Polisi wa Niger wanaendelea kuzingira ubalozi wa Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i101746-polisi_wa_niger_wanaendelea_kuzingira_ubalozi_wa_ufaransa
Polisi nchini Niger wanaendelea kuzingira majengo ya ubalozi wa Ufaransa mjini Niamey, huku Baraza la Kijeshi linalotawala nchi hiyo likichukua uamuzi wa kupiga marufuku shughuli za mashirika ya kimataifa na yasiyo ya kiserikali.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 02, 2023 02:44 UTC
  • Polisi wa Niger wanaendelea kuzingira ubalozi wa Ufaransa

Polisi nchini Niger wanaendelea kuzingira majengo ya ubalozi wa Ufaransa mjini Niamey, huku Baraza la Kijeshi linalotawala nchi hiyo likichukua uamuzi wa kupiga marufuku shughuli za mashirika ya kimataifa na yasiyo ya kiserikali.

Ubalozi wa Ufaransa nchini Niger uko chini ya hatua kali za kiusalama baada ya uamuzi wa Baraza la Kijeshi kumtimua balozi wa Ufaransa na familia yake nchini humo. Jeshi la Ufaransa limeonya dhidi ya hatua yoyote itakayokuwa na madhara kwa wanajeshi au wanadiplomasia wa nchi hiyo huko Niger.

Wakati huo huo, utawala wa kijeshi nchini Niger umetangaza kusimamisha shughuli zote za mashirika ya kimataifa na yasiyo ya kiserikali, na vilevile mashirika ya Umoja wa Mataifa katika "maeneo ya operesheni" za kijeshi kutokana na "masuala ya kiusalama."

Kwa miaka mingi, Niger imekuwa ikikabiliwa na machafuko yanayofanywa na makundi yenye silaha katika mikoa ya kusini-magharibi iliyo karibu na mipaka ya Burkina Faso na Mali, na katika mikoa ya kusini mashariki karibu na bonde la Ziwa Chad na mpaka na Nigeria.

Wanajeshi waliomuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum walitaja "kuzorota hali ya usalama" kama miongoni mwa sababu zilizohalalisha mapinduzi yao.

Itakumbukwa kuwa, Baraza la Taifa kwa ajili ya Ulinzi wa Watani, (National Council for the Safeguard of the Homeland, CNSP) ambalo liliundwa hivi majuzi na viongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Niger, limeitaka Ufaransa ihakikishe kuwa ifikapo Septemba 3, iwe imeshaondoa vikosi vya jeshi lake vilivyoko nchini humo.

Tarehe 26 Julai 2023, walinzi wa rais wa Niger walifanya mapinduzi dhidi ya rais wa nchi hiyo, Mohamed Bazoum; na mkuu wa walinzi hao, Jenerali Abdourahamane Tchiani, alijitangaza kuwa kiongozi mpya wa nchi na mkuu wa baraza la mpito.