Uingiliaji wa kigeni katika mapinduzi ya Niger
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i100570-uingiliaji_wa_kigeni_katika_mapinduzi_ya_niger
Baada ya kupita takribani wiki moja tangu kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini Niger, mgogoro wa kisiasa umeenea katika nchi hiyo na nchi na taasisi za kieneo na kimataifa zimechukua misimamo tofauti katika uwanja huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 01, 2023 11:36 UTC
  • Uingiliaji wa kigeni katika mapinduzi ya Niger

Baada ya kupita takribani wiki moja tangu kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini Niger, mgogoro wa kisiasa umeenea katika nchi hiyo na nchi na taasisi za kieneo na kimataifa zimechukua misimamo tofauti katika uwanja huu.

Hatua ya karibuni zaidi ni ile iliyotangazwa na Jumuiya ya Kiuchumi yaa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ambayo imesitisha miamala yote ya kibiashara na kifedha kati ya Niger na nchi zote wanachama wa jumuiya hiyo na kutangaza kuwa, itaweka marufuku ya kusafiri na kufungia mali za maafisa wa kijeshi waliohusika katika mapinduzi ya Niger.

Jumatano, 26 Julai, kundi la maafisa wa kijeshi wa Niger kupitia televisheni walitangaza mapinduzi, baada ya walinzi wa rais kumuweka kizuizini ndani ya ofisi yake katika mji mkuu wa Niger, Niamey. Kamanda wa kikosi cha ulinzi wa rais, Jenerali Abdourahmane Tchiani, ameteuliwa kuwa mkuu wa baraza la mpito la nchi hiyo.

Mapinduzi ya Niger yamefuatiwa na misimamo tofauti miongoni mwa watu wa nchi hiyo na nchi za nje. Ndani ya Niger, mamia ya wafuasi wa mapinduzi waliandamana mbele ya ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu, Niamey. Walimchukulia Muhammad Bazoum Rais aliyepinduliwa kuwa mshirika wa nchi za Magharibi hasa Ufaransa ambapo huku wakiunga mkono kuondolewa kwake madarakani, walitaka Wamagharibi wasiingilie mambo ya ndani ya nchi yao. Wakati huo huo, waandamanaji wanaounga mkono mapinduzi ya Niger walipeperusha bendera ya Urusi na kutoa nara na kaulimbiu dhidi ya Ufaransa.

Muhammad Bazoum, Rais wa Niger aliyepinduliwa

 

Niger ni mojawapo ya nchi muhimu na zenye ushawishi katika eneo la Afrika Magharibi, ambayo, kama ilivyo kwa nchi nyingi za bara hili, ina rasilimali nyingi za asili, hususan urani, almasi, dhahabu na makaa ya mawe; migodi ambayo siku zote imekuwa muhimu kwa nchi za Magharibi. Kwa mfano, teknolojia ya nyuklia ya Ufaransa, yenye vinu 56 vya nyuklia, takribani inategemea rasilimali nyingi za asili za urani za Niger.

Filihali inaonekana kwamba mapinduzi ya Niger yana athari kubwa kwa maslahi ya Ufaransa barani Afrika; hasa katika nchi mbili za Mali na Burkina Faso, ambazo ni jirani na Niger ambazo zinapinga uwepo wa Wafaransa katika ukanda huo.

Antoine Glaser, mtaalamu na mwandishi wa habari, anasema: "Kuna mambo ya Ufaransa na Magharibi ambayo kwa sasa yapo hatarini."

Kimsingi ni kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, Niger imekuwa kitovu cha juhudi za nchi za Magharibi za kisingizio cha kupambana na ugaidi, na kwa upande mwingine, nchi za Magharibi zinajaribu kuzuia ushawishi unaoongezeka wa Russia katika eneo hilo kwa kuanzisha vituo vya kijeshi na kuweko huko kwa visingizio mbalimbali kama vile kusaidia kupambana na ugaidi. Kwa sababu hii, Marekani ililaani haraka mapinduzi ya Niger na kutaka Rais aliyepinduliwa Muhammad Bazoum aachiliwe huru.

 

Wamagharibi wana wasiwasi kuwa, kupoteza nafasi na maslahi yao nchini Niger, hilo litarahisisha na kufungua zaidi njia ya kuchukua wigo mpana ushawishi wa Russia barani Afrika. Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana, baadhi ya serikali zinazofungamana na Magharibi katika eneo hilo zimetishia kuweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Niger na ikiwezekana kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya nchi hiyo masikini. Wakati huo huo, serikali mpya ya Niger imeonya kwamba itakabiliana na mipango yoyote ya kichokozi na uvamizi.

Vyovyote itakavyokuwa, matukio baada ya mapinduzi nchini Niger yamesababisha hali ya wasiwasi na kuwa tete hali ya usalama wa kisiasa katika kanda na kusababisha kuimarika kwa ushindani kati ya mataifa yenye nguvu nje ya kanda, ushindani ambao unaweza kuwa na taathira hasi kwa nchi maskini za Afrika, ikiwa ni pamoja na Niger.