Apr 05, 2024 02:20 UTC
  • Somalia yamtimua balozi wa Ethiopia kutokana na mgogoro wa mkataba wa bandari ya Somaliland

Somalia imetangaza kumfukuza balozi wa Ethiopia nchini humo huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kuhusu mzozo wa makubaliano ya bandari kati ya Ethiopia na eneo lililojitenga la Somaliland.

Ofisi wa Waziri Mkuu wa Somalia ilitangaza jana Alkhamisi kwamba Balozi wa Ethiopia nchini humo Mukhtar Mohamed amerejeshwa nyumbani kwa mashauriano.
 
Taarifa ya ofisi hiyo aidha imesema, Mogadishu inazifunga balozi ndogo za Ethiopia huko Hargeisa, mji mkuu  na mkubwa zaidi wa Somaliland, na Garowe, mji mkuu wa eneo linalojiendeshea masuala yake la Puntland.
 
Ofisi ya waziri mkuu wa Somalia imeendelea kueleza: "uingiliaji wa wazi wa serikali ya Ethiopia katika masuala ya ndani ya Somalia ni ukiukaji wa uhuru na mamlaka ya Somalia".
 
Katika taarifa fupi aliyotoa kupitia mtandao wa kijamii wa X, Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Ali Omar ameongeza kuwa Mohamed amepewa saa 72 kuondoka nchini humo. "Somalia inasimama kidete katika uhuru wake," amesisitiza Omar akisema: "Uamuzi wetu wa kulinda eneo letu ni thabiti".
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed (kushoto) na Rais Muse Bihi Abdi wa Somaliland wakisaini hati ya makubaliano

Mzozo baina ya nchi mbili uliibuka baada ya Ethiopia isiyo na bandari kusaini hati ya makubaliano mnamo Januari 1 na eneo la Somaliland ya kukodishwa kilomita 20 (maili 12) za ukanda wa pwani ya eneo hilo.

Chini ya mpango huo, ukanda huo ulioko karibu na bandari ya Berbera, kwenye Ghuba ya Aden, utatumiwa na Ethiopia kwa miaka 50 kwa madhumuni ya kijeshi na kibiashara.

Ethiopia ilisema inataka kuanzisha kituo cha jeshi la wanamaji katika ukanda huo wa pwani ya eneo la Somaliland, mkabala wa uwezekano wa kuitambua Somaliland kama nchi na hivyo kuibua ghadhabu na hasira za Somalia - ambayo iliituhumu Ethiopia kuwa inajaribu kunyakua sehemu ya eneo lake - na kuhofia kuwa makubaliano hayo yanaweza kuyumbisha zaidi amani na uthabiti wa eneo la Pembe ya Afrika..../

 

Tags