Dec 14, 2020 02:57 UTC
  • Umoja wa Mataifa wasisitiza msimamo wake kuhusu eneo la Sahara Magharibi

Katika hali ambayo katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la taharuki baina ya serikali ya Morocco na Harakati ya Polisaria kuhusiana na eneo la Sahara Magharibi, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza Alhamisi kuwa Morocco imeafiki kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuongeza kuwa Washington inatambua rasmi eneo la Sahara Magharibi kama milki ya Morocco.

Tangazo hilo la Trump limepingwa vikali katika duru za kimataifa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia msemaji wake,  Stephane Dujarric ametangaza kuwa, msimamo wa umoja huo kuhusu Sahara Magharibi haujabadilika hata baada ya Marekani kulitambua eneo hilo kuwa sehemu ya ardhi ya Morocco.

Guterres amesema anaamini kuwa, suluhisho la mgogoro wa Sahara Magharibi litapatikana tu kwa msingi wa maazimio ya Baraza la Usalama. Huku akiashiria taharuki za hivi karibuni katika eneo hilo, Guterres ametaka pande mbili hasimu kujiepusha na taharuki zozote ambazo zinaweza kushadidisha hali ya mambo.

Eneo la Sahara Magharibi limekuwa likizozaniwa kwa muda mrefu baina ya serikali ya Morocco na Harakati ya Polisario. Utawala wa kifalme wa Morocco unataka eneo la Sahara Magharibi litawaliwe na serikali ya mamlaka ya ndani ambayo itakuwa tegemezi kwa ufalme huo. Aidha Morocco inataka kura ya maoni ambayo tu italipa  eneo hilo mamlaka ya ndani. Hii ni katika  hali ambayo, Harakati ya Polisario inapinga vikali pendekezo hilo la Rabat na inataka kura ya maoni ambayo itawapa wananchi haki ya kuamua hatima yao ya iwapo wanataka kujitenga na Morocco au la.

Mfalme Muhammad wa Sita wa Morocco

Eneo hilo lilishuhudia mapigano ya miaka 16 ambayo yalimalizika mwaka 1991 kufuatia mapatano ya usitishwaji vita wa muda. Lakini Harakati ya Polisario ilitangaza kufika ukingoni mapatano hayo ya usitishwaji vita hivi karibuni baada ya Jeshi la  Morocco kutekeleza oparesheni ya kufungua barabara iliyo karibu na Mauritania.

Hivi karibuni Jeshi la Morocco lilikarabati barabara katika eneo la Guerguerat la Sahara Magharibi kwa kisingizio cha kurahisisha usafiri wa malori katika eneo hilo. Harakati ya Polisario imeitaja hatua hiyo ya Jeshi la Morocco kuwa ni uvamizi ambao umevunja mapatano huku ikisema lengo la ukarabati wa barabara hiyo ni kuanzisha mapigano.

Mohamed Salem Ould Al-Salik, Waziri wa Mambo ya Nje wa Harakati ya Polisario amesema kitendo hicho cha Morocco ni uvamizi na kuongeza kuwa: "Vita vimeanza na Morocco ndiyo iliyovunja mapatano ya usitishwaji vita."

Hivi sasa, Rais wa Marekani sambamba na kutangaza kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Israel na Morocco amesema kuwa Washington inatambua mamlaka ya Morocco katika eneo la Sahara Magharibi. Kimsingi hiyo ndiyo karata ya turufu aliyoitumia Trump kuilazimisha Morocco iafiki kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel. Kitendo hicho cha Trump mbali na kukosolewa kimataifa pia kimekosolewa ndani ya Marekani kwenyewe.

Seneta Jim Inhofe, mwenyekiti wa Kamati ya Vikosi vya Kijeshi katika Bunge la Seneti la Marekani, ambaye pia ni kati ya waitifaki wa karibu wa Donald Trump, amekosoa vikali uamuzi wa Ikulu ya White House wa kutambua eneo la Sahara Magharibi kama ardhi ya Morocco mkabala wa Morocco kuafiki kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel. Amesema uamuzi huo wa Trump kuhusu Sahara Magharibi umemshtua.

Bendera ya eneo linalipigania uhuru la Sahara Magharibi

Harakati ya Polisario imesema imesikitishwa na uamuzi huo wa Marekani na kusisitiza kuwa, haitabadili msimamo wake kuhusu Sahara Magharibi.

Umoja wa Afrika nao pia umechukua msimamo sawa na wa Umoja wa Mataifa. Katika taarifa, Ebba Kalondo, msemaji wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, amesema umoja huo unaunga mkono kura ya maoni ya kuamua hatima ya Sahara Magharibi kama ilivyoamuliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Msimamo uliochukuliwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ni ishara ya kufeli tena sera za upande mmoja za Trump. Aidha mtawala huyo wa Marekani amethibitisha tena anavyopuuza sheria za kimataifa. 

Ni wazi kuwa uamuzi huo wa Trump  umechukuliwa kwa ajili ya kufikia malengo ya Marekani na maslahi ya Israel na hivyo kadhia ya Sahara Magharibi haiwezi kutatuliwa kwa uamuzi kama huo.

Tags