Nov 26, 2023 02:24 UTC
  • Ghana ni kituo kinachoongoza kwa bidhaa za Iran zinazouzwa barani Afrika

Msemaji wa Kamisheni ya Ustawi wa Biashara ya Chama cha Viwanda, Madini na Biashara cha Iran ametangaza kuwa, Ghana ni kituo cha kwanza kinachoongoza kwa bidhaa za Iran zinazopelekwa barani Afrika.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina mtazamo wa upande mmoja tu wa kujali nchi za Ulaya, kwa sababu mabara ya Afrika na Asia yanatiliwa mkazo pia na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
 
Soko kubwa la Afrika ni uwanja mwafaka wa uuzaji bidhaa za Iran; na kutokana na hali hiyo, bara hilo lina nafasi maalumu katika sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
 
Kwa mujibu wa IRNA, Seyed Ruhollah Latifi, msemaji wa Kamisheni ya Ustawi wa Biashara ya Chama cha Viwanda, Madini na Biashara cha Iran, amesema kuhusu rekodi ya biashara kati ya Iran na Afrika kwamba, Ghana imekuwa kituo kinachoongoza kwa bidhaa za Iran zinazopelekwaa barani humo katika kipindi cha miezi saba kuanzia Machi 21 hadi Oktoba 22 mwaka huu, ambapo bidhaa zenye thamani ya dola milioni 434 zilisafirishwa kuelekea nchi 38 za Afrika na bidhaa zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 47 ziliingizwa hapa nchini kutoka nchi 19 za bara hilo.

Latifi ameongeza kuwa kiwango hicho ni punguo la 33% katika uzito wa bidhaa na 53% katika thamani yake ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Msemaji wa Kamisheni ya Ustawi wa Biashara ya Chama cha Viwanda, Madini na Biashara cha Iran amesema kuhusu vituo zinakopelekwa bidhaa za Iran katika bara la Afrika kwamba, Ghana ni kituo kilichoongoza kwa mauzo ya bidhaa za Iran katika kipindi hicho kwa ununuzi wa bidhaa zenye thamani ya dola milioni 116.3, ikifuatiwa na  Afrika Kusini iliyonunua bidhaa zenye thamani ya dola milioni 89. 5, Tanzania dola milioni 61.4, Nigeria dola milioni 46.5, Msumbiji dola milioni 40, Kenya dola milioni 28.3, Somalia dola milioni 16.5, Sudan dola milioni 7.1, Libya dola milioni 5.5, Djibouti dola milioni 5.1, Algeria dola milioni 4.9, Kongo dola milioni 3.4 na Cote d'Ivoire dola milioni 3.4.../

Tags