Maafisa sita wa polisi Kenya wauawa katika hujuma ya kigaidi
Maafisa wasiopungua sita wa polisi wanaripotiwa kuuawa nchini Kenya baada ya gaidi kushambulia kituo cha polisi katika eneo la Kapenguria katika kaunti ya Pokot Magharibi inayopakana na Uganda.
Duru zinaarifu gaidi huyo anayeshukiwa kuwa mfuasi wa kundi la Al Shabab aliingia katika kituo hicho cha polisi na kumpokonya silaha mmoja kati ya maafisa waliokuwa hapo na kisha kuanza kufyatua risasi kiholela.
Maafisa wasiopungua sita wa polisi wanaripotiwa kuuawa. Inasemekana gaidi huyo alifika kituoni hapo kumuokoa mwenzake aliyekamatwa kwa kushukiwa kuwa ni gaidi.
Inspetka Jenerali wa Polisi Kenya Joseph Boinnet ametihbitisha kutokea tukio hilo na kusema maafisa zaidi wametumwa katika eneo hilo. Baadhi ya duru zinasema gaidi huyo amewateka nyara maafisa kadhaa wa polisi.
Kenya imekuwa ikikumbwa na hujuma za kundi la kigaidi la Al Shabab ambalo hushambulia maeneo mbali mbali ya nchi hiyo. Kundi la Al Shabab lenye makao yake Somalia linapinga kuwepo jeshi la Kenya Somalia. Serikali ya Kenya ilituma jeshi lake Somalia kukabiliana na kundi la Al Shabab ambalo lilikuwa likishambulia maeneo ya kitalii nchini humo.