Jan 28, 2021 10:53 UTC
  • Kujitakia makuu serikali ya Biden kuhusu Iran na mapatano ya JCPOA

Maafisa wa serikali mpya ya Joe Biden nchini Marekani ambao huko nyuma walikuwa wakitoa matamshi kinyume na msimamo wa serikali ya wakati huo ya nchi hiyo, hivi sasa wanaonyesha kuwa na mitazamo sawa, bali hata kutumia lugha ile ile ya serikali ya Donald Trump kuhusu Iran na mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken  siku ya Jumatano katika mkutano wake wa kwanza na waandishi habari aliashiria kadhia ya Iran na kusema: "Iwapo Iran itafungamana kikamilifu  na ahadi zake katika mapatano ya JCPOA, Marekani nayo itafanya hivyo." Aidha aliongeza kuwa, kurejea Marekani katika JCPOA kutaandamana na kuwepo mapatano madhubuti zaidi na yatakayodumu kwa muda mrefu zaidi yatakayojumuisha masuala mengine yenye utata katika uhusiano na Iran. Amesema mapatano kama hayo yatafikiwa kwa msaada wa waitifaki wa Marekani.

Ni wazi kuwa kwa msingi wa msimamo huo uliotangazwa na Blinken hakuna matumaini ya Marekani kurejea katika mapatano ya JCPOA bila masharti. Iran imetangaza mara kadhaa kuwa iwapo Marekani itarejea katika JCPOA na kuondoa vikwazo vyote vilivyowekwa kinyume cha sheria wakati wa Trump, nayo pia itakuwa tayari kutekeleza ahadi zake katika JCPOA. Lakini inavyoonekana sasa ni kuwa utawala wa Biden umetumia ujanja wa kuutupa mpira katika uwanja wa Iran na kudai kuwa Iran ndiyo inayopaswa kuanza kutekeleza ahadi zake katika JCPOA.

Inaelekea kuwa wakuu wa serikali mpya ya Marekani wamesahau kuwa, ni Marekani ambayo, wakati wa utawala wa Trump, mnamo Mei 2018 ilijiondoa katika JCPOA na kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi katika fremu ya ile sera ya 'mashinikizo ya juu kabisa'.

Hatua mpya ambazo Iran imechukua katika kupunguza ahadi zake katika JCPOA ikiwa ni pamoja na hatua ya karibuni ya kutekeleza sheria iliyopitishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ya kutaka urutubishaji urani uongezwe hadi kiwango cha asilimia 20, yote hayo ni katika fremu ya kujibu uhasama wa Marekani dhidi ya JCPOA. Aidha Iran imechukua hatua hizo baada ya nchi za Ulaya katika kundi la 4+1 kukwepa kutekeleza ahadi zao katika JCPOA.

Kwa hivyo, inashangaza sana kuona kuwa, katika wakati huu badala ya serikali mpya ya Biden kuomba msamaha na kurejea katika JCPOA, utawala huo wa Wademocrat unaanza kutoa matamshi ya kujitakia makuu dhidi ya Iran.

Alireza Miryusefi, msemaji wa ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa katika kujibu matamshi hayo ya mwanzo kutolewa na waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani amesema kuwa, "ni Marekani na wala si Iran iliyokataa kutekeleza ahadi zake katika JCPOA sambamba na kukiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la  Umoja wa Mataifa."

Nukta nyingine katika matamshi ya kujitakia makuu Blinken  ni kuwa anataka mapatano mapya na Iran yaliyo nje ya mapatano ya awali wa JCPOA.

Makusudio ya Blinken ni kuwa, maudhui za uwezo wa kimakombora na sera za kieneo za Iran ziwekwe kwenye meza ya mazungumzo yajayo na Iran.  Aidha katika matamshi yake hayo amesema Marekani itapata msaada wa waitifaki wake. Kwa kuzingatia matamshi ya huko nyuma ya Biden na timu yake ya sera za kigeni, inaelekea kuwa makusudio ya waitifaki hapa ni nchi za Ulaya zinazoafikiana na Marekani hasa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza na pia waitifaki wa kieneo wa Marekani kama vile utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia.

Kwa hivyo ni wazi kuwa, utawala wa Biden si tu kuwa unataka kupanua zaidi mapatano ya nyuklia ya JCPOA ili kuweka vizingiti zaidi katika shughuli za nyuklia za Iran zenye malengo ya amani bali pia sasa Washington inataka kujadili uwezo wa makombora ya Iran na halikadhalika sera za Iran katika eneo.

Makombora ya Iran yakifanyiwa majaribio

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa, itafungamana tu na mapatano ya nyuklia ya JCPOA na katu haitasalimu amri mbele ya matakwa mapya ya Marekani.

Msimamo huu wa Tehran unaungwa mkono wa wanachama wa Mashariki katika kundi la 4+1 yaani China na Russia. Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia hivi karibuni imetoa taarifa na kusisitiza kuwa, kurejea Marekani katika JCPOA hakupaswi kutoa mwanya au kisingizio cha kuibebesha Iran masharti mapya.

Kwa vyovyote vile, kilicho wazi ni kuwa, iwapo serikali ya Biden itakariri makosa ya Trump kuhusu Iran na hivyo ifuate mkondo uliofeli huko nyuma, Iran nayo pia itatekeleza stratijia yake ya muqawama na mapambano ya hali ya juu katika fremu ya kuimarisha kiwango na kasi ya shughuli zake za nyuklia kwa malengo ya amani.

Tags