Uganda haitatuma UPDF S/Kusini huku KQ ikisimamisha safari za ndege Juba
Jeshi la Ulinzi la Uganda UPDF limesema halitatuma askari wake kwenda kudhibiti hali ya mambo nchini Sudan Kusini, muda mfupi baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzitaka nchi za kanda ya Afrika Mashariki kuingilia kati na kusuluhisha mgogoro na mapigano mapya yaliyozuka nchini humo.
Msemaji wa UPDF Luteni Kanali Paddy Ankunda amekanusha madai kuwa Uganda inajiandaa kutuma wanajeshi wake huko Sudan Kusini kama ilivyofanya Disemba mwaka 2013, kutokana na kushtadi mapigano na mauaji katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika, hususan katika mji mkuu Juba. Jana Jumapili, Baraza la Usalama liliizitaka nchi ambazo ni jirani na Sudan Kusini kuupatia ufumbuzi mzozo huo mpya unaoaminika kuwa wa kisiasa.
Wakati huohuo, Msemaji wa Ikulu ya Nairobi Manoah Esipisu amesema Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amewasiliana na Rais Salva Kiir na kumuomba ashirikiane na makamu wake Dakta Riek Machar kukomesha mapigano hayo. Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) limesimamisha safari zake za ndege mjini Juba, likihofia mapigano hayo. Shirika hilo huwa na safari tatu za ndege kutoka Nairobi hadi Juba kwa siku. Mapigano hayo baina ya askari wanaomuunga mkono Machar kwa upande mmoja na waitifaki wa Kiir kwa upande mwingine, yamesababisha watu zaidi ya 270 kuuawa tangu yalipoanza Ijumaa iliyopita.