Sep 04, 2023 12:57 UTC
  • Al Burhan atembelea Juba huku vita vikiendelea nchini Sudan

Rais wa Baraza la Utawala wa Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan, mapema leo alikuwa Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini, kwa ziara rasmi ya siku moja, kujadili hali ya Sudan na uhusiano kati ya nchi hizo mbili, huku mapigano makali yakiendelea kuripotiwa nchini kwake.

Baraza la Utawala wa Mpito limesema katika taarifa yake kwenye Facebook kwamba, katika mazungumzo yake na Rais Salva Kiir Mayardit, Al Burhan amejadili uhusiano wa pande mbili, njia za kustawisha ushirikiano kati ya nchi hizo na maslahi ya pamoja.

Hii ni ziara ya pili rasmi ya Al-Burhan nje ya nchi tangu kuanza kwa mapigano kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka mwezi Aprili mwaka huu.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti, Abdel Fattah al Burhan alifanya ziara nchini Misri na kukutana na viongozi wa nchi hiyo.

Ziara ya Al Burhan nchini Sudan Kusini inafanyika huku mapigano makali yakiedelea nchini Sudan. Jana, Jumapili, mapigano kati ya pande hizo mbili yaligharimu maisha ya zaidi ya watu 23 katika maeneo ya Al-Khudir na Karari huko Omdurman, na karibu na Hospitali ya Al-Raqi, kusini mwa Khartoum.

Ripoti zinasema, jeshi la Sudan (SAF) limezidisha mashambulizi ya anga na ya mizinga kwenye maeneo ya Kikosi cha Wanajeshi wa Msaada wa Haraka (RSF) katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.

Umoja wa Mataifa umesema mapigano makali yanayoendelea kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) yamelazimisha watu karibu mamilioni tano kuyahama makazi yao.

Tags