Niger yawataka wanajeshi wa mkoloni Ufaransa waondoke nchini humo haraka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i101686-niger_yawataka_wanajeshi_wa_mkoloni_ufaransa_waondoke_nchini_humo_haraka
Serikali ya Niger imetoa amri kwa wanajeshi wa mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa wafungashe virago na toke nchini humo haraka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 31, 2023 03:23 UTC
  • Niger yawataka wanajeshi wa mkoloni Ufaransa waondoke nchini humo haraka

Serikali ya Niger imetoa amri kwa wanajeshi wa mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa wafungashe virago na toke nchini humo haraka.

Shirika la habari la IRNA limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, serikali mpya ya Niger imewataka wanajeshi wa Ufaransa wawe wameondoka nchini humo ifikapo tarehe 3 mwezi ujao wa Septemba, yaani katika kipindi cha siku chache zijazo.

Mgogoro baina ya Niger na mkoloni Mfaransa umepamba moto katika siku za hivi karibuni. Kabla ya hapo serikali ya Niger ilikuwa imetoa amri kwa ofisi za kibalozi wa Ufaransa ziondoke nchini humo katika kipindi cha saa 48 lakini Ufaransa ilikataa kuondoka kwa madai kuwa haiitambui serikali iliyoko madarakani. 

Siku chache zilizopita kuliripotiwa kuwa, serikali ya mpito nchini Niger ilizikata maji na umeme balozi za Ufaransa katika mji mkuu Niamey na ubalozi mdogo wa dola hilo la kikoloni ulioko Zinder na kupiga marufuku kupelekwa chakula kwenye balozi hizo.

Wananchi wa Niger wakiandamana kuunga mkono wanajeshi na kutimuliwa Wafaransa

 

Taarifa ya hiyo iliongeza kuwa, Mkuu wa Kamati ya Taifa ya Msaada ya Baraza la Taifa la Kulinda Nchi (CNSP), Elh Issa Hassoumi Boureima, amewataka washirika wote wa vituo vya Ufaransa nchini Niger kusimamisha usambazaji wote wa maji, umeme na bidhaa za chakula.

Vilevile alisema, mtu au upande wowote utakaoendelea kuwasaidia Wafaransa katika kusambaza bidhaa na huduma zozote zile watahesabiwa kuwa ni "maadui wa watu huru wa Niger."

Taarifa nyingine zilisema kuwa, maelfu ya wananchi wa Niger wamefanya maandamano karibu na kambi ya jeshi la Ufaransa katika mji mkuu Niamey kwa lengo la kutangaza uungaji mkono wao kwa serikali ya kijeshi na kutaka wanajeshi wa Ufaransa waondoke mara moja katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Waandamanaji hao walikusanyika karibu na kambi ya jeshi la Ufaransa katika mji mkuu siku ya Jumapili na kupeperusha bendera za Niger na kubeba mabango yenye kaulimbiu za kuipinga Ufaransa kama zinazosema: "Hatutaki jeshi la Ufaransa nchini Niger" na "Waache Wafaransa waondoke."