Jul 28, 2021 01:37 UTC
  • Kutokea mapinduzi baridi nchini Tunisia

Katika hatua inayotathminiwa na wajuzi wa mambo kama mapinduzi baridi, Rais Kais Saied wa Tunisia amechukua hatua kadhaa kama kumfuta kazi Waziri Mkuu wa nchi hiyo Hichem Mechichi, kuvunja baraza la mawaziri, kusitisha shughuli za Bunge na kinga ya kisiasa ya Wabunge na kisha kudhibiti madaraka yote ya nchi.

Rais wa Tunisia ametangaza kuwa, kwa msaada wa Waziri Mkuu mpya atachukua madaraka ya utendaji. Hatua hiyo inatajwa kuwa ya aina yake dhidi ya katiba ya nchi katika kipindi cha muongo mmoja uliopita nchini Tunisia, katiba ambayo inagawa mamlaka baina ya Rais, Waziri Mkuu na Bunge.

Weledi wa mambo wanasema kuwa, hatua hiyo inaweza kuitumbukiza Tunisia katika mgogoro mkubwa kabisa wa kisiasa ambao haujashuhudiwa tangu alipoondolewa madarakani kwa vuguvugu la wananchi Zeinul Abidin bin Ali mwaka 2011. Mapinduzi hayo baridi yamefuatia miezi kadhaa ya vuta nikuvute ya kisiasa katika nchi hiyo ndogo ya kaskazini mwa Afrika. Pamoja na hayo, hatua ya Rais wa Tunisia imekabiliwa na radiamali hasi huku wimbi la ukosoaji likichukua wigo mpana zaidi.

Ali al-Aridh, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya al-Nahdha ametangaza kuwa, maamuzi yaliyotangazwa na Rais Kais Saied yanahesabiwa kuwa ni mapinduzi dhidi ya asasi za serikali, katiba na mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo. Inaonekana kuwa, katika siku za usoni tutaraji maandamano na mikusanyiko ya wapinzani na waungaji mkono wa mapinduzi hayo baridi ya Rais Kais Saied.

Hichem Mwechichi, Waziri Mkuu wa Tunisia aliyefutwa kazi  na Rais

 

Katika kuhalalisha uamuzi wake huo wa kushtukiza na ulio dhidi ya katiba, Rais Kais Saied amesema kuwa, amechukua hatua hiyo kutokana na utendaji mbya wa serikali katika kukabiliana na virusi vya corona na kuzidi kuzorota hali ya uchumi wa nchi.

Pamoja na hayo hatupasi kusahau kwamba, kwa muda sasa Tunisia imekuwa katika vuta nikuvute ya kisiasa ambapo Waziri Mkuu na Rais wamekuwa wakizozana na kuhitalifiana hasa katika mchakato wa kuchagua mawaziri wa kushika wizara mbalimbali. Kimsingi ni kuwa, kumekuweko na vita vya madaraka baina ya wawili hao.

Katika majuma kadhaa ya hivi karibvuni, wananchi wa Tunisia wamekuwa wakifanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kulalamikia utendaji mbovu wa serikali katika kukabiliana na virusi vya corona, hali ya mbaya ya uchumi na maisha kuzidi kuwa magumu. Rais Kais Saied aliwaonya waaandamanaji akiwataka vijana kutoanzisha vurugu kwa sababu ya umasikini wao.

Mzozo wa kisiasa nchini Tunisia unashika kasi katika hali ambayo, nchi hiyo hivi sasa inakabiliwa na janga la virusi vya corona, ambalo limesababisha hali ya uchumi wa nchi kubwa mbaya kuliko hapo kabla, huku umasini na ukosefu wa ujira ukifikia katika kiwango cha juu kabisa.

Maandamano ya wananchi wa Tunisia

 

Hali hiyo imewafanya wananchi wengi wa Tunisia kujitoikeza katika mitaa na barabara za miji mbalimbali ya nchi hiyo na kuandamana wakilalamikia hali mbaya ya kiuchumi na kijamii.

Jumapili ya juzi, maelfu ya waandamanaji walikabiliana na polisi waliokuwa wakiwazuia kuandamana ambapo wakiwa na mabango na maberamu walikuwa wakipiga nara dhidi ya chama tawala. Ikumbukwe kuwa, miezi kadhaa iliyopita, Jumuiya ya Wafanyakazi nchini Tunisia ilitahadharisha kuhusiana na kuendelea hali mbaya ya kiuchumi na kijamii katika nchi hiyo hasa kutokana na serikali kutochukuua hatua za maana na athirifu kwa ajili ya kuhitimisha mwenendo huu wa kuporomoka kiuchumi nchi na mzozo wa kisiasa.

Wajuzi wa mambo wanasema kuwa, licha ya kupita miaka 10 tangu kuibuka vuguvugu la wananchi lililomuandoa madarakani dikteta bin Ali, siyo tu kwamba, uthabiti wa kisiasa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika haujarejea, bali demokrasia, matakwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ya wananchi yamegubikwa na wingi zito la mzozo na vita vya kuwania madaraka.

Filihali kushindwa serikali kuboresha uchumi na kutochukua hatua athirifu za kukabiliana na virusi vya corona imekuwa sababu na kisingizio sasa cha rais kuvunja baraza la mawaziri na kusimamisha shughuli za Bunge. Hatua ya Rais ya kupuuza mamlaka ya Katiba inayogawa madaraka, na kuchukua uamuzi wa kumfuta kazi Waziri Mkuu na kuvunja Bunge, kivitendo kiongozi huyo amehodhi madaraka yote ya nchi kwa himaya na uungaji mkono wa jeshi.

Pamoja na hayo, siku za usoni huko Tunisia zinatarajiwa kuambatana na malalamiko makubwa na maandamano ya kupinga hatua hiyo ya Rais Kais Saied, hali ambayo bila shaka itazidi kuchochea kuni za moto wa mivutano ya kisiasa nchini humo na kupanua wigo wake; na hivyo kuitumbukiza zaidi nchi hiyo katika vurugu na machafuko.

Tags