Jun 16, 2024 06:08 UTC
  • Rais wa Malawi aitangaza Jumatatu kuwa siku ya mapumziko kwa ajili ya maziko ya Makamu wa Rais

Rais Lazarus Chakwera wa Malawi ameitangaza Jumatatu ya kesho ya Juni 17 kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa ili kuruhusu raia wa Malawi kuhudhuria au kufuatilia, maziko ya Makamu wa Rais wa nchi hiyo Saulos Chilima aliyefariki dunia katika ajali ya ndege siku ya Jumatatu iliyopita ya Juni 10.

Waziri wa Habari na Uwekaji wa Kidijitali wa Malawi, Moses Kunkuyu alitoa tangazo jana Jumamosi katika mkutano na waandishi wa habari huko Lilongwe, mji mkuu wa Malawi, wakati alipoutangazia umma kuhusu ratiba ya kitaifa ya mazishi ya makamu wa rais.

Mwili wa Chilima umepangwa kuzikwa Jumatatu kijijini kwao Ntcheu, takriban kilomita 165 kusini mwa Lilongwe.

Wakati huo huo, viongozi kadhaa wa kigeni wamethibitisha kuhudhuria maziko hayo. 

Jana Jumamosi, mwili wa Chilima ulipelekwa katika Jengo la Bunge Jipya mjini Lilongwe. Ratiba zilizokuwa zinaonesha kuwa, mwili huo ungepelekwa katika Uwanja wa Taifa wa Bingu, mjini Lilongwe, wenye uwezo wa kuchukua watu 40,000, kwa ajili ya wananchi kutoa heshima zao za mwisho kwa Chilima, kabla ya kupelekwa kijijini kwao Ntcheu kwa maziko kesho Jumatatu.

Chilima, pamoja na maafisa wengine wanane, akiwemo Mke wa Rais wa zamani wa nchi hiyo Patricia Shanil Dzimbiri, walikuwa wanaelekea kwenye mazishi ya aliyekuwa mwanasheria mkuu na waziri wa sheria, Ralph Kasambara, ajali hiyo ilipotokea kutokana na hali mbaya ya hewa kama taarifa rasmi zilivyosema. 

Rais Chakwera ametangaza siku 21 za maombolezo. Katika kipindi hicho, bendera za taifa zitapepea nusu mlingoti na hakutakuwa na sherehe zozote nchi nzima katika kipindi hicho cha siku 21.

Tags