Mar 13, 2024 07:44 UTC
  • Kenya yaakhirisha mpango wa kutuma askari polisi Haiti

Kenya imetangaza habari ya kuakhirisha mpango wake wa kutuma kikosi cha askari polisi 1,000 nchini Haiti, kufuatia kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini, Ariel Henry.

Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Korir Sing’oei amesema kufuatia mabadiliko ya kisiasa yaliyojiri nchini Haiti, serikali ya Nairobi imesimamisha mpango wa kutuma maafisa wake nchini humo.

Korir amesema, "Kenya itasubiri hadi pale fremu ya Katiba ya Haiti itakapopata misingi madhubuti tena, kabla ya kuchukua hatua yoyote ile."

Mwishoni mwa mwezi Februari, Waziri Mkuu huyo wa Haiti aliyejiuzulu, Ariel Henry aliitembelea Kenya ambapo akiwa ameandamana na Rais William Ruto wa nchi hiyo, walishuhudia kutiwa saini mapatano ya kutumwa askari polisi wa Kenya watakaoongoza kikosi cha kimataifa cha kukabiliana na magenge nchini Haiti, chini ya uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa.

Henry, ambaye aliingia madarakani baada ya kuuawa Rais Jovenal Moise wa Haiti, alikuwa ameahidi kuondoka madarakani mapema mwezi Februari, lakini baadaye akasema lazima kwanza usalama uimarishwe upya ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki unafanyika. 

Rais Ruto alipompokea Ariel Henry, Waziri Mkuu wa Haiti aliyejiuzulu

Ghasia za magenge zimeikumba Haiti kwa miaka mingi, lakini zimeongezeka zaidi tangu kuuawa Rais Jovenel Moise mnamo 2021. Umoja wa Mataifa unakadiria mzozo huo ulisababisha vifo vya takriban watu 5,000 mwaka jana na kupelekea wengine 300,000 kuhama makazi yao, huku kukiwa na uhaba wa chakula na huduma za matibabu.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa siku chache zilizopita alisema nchi tano zimeuarifu rasmi Umoja wa Mataifa kuhusu nia yao ya kuchangia maafisa katika kikosi cha kimataifa cha kurejesha usalama Haiti, ambacho Henry aliomba kitumwe katika nchi hiyo mwaka 2022. Haiti ni kati ya nchi maskini zaidi duniani na maskini zaidi katika bara la Amerika.

Tags