Jenerali Tchiani atangazwa mkuu wa serikali ya mpito Niger
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i100416-jenerali_tchiani_atangazwa_mkuu_wa_serikali_ya_mpito_niger
Jenerali Abdourahmane Tchiani, Mkuu wa Gadi ya Rais wa Niger ameteuliwa kuwa kiongozi wa serikali ya mpito ya nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika, siku moja baada ya jeshi la nchi hiyo kutangaza kuwa limemuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 28, 2023 08:45 UTC
  • Jenerali Tchiani atangazwa mkuu wa serikali ya mpito Niger

Jenerali Abdourahmane Tchiani, Mkuu wa Gadi ya Rais wa Niger ameteuliwa kuwa kiongozi wa serikali ya mpito ya nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika, siku moja baada ya jeshi la nchi hiyo kutangaza kuwa limemuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum.

Kwa mujibu wa tangazo hilo la leo Ijumaa kupitia televisheni ya dola, Abdourahmane Tchiani anayefahamika pia kama Omar Tchiani, ni jenerali wa kijeshi mwenye miaka 62 ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo Maalumu tokea mwaka 2015.

Inasemekana kuwa anatokea jimbo la Tillaberi magharibi mwa Niger, ambalo limesalia kuwa eneo linalosajili idadi kubwa zaidi ya wanajeshi wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi. 

Jenerali Tchiani aliongoza mapambano dhidi ya jaribio la mapinduzi mengine mnamo Machi 2021, wakati kitengo cha jeshi la nchi hiyo kilipojaribu kutwaa Kasri ya Rais,siku chache kabla ya Bazoum kuapishwa. 

Bazoum alichaguliwa kuwa rais katika uchaguzi wa 2021 ambao ulikuwa wa kwanza wa mpito wa mamlaka ya kidemokrasia katika nchi hiyo ambayo imeshuhudia mapinduzi manne ya kijeshi tangu uhuru kutoka kwa Ufaransa mnamo 1960.

Rais Bazoum aliyepinduliwa huko Niger

Usiku wa kuamkia jana, Kanali Amadou Abdramane, aliyeandamana na maafisa wengine tisa wa kijeshi alisema katika taarifa kuwa, vikosi vya ulinzi na usalama vya Niger vimeamua kumpindua Bazoum kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama na utawala mbaya.

Viongozi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) wamelaani mapinduzi hayo ya kijeshi Niger na wametaka Rais Bazoum aachiliwe huru bila masharti yoyote na wanajeshi warejee kwenye kambi zao.