Dec 13, 2020 10:52 UTC
  • Vyama vya Kiislamu Morocco vyapinga uhusiano wa nchi hiyo na Israel

Vyama vya Kiislamu nchini Morocco vimepinga vikali uamuzi wa ufalme wa nchi hiyo wa kuafikia kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel kufuatia mapatano yaliyosimamiwa na Marekani.

Chama cha MUR ambacho kiko katika muungano tawala kimetoa taarifa na kulaani jitihada zote za kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel na kujipenyeza Wazayuni nchini humo. Nacho chama cha  PJD kimesisitiza msimamo wake imara dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Aidha  chama cha Adl Wal Ihssane, ambacho ni kati ya vyama vikubwa zaidi vya upinzani, kimesema kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel ni kusaliti harakati ya kupigania ukombozi wa Palestina.

Donald Trump  Alhamisi iliyopita alitangaza kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba: Mfalme wa Morocco na Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano kamili kati yao. Morocco iliafiki kuanzisha uhusiano na utawala bandia wa Israel baada ya Marekani kusema inatambua rasmi mamlaka ya Morocco katika eneo la Sahara Magharibi ambalo linapigania kujitenga.

Harakati kaadhaa za kupigania ukombozi wa Palestina zimetoa taarifa na kulaani hatua ya Morocco ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na kusema huo ni usaliti wa wazi kwa Wapalestina. Aidha harakati hizo zimesema kufuatia usaliti huo, Morocco haistahiki tena kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Quds (Jerusalem) ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu.

 

Tags