UN: Maelfu wanahitaji msaada wa dharura DRC kutokana na mafuriko
Umoja wa Mataifa umesema mamia ya maelfu ya watu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanahitaji msaada wa dharura kutokana na athari za mafuriko katika pembe mbali mbali za nchi hiyo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha yameathiri watu zaidi ya 330,000.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema taasisi 9 kati ya 12 za nchi hiyo zimeathiriwa na mafuriko hayo yaliyoharibu hospitali na taasisi za afya, shule na hata mashamba ya kilimo.
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani imebainisha kuwa: Mafuriko hayo nchini DRC yamebomoa vituo 34 vya afya, skuli 120 na nyumba zaidi ya 64,000.
Wizara ya Masuala ya Kijamii ya nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika ilisema hivi karibuni kuwa, watu zaidi ya 300 wameaga dunia katika mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa za msimu nchini humo.

Serikali ya DRC imetoa wito wa kutolewa fedha haraka za kuwasaidia waathiriwa wa mvua na mafuriko hayo, huku aikiasa pia mshikamano wa kimataifa wa kuzisaidia timu za misaada ya kibinadamu zinazoendesha shughuli zao hivi sasa ndani ya maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo.
Mafuriko na maporomoko ya ardhi ni vitu vya kawaida huko DRC wakati wa msimu wa mvua, ambao huanza Septemba hadi Mei. Mwezi Mei mwaka jana, takwimu zilizotolewa Kongo DR zilisema kuwa idadi ya watu walioaga dunia kufuatia janga la mafuriko na maporomoko ya udongo mashariki mwa nchi hiyo ilifikia 438.