Apr 01, 2024 02:17 UTC
  • Ufaransa, Misri na Jordan zapinga shambulio la Rafah na kuunga mkono usitishaji vita Gaza

Mkutano wa pande tatu wa mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Jordan na Ufaransa ulifanyika Jumamosi Cairo, mji mkuu wa Misri, kuhusiana na matukio ya hivi karibuni katika vita vya Gaza na mashauriano ya kusitisha mapigano hayo.

Katika mkutano huo, Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Ayman Safadi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan na Stéphane Sjourney, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa walishauriana kuhusu matukio ya Ukanda wa Gaza na kujadili matokeo ya vita katika ukanda huo.

Kuharibiwa Gaza

Mawaziri hao walitoa wito wa kuwepo usitishaji vita wa kudumu katika Ukanda wa Gaza,  kubadilishana mateka na kutangaza upinzani wao dhidi ya kufanyika mashambulizi yoyote ya kijeshi huko Rafah, ambayo inawahifadhi wakimbizi milioni 1.5 wa Kipalestina. Walitahadharisha kuhusu matokeo mabaya ya hali ya kibinadamu na njaa na kuporomoka mfumo wa afya huko Gaza na kusisitiza upinzani wao dhidi ya jaribio lolote la kuwahamisha kwa nguvu watu wa Palestina. Mawaziri hao wa mambo ya nje wa Misri, Jordan na Ufaransa pia walisisitiza juu ya utekelezaji wa suluhisho la "serikali mbili" kwa kuzingatia maazimio ya Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na kuundwa taifa huru la Palestina, linalojitawala ndani ya mipaka ya 1967.

Kutangazwa msimamo huo wa Ufaransa ikiwa ni nchi ya pili muhimu katika Umoja wa Ulaya pembeni ya Misri na Jordan ambazo ni majirani wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa namna fulani kunaakisi matakwa ya kimataifa kuhusu vita vya Gaza. Huku vita hivyo vikiwa mwishoni mwa mwezi wake wa sita, viongozi wa utawala wa Kizayuni hususan Benjamin Netanyahu bado wanasisitiza misimamo yao ya kivita na hata kuvuruga mazungumzo ya usitishaji vita ili wafikie lengo la kuishambulia Rafah kwa madai eti ya kuangamiza makundi ya muqawama wa Palestina hususan Hamas.

Israel, ikiwa imepata alama ya taa ya kijani kutoka Marekani ambayo ni muungaji mkono wake mkuu, na ambayo katika kipindi chote cha vita imepokea misaada mikubwa ya kisiasa, kiuchumi, na kijeshi kutoka Washington, inahusika waziwazi katika mauaji ya halaiki ya wakaazi wa Gaza na kukiuka haki zao za kimsingi kabisa za binadamu, ikiwa ni pamoja na kuwaweka njaa kwa makusudi. Hali hii imepelekea watoto wengi wachanga kufa njaa.

Mashirika yanayohusiana na Umoja wa Mataifa yameonya kuwa huenda balaa la njaa likalikumba eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza mwezi ujao na kuenea katika maeneo mengine ya ukanda huo ifikapo Julai. Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema "ukosefu wa usalama, kutoshirikiana Israel, uhaba wa malori na mafuta" ni "changamoto kubwa" katika juhudi za kusambaza misaada huko Gaza.

Misafara ya misaada ya kibinadamu imezuiwa na utawala wa Kizayuni kuingia Gaza

Kuendelea kuharibika hali ya Ukanda wa Gaza sambamba na kuendelea mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni katika eneo hilo ambalo lina msongamano mkubwa zaidi wa watu duniani, kumepelekea kuongezeka maombi ya kushughulikiwa haraka hali ya kibinadamu na kufunguliwa njia za kufikishwa misaada ya dharura katika eeo hilo. Kuhusiana na hilo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetahadharisha kuhusu baa la njaa huko Gaza na kutaka mashinikizo yaongezwe dhidi ya utawala wa Kizayuni ili utekeleze hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu ufikishaji wa misaada ya kibinadamu katika ukanda huo.

Pamoja na hayo, Kamishna Mkuu wa UNRWA amefichua kuwa Israel imeliambia shirika hilo kuwa haitakubali kutumwa misafara ya misaada ya kibinadamu kaskazini mwa Gaza. Hivi karibuni UNRWA ilisema kuzuiwa misaada ya kibinadamu kuingia huko Gaza kunahatarisha pakubwa maisha ya wakazi wa ukanda huo.

Tags