May 21, 2021 03:36 UTC
  • Morocco yazuia maandamano ya kulalamikia jinai za Israel kwa Wapalestina

Serikali ya Morocco ambayo hivi sasa imo kwenye mkumbo wa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia ya utawala wa Kizayuni wa Israel, imezuia kufanyika maandamano ya mamilioni ya wananchi wa nchi hiyo waliokusudia kupaza sauti zao, kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina.

Mtandao wa habari wa "Arabi 21" umeripoti kuwa, serikali ya Morocco imekataa kutoa kibali cha kufanyika maandamano ya mamilioni ya watu ya kuiunga mkono Quds na Ghaza na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni. Maandamano hayo yalikusudia pia kulaani vikali jinai ya Israel ya kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa, kupora ardhi za Wapalestina, kuendelea kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na njama za kuwafukuza Wapalestina kwenye makazi yao.

Siku chache zilizopita, mamia ya wananchi wa Morocco walifanya maandamano ya kutangaza mshikamano wao na wananchi wa Palestina na kushinikiza kufutwa makubaliano ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Maandamano ya kupinga utawala wa Kizayuni wa Israel Morocco

Kwa mujibu wa gazeti la al Quds al Arabi, washiriki wa maandamano hayo yaliyofanyika kwenye mji wa al Qunaitra wa kaskazini wa Morocco, walitangaza kuungana kwao na wananchi wa Palestina na kulaani vikali jinai na mashambulizi yanayoendelea ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Waandamanaji hao walielezea kukasirishwa mno pia na jinai ya Wazayuni ya kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu, kupora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.

Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain, Sudan na Morocco zimetangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni hatua ambayo inahesabiwa ni usaliti wa wazi wa matukufu ya Palestina.

Tags