Jul 26, 2021 12:27 UTC
  • Jeshi la Somalia lamkamata kamanda mkuu wa al-Shabaab

Jeshi la Taifa la Somalia limetangaza habari ya kumtia mbaroni kiongozi wa ngazi ya juu wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab kusini mwa nchi hiyo.

Taarifa ya jeshi hilo imesema Ali Mohamed Adan, kamanda mkuu wa operesheni za kigaidi za kundi hilo katika jimbo la Lower Shabelle ametiwa mbaroni katika operesheni iliyofanyika jana Jumapili katika mji wa Janaale, kusini mwa nchi.

Maafisa wa Jeshi la Taifa la Somalia wamesema Adan ndiye mhusika mkuu wa aghalabu ya mashambulizi yaliyofanyika katika eneo hilo, zikiwemo hujuma za mabomu ya kutegwa kando kando ya barabara kuu za jimbo hilo.

Jeshi la Somalia limeapa kuendeleza operesheni za kusafisha mabaki ya wanachama wa genge hilo la ukufurishaji katika maeneo hayo ambayo yangali chini ya udhibiti wa kundi hilo.

Ramani inayoonesha jimbo la Lower Shabelle la kusini mwa Somalia

Katika hatua nyingine, wanachama 13 wa al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni ya askari wa Somalia katika mji wa Awdhegle, yapata kilomita 70 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu.

Habari zaidi zinasema kuwa, jeshi la Somalia limefanya shambulio hilo, kama jibu la hujuma ya Jumamosi ya juzi ya wanachama wa kundi hilo dhidi ya kambi za kijeshi katika mji huo ulioko katika jimbo la Lower Shabelle. Operesheni nyingine ya ulipizaji kisasi dhidi ya genge hillo la kigaidi imefanyika katika mji wa Baadweyn katika jimbo la Mudug.

 

 

 

Tags