Ujerumani na washirika wake wa Ulaya hawana wasiwasi kuhusu wanawake na watoto wa Yemen wanaouawa kwa silaha za nchi za Ulaya na Marekani? Je, raia wa Yemen wanaochinjwa na kuuliwa kila siku kwa silaha za Magharibi zinazotumwia na Saudia na washirika wake si binadamu au ni viumbe kutoka sayari nyingine? Je, madola ya Magharibi yanakuwa vipofu, viziwi na mabubu kiasi kwamba hayaoni uhalifu na mauaji yanayofanywa kila siku na utawala haramu wa Israel huko Palestina? Marekani na nchi za Ulaya hazioni maafa ya wakimbizi wa Kiafrika na mataifa mengine wanaofariki dunia mara kwa mara wakiwa njiani kuelekea Ulaya na badala yake zinawafungia mipaka na kuwaacha wakifamaji au kuangamia kwa baridi kali?
Ukweli ni kwamba nchi za Ulaya zimeanzisha vita vya propaganda na vya vyombo vya habari dhidi ya Iran kupitia njia ya kupindua ukweli na matukio yanayojiri nchini Iran. Hata hivyo hapana shaka kuwa siku hizi pia zitapita na Iran ya Kiislamu itavuka salama njama na hila hizi za kishetani za madola ya Magharibi.