Jul 22, 2021 11:17 UTC
  • Wafaransa wawili watiwa mbaroni kwa kufanya njama za kumuua rais wa Madagascar

Duru za habari zimeripoti kutiwa mbaroni raia wawili wa Ufaransa kwa tuhuma za kufanya njama za kutaka kumuua Rais wa Madagascar.

Vyombo hivyo vya habari vimeripoti hayo leo Alkhamisi na kuongeza kuwa, Wafaransa hao wawili walitiwa mbaroni siku chache zilizopita wakikabiliwa na tuhuma za kuendesha njama za kumuua Rais Andry Rajoelina wa Madagascar.

Ripoti hizo zinasema kuwa, Rais Rajoelina ameokoka katika njama hizo na hivi sasa sasa wageni wengine pamoja na Wamadagascar wenye uraia wa zaidi ya nchi moja wametiwa mbaroni na wanashikiliwa korokoroni.

Radio ya Kimataifa ya Ufaransa kwa upande wake imetangaza kuwa, raia wa Ufaransa waliotiwa mbaroni wakihusishwa na njama hizo ni Mmadagascar mwenye uraia wa Ufaransa na mwingine ni raia wa Ufaransa mwenye asili ya Ufaransa anayejulikana kwa jina la Philip Francoi.

Viongozi wawili wenye ushindani mkubwa nchini Madagascar, Rais Andrey Rojoelina (kushoto) na Marc Ravalomanana

 

Baada ya kutiwa mbaroni Wafaransa hao wawili juzi Jumanne, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali ya Madagascar amesema leo kuwa, nchi hiyo imevunja njama za kutaka kumuua Rais Andry Rajoelina.  Berthine Razafiarivony amesema kuwa, kulikuwa njama za kuwaua viongozi kadhaa muhimu wa Madagascar akiwemo mkuu wa nchi lakini njama hizo zimeshindwa.

Watu kadhaa walitiwa mbaroni juzi Jumanne wakiwemo Wafaransa hao wawili. Wafaransa hao wawili na wanajeshi wastaafu wa serikali ya Ufaransa. 

Madagascar ambayo ni koloni la zamani la Ufaransa lina historia ndefu ya mapinduzi ya kijeshi, mauaji na machafuko tangu ilipojikomboa kutoka katika makucha ya mkoloni kizee, Ufaransa, mwaka 1960. Mara kwa mara Wafaransa wanahusika na machafuko ya Madagascar.

Tags