Niger yasimamisha matangazo ya France 24 na RFI
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i100666-niger_yasimamisha_matangazo_ya_france_24_na_rfi
Serikali ya mpito ya kijeshi ya Niger imetangaza kusitisha nchini humo matangazo na shughuli za redio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 zinazofadhiliwa na serikali ya Ufaransa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 04, 2023 04:37 UTC
  • Niger yasimamisha matangazo ya France 24 na RFI

Serikali ya mpito ya kijeshi ya Niger imetangaza kusitisha nchini humo matangazo na shughuli za redio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 zinazofadhiliwa na serikali ya Ufaransa.

Serikali ya kijeshi ya Niger imechukua hatua hiyo baada ya kuvituhumu vyombo hivyo vya habari vya Ufaransa kuwa vinaripoti habari za uwongo na za kipropaganda.

Jeshi hilo limesema kuwa, taarifa zilizorushwa na France 24 na redio RFI zinakusudia kuvuruga mabadiliko ya kisiasa huko Niger, kuwavunja moyo wananchi na kuwashawishi walidharau jeshi la nchi hiyo ya Kiafrika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imetiwa kiwewe na uamuzi huo wa wanajeshi wa Niger walioongoza mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Mohamed Bazoum wa nchi hiyo ya Kiafrika mnamo Julai 26.

Maandamano dhidi ya Ufaransa na US nchini Niger

Uhusiano kati ya nchi mbili za Niger na Ufaransa uliharibika zaidi kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya karibuni na matamshi ya viongozi wa Paris juu ya matukio hayo; huku hisia za chuki dhidi ya Ufaransa zikiongezeka katika eneo la Sahel.

Hapo jana maelfu ya wananchi wa Niger walifanya maandamano katika mji mkuu Niamey, wakitaka kufukuzwa nchini humo mara wanajeshi wa Marekani na Ufaransa.

Waandamanaji hao wamesema taifa hilo linapaswa liachwe lijiendeshee mambo yake, na kuzitaka nchi za Magharibi kukoma kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo.