Viongozi wa mapinduzi Niger waishutumu Ufaransa kwa kukiuka anga ya nchi hiyo
Baraza la kijeshi la viongozi wa mapinduzi nchini Niger limeishutumu Ufaransa kuwa imekiuka anga iliyofungwa ya nchi hiyo.
Viongozi wa baraza hilo wameituhumu Ufaransa kuwa inayumbisha usalama na amani ya nchi hiyo, na kusema kuwa ndege ya Ufaransa imekiuka anga ya Niger iliyofungwa na baraza la kijeshi siku chache zilizopita.
Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Taifa la Wokovu la Niger, "Ufaransa imewaachilia huru wafungwa magaidi," na kueleza kwamba, "magaidi waliachiliwa na Ufaransa walishiriki katika mkutano wa kupanga mashambulizi kwenye vituo vya kijeshi katika eneo la mpaka wa pamoja wa nchi tatu za Niger, Burkina Faso na Mali.
Kanali Amadou Abdramane, msemaji wa "Baraza la Ulinzi wa Nchi" lililoundwa na viongozi wa mapinduzi ya Niger, amesema kuwa vikosi vya jeshi la Ufaransa vimekiuka anga ya Niger na kuwaachilia magaidi, suala ambalo limepelekea maeneo ya Walinzi wa Kitaifa kukabiliwa na mashambulizi ya "kigaidi".
Wakati huo huo, chanzo cha serikali ya Nigeria kimesema kuwa baraza la kijeshi nchini Niger limekutana na wajumbe wawili wa Rais wa Nigeria ambaye pia ni mkuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Bola Tinubu katika mji mkuu wa Niger jana, Jumatano.
Mkutano huo wa jana ulifanyika kabla ya mkutano wa kilele wa kundi la ECOWAS unaotazamiwa kufanyika leo, Alhamisi.
Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa ECOWAS, alisema Jumanne iliyopita kwamba diplomasia inasalia kuwa "njia bora" ya kufuatwa katika mzozo wa Niger, bila kutupilia mbali uwezekano wa kutumia nguvu kijeshi.
Awali ECOWAS iliwataka wanajeshi waliompindua Mohamed Bazoum kumrejesha madarakani rais huyo wa Niger ndani ya siku saba, kipindi ambacho kilimalizika Jumapili iliyopita, la sivyo watakabiliwa na nguvu za kijeshi ili kurejesha 'utawala wa kikatiba'.