Utekaji nyara watu nchini CAR waongezeka na kuogofya raia
Asasi za kiraia nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati zimeonyesha wasi wasi wake kufuatia zaidi ya watu 300 kutekwa nyara na wabeba silaha nchini humo.
Taasisi ya Invisible Children na The Resolve kwa pamoja zilitangaza jana kwamba, kwa kipindi cha miezi sita ya mwaka huu wa 2016, jumla ya watu 344 wakiwemo watoto 65 wametekwa nyara na waasi wa Kikristo wa Anti-Balaka. Kwa mujibu wa taasisi hizo, idadi ya watu ambao wametekwa nyara nchini humo tangu mwaka 2010, haina mfano wake.
Kadhalika taasisi hizo zimetangaza kuwa, hadi sasa baadhi ya watu miongoni mwa idadi hiyo bado wanaendelea kushikiliwa na wanachama wa kundi hilo. Kwa upande wake Sean Poole mkuu wa taasisi ya kimataifa ya watoto ameitaka jamii ya kimataiafa kusaidia kuwalinda raia kutokana na hujuma za makundi ya waasi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Nchi hiyo ilitumbukia katika machafuko mwaka 2013 baada ya makundi ya waasi kumfurusha aliyekuwa raia wa nchi hiyo François Bozizé.