Aug 01, 2021 02:29 UTC
  • Muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia waendeleza mashambulio ya anga dhidi ya Yemen

Muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala vamizi wa Saudi Arabia umeendelea kuyashambulia maeneo mbalimbali ya nchi masikini ya Yemen.

Kanali ya Televisheni ya al-Masirah iliripoti jana Jumamosi kwamba, katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, majeshi vamizi yakiongozwa na Saudi Arabia yametekeleza mashambulio mara tatu katika kitongoji cha al-Abdiyah katika mkoa wa Ma'rib wa katikati mwa nchi hiyo.

Aidha maeneo kadhaa katika mkoa wa al-Jawf nayo yameshambuliwa na muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia mara mbili na kusababisha uharibifu mkubwa.

Wakati huo huo imeelezwa kuwa, katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia umekiuka mara 136 usitishaji vita huko al-Hudaydah ukiushambulia mji huo wa bandari kwa mizinga na silaha nzito.

Mashambulio ya anga ya Saudi dhidi ya Yemen

 

Saudi Arabia huku ikungwa mkono na Marekani na nchi nyingine kadhaa, Machi 25 mwaka 2015 zilianzisha hujuma na mashambulizi makubwa huko Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, angani na nchi kavu. 

Vita hivyo vya kidhulma vya Saudia na waitifaki wake huko Yemen hadi sasa vimesababisha kuuliwa Wayemeni zaidi ya elfu 16, kujeruhiwa makumi ya maelfu na kuwa wakimbizi mamilioni ya wengine. 

Aidha asasi na jumuiya mbalimbali za misaada ya kibinadamu zimetahadharisha mara chungu nzima kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu inayoikabili Yemen na hata uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu katika nchi hiyo.

Tags