Dec 28, 2023 06:39 UTC
  • Idadi ya walioaga dunia katika mripuko wa lori la mafuta Liberia yaongezeka

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika mripuko wa lori la mafuta uliotokea katikati ya Liberia imeongezeka na kufikia watu 40.

Francis Kateh, Afisa Mkuu wa Afya wa nchi hiyo aliliambia shirika la habari la Reuters jana Jumatano kuwa, makumi ya watu wengine wamejeruhiwa kwenye mkasa huo uliotokea baada ya lori la mafuta kupinduka na kuanguka kwenye mtaro kando ya barabara mjini Totota, Kaunti ya Bong.

Kateh amesema yumkini idadi ya wahanga wa ajali hiyo ya Jumanne ikaongezeka kutokana na hali mbaya ya mejeruhiwa waliolazwa hospitalini.

Aidha Afisa wa Afya wa Kaunti ya Bong, Dakta Cynthia Blapooh ameliambia gazeti linalochapishwa nchini humo la Front Page Africa kwamba, "Bado tuna wagonjwa wengi waliojeruhiwa vibaya wakiwemo watoto na mwanamke mjamzito. Tumepokea jumla ya majeruhi 36."

Ramani ya Liberia

Kwa upande wake, Malvin Sackor, afisa wa polisi katika eneo hilo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "Lori la mafuta lililokuwa limesheheni petroli lilipinduka na watu katika eneo hilo wakaanza kuchota mafuta, hali iliyopelekea lori hilo kuripuka na kuua na kujeruhi watu wengi."

Naye Aaron Massaquoi, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, lori hilo la mafuta liliposhika moto baada ya kuripuka, watu waliokuwa juu yake wakijaribu kuchota mafuta waliungua kiasi cha kutotambulika.

Miundumbinu mibovu na upuuzaji wa sheria za usalama barabarani vimeifanya Liberia kuwa moja ya nchi za chini ya eneo la jangwa la Sahara barani Afrika zinazapoteza maelfu ya watu katika ajali za barabarani kila mwaka.

Tags