Mar 06, 2021 02:54 UTC
  • Marekani na miundombinu yake iliyoatilika kwa ndani na kupenda kwake vita duniani

Baada ya kipindi cha vita baridi lakini zaidi baada ya mashambulio ya Septemba 11, 2001, Marekani imeshadirisha siasa zake za kupenda vita na kuzusha machafuko duniani kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Hadi hivi sasa imeshatumia mamia ya mabilioni ya dola katika jambo hilo. Hiyo ni katika hali ambayo, wataalamu wa ndani ya Marekani wanakiri kwamba miundombinu muhimu ya nchi hiyo iko katika hali mahututi.

Ripoti ya kurasa 170 ya Jumuiya ya Wahandisi wa Miji ya Marekani ambayo ilisambazwa siku ya Jumatano inasema kuwa, sasa hivi Marekani ina nakisi ya dola trilioni mbili na bilioni 590 zinazohitajika kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya taasisi zake za miundombinu. Ubovu wa miundombinu kama vile kutokuwa barabara za Marekani na viwango vinavyotakiwa, kushindwa kukarabatiwa madaraja, na kutoendelezwa inavyotakiwa miradi mingine ya ujenzi kunazitia hasara ya fedha nyingi, serikali za Marekani. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hivi sasa Marekani inatumia zaidi ya nusu tu ya fedha zinazohitajika kwa ajili ya kuimarisha miundombinu yake hivyo. Hii ni kusema kuwa, hali jumla ya miundombinu ya Marekani hivi sasa ni ya kati na kati. Ripoti hiyo ambayo hutolewa mara moja kila baada ya miaka minne imeipa Marekani daraja C wakati ambapo mwaka 2017, Marekani ilipata daraja D+ katika ripoti hiyo. Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20 iliyopita kwa Marekani kuporomoka kiasi hicho cha hadi daraja C katika ripoti hiyo.

Miundombinu mibovu imewasababishia matatizo mengi wananchi wa Marekani

Ripoti hiyo imetolewa katika hali ambayo Joe Biden, hivi sasa ana nia ya kuongeza kwa kiwango kikubwa fedha za kuimarisha miudombinu ya Marekani katika serikali yake. Wakati ambapo marais wa huko nyuma yaani Donald Trump na Barack Obama walishindwa kuikinaisha Congress ya nchi hiyo ipashishe fedha za kuwawezesha kuimarisha mindumbinu hiyo, sasa hivi Joe Biden ana matumaini ya kutengewa fedha hizo.

Cha kushangaza zaidi hapa ni kwamba, rais aliyepita wa Marekani Donald Trump ambaye alikuwa na vituko na makelele mengi, muda wote alikuwa akikiri hadharani kwamba hali ya miundombinu ya Marekani haifai bali ni mahututi. Muda wote alikuwa akisema kuwa miundombinu hiyo imetumbukia kwenye shimo la kusambaratika na aliahidi kwamba atachukua hatua kubwa na za kimsingi za kuzuia kusambaratika huko. Hata hivyo na licha ya kutoa ahadi hizo lakini kama kawaida yake hakuzitekeleza na badala yake aliongeza kwa wingi bajeti ya kijeshi na kupanua wigo wa vita na kueneza machafuko katika sehemu mbalimbali duniani. Bajeti ya kwanza ya kijeshi iliyopasishwa wakati wa urais wa Donald Trump mwaka 2018 ilikuwa ni dola bilioni 700. Bajeti hiyo iliendelea kupanda kiasi kwamba katika mwaka wa mwisho wa urais wa Trump yaani 2021, bajeti ya kijeshi ya Marekani ilikuwa imeshafikia dola bilioni 740. Huo ni uthibitisho wa wazi kwamba serikali za Marekani zinashungulishwa zaidi na bajeti za kijeshi na kuzusha vita na machafuko duniani kuliko kutenga fedha za kutosha za kukarabati madaraja na mabarabara, maji na umeme na kuimarisha miundombinu ndani ya nchi hiyo kwa manufaa ya Wamarekani.

Foleni ya gesi Texas Marekani. Miundombinu mibovu imewasababishia matatizo mengi wananchi wa Marekani

 

Sayyid Ahmad Mousavi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema. katika dunia ambayo China na nchi mbalimbali za Magharibi na zinazoendelea zinafikiria kuimarisha zaidi miundombinu yao, Marekani inafuata siasa zinazokinzana kabisa na hizo.

Matokeo ya siasa hizo mbovu za Marekani ni kwamba mwezi Februari 2021, nchi hiyo inayojigamba kuwa imeendelea zaidi duniani, ilikumbwa na mgogoro wa kukatika mara kwa mara umeme na maji katika jimbo la Texas kutokana na kunyesha kiwango kikubwa cha theluji. Wakazi wa jimbo la Texas walikumbwa na wakati mgumu sana, walilazimika kupanga foleni za kilomita kadhaa kwa ajili ya kupata lita chache za maji ya kunywa. Moja ya sababu za hali hiyo mbaya ni kuchakaa mabomba ya kusambazia maji katika jimbo hilo la Texas. Hali hiyo mbaya bado ipo hadi hii leo. Hali katika majimbo mengine ya Marekani inafanana na hiyo. Hali hiyo mbaya ya kuatilika na kuchakaa miundombinu si tu inawakosesha amani wananchi, lakini ina madhara makubwa na hatari pia kwa uchumi wa Marekani.

Ukweli ni kwamba serikali zote zinazoingia madarakani huko Marekani, iwe za Wademocrat au Warepublican, zote zimekuwa zikishughulishwa zaidi na bajeti za kijeshi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, badala ya kutenga fedha za kutosha za kuimarisha miundombinu na huduma kwa umma.

Foleni ya maji Texas Marekani. Miundombinu mibovu imewasababishia matatizo mengi wananchi wa Marekani

 

Tags